Mambo ya kufanya ng’ombe wako watoe maziwa mengi

Kulisha ng’ombe kwa kutumia aina yoyote ya malisho haitoshi kukuhakikishia ng’ombe kuwa na afya nzuri na kutoa maziwa ya kutosha.

Kama ilivyo kwa binadamu, ng’ombe anahitaji mlo kamili. Malisho ni lazima yawe na uwiano sahihi wa viungo.

Mifugo inahitaji chakula kitakachowapa nguvu, protini, madini, na vitamin ili kujenga miili yao, kuzalisha maziwa, na kuzaliana.

Wanyama wadogo wanahitaji virutubisho vya kutosha, ili wakue na kuongeza uzito.

Ng’ombe wa maziwa wanahitaji virutubisho zaidi ili kuweza kuzalisha maziwa kwa wingi hasa katika kipindi cha miezi 3-4 ya mwanzo baada ya kuzaa, wakati ambao uzalishaji wa maziwa unakuwa juu.

Malisho ya kijani ni mlo mkuu kwa mifugo

Mlo muhimu na wenye virutubisho kwa mifugo ni majani. Lakini malisho bora ya kijani ni yale yanayoweza kumpatia ng’ombe wa maziwa virutubisho muhimu vinavyohitajika.

Malisho bora yanakuwa na sifa mbili muhimu: ni ya kijani kibichi na machanga, hii ina maana kuwa, majani ya malisho ni lazima yakatwe na kuhifadhiwa yakiwa bado machanga kabla ya kuchanua.

Ni lazima mfugaji afahamu kuwa mimea ambayo imepoteza rangi yake halisi ya kijani inaweza tu kuwasaidia mifugo kuishi lakini haina virutubisho muhimu vya kuwapa mifugo nguvu, madini, protini na haiwezi kusaidia katika uzalishaji wa maziwa.

Malisho yenye viwango vya chini vya virutubisho ni lazima yaongezewe kwa chakula cha ziada chenye virutubisho vya kutosha kitakachoziba pengo la virutubisho vilivyokosekana.

Vyakula vya kutia nguvu

Aina zote za majani ni chanzo kizuri cha vyakula vya kutia nguvu kwa mifugo, endapo tu yatalishwa yakiwa bado machanga.

Majani yaliyo maarufu kwa malisho ni pamoja na matete, ukoka, majani ya tembo, seteria na guatemala.

Majani ya mahindi au mtama ni chakula kizuri sana kwa kuwapa nguvu mifugo. Vyakula vya kutia nguvu vilishwe kwa kiasi kidogo. Vyakula hivi vinaweza kutokana na aina zote za nafaka, punje za ngano, au molasesi.

Vyanzo vya protini

Kanuni ya 1: Mimea michanga ina kiasi kikubwa cha protini kuliko mimea iliyokomaa.

Mahindi machanga pamoja na majani ya viazi vitamu ni mahususi kwa protini.

Kanuni ya 2: Mikunde ina protini nyingi zaidi kuliko nyasi. Mfano mabaki ya majani ya maharage, njegere, desmodium na lusina.

Majani yanayotokana na mimea kama lusina, calliandra au sesbania ina kiwango kikubwa cha protini pia.

Ng’ombe wasilishwe kwa kutumia aina zote za jamii ya mikunde kwa zaidi ya asilimia 30 ya uwiano wa mchanganyiko wa malisho ili kuepuka matatizo ya kiafya. Aina nyingine ya vyakula vyenye protini ni mashudu ya pamba, mashudu ya alizeti na soya.

Madini

Mifugo inahitaji madini ya ziada. Ni lazima yapatikane muda wote, mfano kama jiwe la chumvi. Wanyama wanaokuwa, wenye mimba, na ng’ombe anayenyonyesha wanahitaji kiasi kikubwa cha madini kama vile kalshiamu na fosforasi. Mimea ya jamii ya mikunde na mengineyo isipokuwa nyasi inatoa kiasi kikubwa cha lashiamu na madini mengineyo.

Tumia kiasi kidogo cha pumba

Pumba aina ya Dairy meal ina kiwango kikubwa sana cha madini. Lakini ina madhara kwa mifugo endapo wanyama watalishwa kwa kiwango kikubwa. Malisho yanayotokana na majani au nyasi kavu ni lazima yabakie kuwa chakula kikuu kwa mifugo.

Haishauriwi kulisha zaidi ya kilo sita za pumba kwa siku kwa ng’ombe mwenye kilo 450. Ni lazima wapewe kwa kiwango kidogo sana, ambacho si zaidi ya kilo mbili kwa mara moja na kichanganywe na majani.

Kuongeza kiwango cha pumba kabla na wakati wa kunyonyesha/kukamuliwa, kisizidi kiasi cha kilo mbili kwa wiki ili tumbo la mnyama lizoee. Wafugaji wazoefu huongeza majani ya malisho na mbaazi kwenye lishe ya mifugo. Wanaweza hata kuacha pumba kwa muda au kupunguza matumizi ya pumba kupitia njia hii.

Utafiti unaonyesha kuwa kilo tatu za malisho ya Majani na chakula jamii ya mikunde kama vile Desmodium au majani ya viazi vitamu hutoa maziwa sawa na kilo moja ya pumba. Kwa hivyo, mfugaji anaweza kuokoa fedha akilisha ng’ombe wake kwa kutumia chakula cha jamii ya mikunde badala ya kununua aina nyingine ya virutubisho.

Makala haya kwa hisani ya mtandao wa mkulima mbunifu.