Mambo ya kufanya unapopata ajira mpya

Muktasari:

  • Umesikia tangazo la nafasi ya kazi, umeomba kazi, umeitwa kwenye usaili wa kazi, umeshinda. Nini kinafuata baada ya kupata ajira? Unafahamu makosa yanayoweza kuwa mwanzo wa kupoteza kazi yako? Makala haya yanakusaidia kujua ufanye nini unapoingia kazini.

Mara baada ya kupata kazi, watu wengi hujisahau. Hufikiri kwa sababu tayari wameajiriwa, hawana sababu ya kufanya jitihada za kulinda kazi waliyopambana kuipata. Usipojua namna ya kulinda kazi uliyoipata huo unaweza kuwa mwanzo wa safari ya kupoteza ajira yako. Unahitaji kujifunza namna ya kulinda kazi uliyoipata.

Mara baada ya kuanza ajira mpya, kwa kawaida, unakuwa kwenye kipindi cha matazamio. Kulingana na mazingira ya kazi na matakwa ya mkataba, kipindi hiki kinaweza kuwa kati ya miezi mitatu mpaka miezi 12. Hata hivyo, wakati mwingine mwajiri huweza kuongeza urefu wa kipindi hiki cha matarajio ikiwa mwajiriwa hajaweza kufikia matarajio yake.

Kwa ujumla, hiki ni kipindi cha mwanzo kabisa kinachojenga uhusiano wa kikazi kati ya mwajiri na mwajiriwa. Mwajiri hukitumia kipindi hiki kujiridhisha ikiwa kweli alifanya chaguo sahihi katika usaili wa kazi. Mwajiriwa naye, hutumia kipindi hiki kuona ikiwa mazingira ya kazi yanafikia matarajio yake.

Kipindi cha matazamio kina umuhimu wake kwa sababu, tunafahamu, mchakato mzima wa kumwajiri mfanyakazi unaweza kuwa na upungufu. Pamoja na umakini wote wa kumpata mtu anayeaminiwa kuwa sahihi, bado inawezekana kabisa mwajiri akaishia kumpata mtu asiyeweza kukidhi vigezo vya kazi. Kipindi cha majaribio, kwa maana hiyo, kinajaribu kutoa nafasi nyingine ya mwajiri kujiridhisha na sifa na ujuzi wa mwajiriwa mpya kabla ya kumthibitisha kazini.

Katika kipindi hiki, mwajiriwa anakuwa hafungwi sana na mkataba alionao na mwajiri. Kwa mfano, wakati wa kipindi cha majaribio, mwajiriwa anaweza kuacha kazi bila kulazimika kufuata matakwa ya mkataba. Mwajiri naye anaweza kumwachisha kazi mwajiriwa mpya bila kulazimika kufuata matakwa ya mkataba wake na mwajiriwa.

Hata hivyo, kutokufungwa na mkataba hakumaanishi uhuru wa kumtendea mwajiriwa/mwajiri chochote bila kufuata taratibu za kazi. Katika mazingira ambayo mwajiri anafikiri hajaridhishwa na mwajiriwa mpya, analazimika kufutaa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya Mwaka 2004, kanuni za ajira na uhusiano kazini za Mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi ya Mwaka 2003 na marekebisho yake.

Makala haya yanasaili mambo ya kuzingatia unapokuwa kwenye kipindi hiki ili kukusaidia kufikia hatua ya kuthibitishwa kazini.

Kidhi matarajio ya mwajiri

Kazi yako ya kwanza mara baada ya kuajiriwa ni kumthibitishia mwajiri wako mpya kuwa kweli unao ujuzi uliouonyesha kwenye mchakato wa kukupata. Usifanye kosa la kujisahau ukajikuta unashindwa kufikia matarajio yake.

Katika kukusaidia kuelewa wajibu wako ni upi, mwajiri makini atakupa barua inayofafanua majukumu yanayoambatana na nafasi yako mpya pamoja na mkataba wa kazi. Soma nyaraka hizi na uzitunze vizuri kwa sababu ndizo zinazokulinda kwenye eneo la kazi.

Mwajiri naye, kwa upande wake, anao wajibu wa kuweka utaratibu mzuri wa kukuwezesha kutekeleza majukumu yako kwa viwango anavyovitarajia. Hiyo ni pamoja na kukufahamisha tunu na miiko ya nafasi ya kazi uliyopewa; mambo yatakayotazamwa katika kipindi cha majaribio; ujuzi unaotarajiwa kuwa nao na mpango utakaotumika kubaini changamoto za kazi zitakazojitokeza katika kipindi hicho.

Unapopata changamoto katika kipindi hiki, ni vizuri kushirikiana na afisa (idara ya) raslimali watu kazini kwako ili kuweza kupata ushauri na maelekezo yatakayosaidia kutekeleza majukumu yako vizuri.

Onyesha umakini kazini

Ufanisi katika kazi, kwa kiasi kikubwa, unategemea nidhamu. Namna gani wewe kama mwajiriwa mpya unaheshimu kazi yako kwa kuwahi kazini, kuwasilisha mrejesho wa kazi kwa muda uliopangwa hiyo ndiyo inaitwa nidhamu ya kazi.

Hakikisha unawahi kazini mapema. Kama ofisi ina utaratibu wa kusaini kitabu cha mahudhurio, usiache kusaini ndani ya muda uliopangwa. Usiwe mtu wa kukosa vikao vinavyoitishwa kazini. Unapokosekana kwenye vikao, ni rahisi kuonekana huna nidhamu ya kazi inayotakiwa.

Kadhalika, nidhamu ya kazi ni pamoja mpangilio mzuri wa jumla wa majukumu yako ya kila siku. Huwezi kupangilia majukumu yako kama huwezi kutunza muda wako vizuri. Amka mapema, anza safari ya kwenda kazini mapema.

Tumia kitabu cha kumbukumbu za kila siku kuainisha majukumu unayotakiwa kuyakamilisha kila siku. Unapofanya hivyo, utaweza kupima utendaji wako na hivyo kukamilisha na kukabidhi ripoti zako kwa muda unaotarajiwa. Kuchelewesha kazi si dalili nzuri kwa mwajiriwa mpya anayetakiwa kuthibitisha kuwa ana ari na weledi wa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Fahamu utamaduni wa taasisi

Kila eneo la kazi lina utamaduni wake. Huu ni utaratibu usio rasmi uliozoeleka katika taasisi ambao kila mmoja anajikuta akiufuata ingawa haujaandikwa kokote. Unawajibika kudadisi na kujua taasisi yako inaongozwa na utamaduni upi. Kwa mfano, kuna taasisi zisizoruhusu mavazi ya namna fulani kuvaliwa kazini. Kuwa mwepesi kujifunza mambo kama hayo.

Kadhalika, kila taasisi inaongozwa na ‘siasa’ zake za ndani na nje. ‘Siasa’ ni taratibu zisizo rasmi zinazongoza mahusiano baina ya wafanyakazi ndani ya taasisi, na namna taasisi inavyojenga taswira yake machoni pa jamii. Unalazimika kufanya kazi ya ziada kuzielewa.

Jenga uhusiano na watu

Huwezi kufanikiwa kama huna mahusiano mazuri na watu. Kumbuka watu uliowakuta kazini, hata kama umewazidi elimu, bado wana uzoefu kuliko wewe. Unapojenga mahusiano mazuri na watu hawa unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kupunguza makosa.

Tafiti kujua nani ana sauti ipi kwa wakati gani. Kuna watu hawa nyadhifa lakini wana nguvu kubwa kwenye taasisi. Ukiwafahamu itakusaidia kujua unaanzia wapi unapokuwa na wazo jipya.

Lakini pia hawakosekani watu wanaopenda majungu. Huhitaji muda mrefu kuwabaini watu wa namna hii na kujua namna bora ya kufanya nao kazi bila kuwa sehemu ya mtandao wa majungu kazini.

Christian Bwaya ni Mhadhiri Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Kwa ushauri wasiliana naye kwa 0754870815