Mambo ya kuzingatia wakati wa kuandaa bajeti ya mshahara wako

Friday August 24 2018

 

By Gidion Obeid, Mwananchi [email protected]

Nyenzo muhimu ambayo itakusaidia kufikia malengo yako ya kifedha ni bajeti.

Mfanyakazi yeyote makini kila anapopokea mshahara huwa anajiuliza,

Je utanitosha kutimiza mahitaji na matakwa yangu kabla ya kupokea mshahara mwingine?

Bajeti ni mpango wa namna gani utautumia mshahara wako ili kuhakikisha siku zote unakuwa na hela ya kutosha kununua mahitaji yako ya msingi na mambo ya muhimu unayoyahitaji.

Mara nyingi ukisikia mtu anasema anaishi kwa bajeti, ujue ameishiwa.

Mshahara ukiisha ndiyo tunakumbuka umuhimu wa kuwa na bajeti.

Bajeti inakusaidia wewe kuweza kuitawala fedha yako, badala ya fedha yako kukutawala.

Bajeti inauamuru mshahara wako mahali unapopaswa kwenda badala ya wewe kuanza kushangaa mshahara wako umeenda wapi.

Ukianza kuwa na utamaduni wa kuandaa bajeti, itakusaidia kuwa na maisha yanayoendana na kipato chako.

Utajifunza namna bora ya kuyaongoza maisha yako kwenye mafanikio.

Yafuatayo ni mambo ya msingi yatakayokusaidia kuandaa bajeti;

Kuwa na malengo

Bajeti yeyote iliyoandaliwa vizuri inaonyesha taswira ya muelekeo wa kifedha wa maisha. Orodhesha vitu ambavyo unatamani kuvifanikisha kwa muda mfupi na kwa muda mrefu. Yapangilie malengo ya muda mfupi na ya muda mrefu kwa vipaumbele.

Malengo ya muda mfupi ni kama vile kulipa ada, kununua fenicha n.k.

Malengo haya ni yale ambayo umedhamiria kuyatimiza kipindi cha miezi kadhaa hadi mwaka mmoja.

Malengo ya muda mrefu ni yale ambayo kwa uwezo wako itakuchukua zaidi ya mwaka mmoja kuyakamilisha. Malengo haya yanaweza kuwa ujenzi wa nyumba, ununuzi wa gari n.k.

Lengo la muda mrefu kwa mtu mmoja linaweza likawa ni lengo la muda mfupi kwa mwingine.

Inategemeana na kiwango cha mshahara.

Swali la msingi la kujiuliza wakati unaanda malengo yako ni, Je kipato chako kinaendana na malengo uliyonayo?

Wakati kuwa na malengo makubwa inaweza kuwa chachu ya kutafuta hela kwa bidii ni vyema pia malengo hayo yasiwe makubwa sana kuliko uhalisia wa kipato chako.

Ni muhimu pia kuwaza kuhusu vyanzo vyako vyote vya mapato. Je, kuna vyanzo vipya unaweza kuvianzisha? Uwezo wako wa kupata hela zaidi utakusaidia kuweza kuwa na malengo makubwa zaidi.

Mchanganuo wa bajeti

Baada ya kuwa na malengo, unapaswa kuwa na makadirio ya kiasi cha fedha kinachohitajika ili kuweza kufanikisha kila lengo.

Baadhi ya malengo hasa yale ya muda mfupi ni rahisi kupata makadirio yake kwa uhakika, ila yale ya muda mrefu yanaweza kuhitaji kumshirikisha mtaalamu.

Weka kwanza bajeti kwa ajili ya matumizi ya lazima kama chakula,kodi, umeme na maji.

Ni aibu kwa mfanyakazi mwenye kipato kizuri kuishiwa hela ya chakula.

Kama kiwango cha mshahara hakiwezi kukidhi mahitaji ya lazima usilazimishe kuwa na malengo mengine zaidi ya kutimiza mahitaji yako ya kawaida.

Kwa wale wenye kipato cha kati cha mshahara, inashauriwa usitumie zaidi ya asilimia 50 kwenye matumizi ya lazima.

Baada ya kuwa umeishakadiria kiasi kinachokutosha kwa matumizi ya lazima, angalia ni kiasi gani kimebaki kwa ajili ya malengo mengine?

Kama una zaidi ya chanzo kimoja cha kipato, unaweza kuamua kipato kutoka chanzo fulani kitashughulikia swala la ada tu.

Anza kuyaweka yale malengo ya muda mfupi kwenye bajeti yako kutokana na umuhimu wa kila lengo. Kama fedha haitatosha, tafakari kama unaweza kupata bidhaa ya bei rahisi zaidi itakayoweza kukufikisha kwenye lengo hilo hilo.Baada ya hapo, yaweke malengo ya muda mrefu kwenye bajeti kwa kuzingatia vipaumbele.

Usijali, kama itakulazimu ufute baadhi ya malengo ili uwe na bajeti inayotekelezeka.

Kuna wakati wa kufurahi kwenye maisha. Unaweza kuitumia fedha yako kufurahia maisha pia. Ni vizuri kuwa na kiasi cha fedha ambacho utakitumia kwa ajili ya kununua kitu unachokipenda au kwenda kupumzika pamoja na familia yako mahali pazuri.

Uwe makini kiasi hiki kisiwe kikubwa sana kiasi cha kukutoa nje ya malengo makuu ya msingi.

Kama mshahara wako unaruhusu unaweza kutafakari pia kuhusu kuwa na fedha ya dharura na kiasi cha kuwasaidia watu wenye uhitaji nje ya familia yako.

Fuatilia bajeti yako

Ukiwa na bajeti usiyoifuatilia haina maana. Lazima uwe unaangalia kile unachokitumia kama kinaendana na mpango.

Bajeti siyo biblia au msaafu, unaweza kuibadilisha pale ambapo malengo au vipaumbele vinapobadilika.

Pia wakati wa kuandaa bajeti unaweza ukawa haukuwa na taarifa za uhakika kuhusu gharama za baadhi ya vitu, hivyo unaweza kuibadilisha ili iendane na uhalisia. Usibadilishe bajeti bila kuwa na sababu za msingi.

Weka mkakati wa kuhakikisha malengo yanatimia. Ni rahisi kushawishika kutumia fedha zaidi ya bajeti kwenye mambo yasiyo na maana. Tengeneza mfumo wa maisha utakaoweza kukusaidia usitoke nje ya malengo ya bajeti yako.

Utakapopokea mshahara jifunze kuzigawa zile fedha kabla ya kutumia. Kama siyo wewe unanunua chakula nyumbani, unaweza kumpa anayehusika fedha yote. Au unaweza kununua chakula cha mwezi mzima kwa wakati mmoja.

Kama kuna fedha umedhamiria kuiweka akiba, iweke mahali ambapo siyo rahisi wewe kufikia mara kwa mara. Kama una mke au mume mnayeaminiana mnaweza kuwa na akaunti ya pamoja na kuziweka fedha zenu za akiba huko.

Hakuna kuzitoa fedha bila wawili kuwa mmekubaliana.

Siku hizi ziko “application za simu na kompyuta” ambazo zinaweza kukusaidia kupanga bajeti na kuifuatilia. Unaweza kupakua baadhi ya “applications” hizo ukaziweka kwenye simu au komputa.

Kumbuka

Bajeti inatusaidia kujua kile ambacho hatuna uwezo wa kukinunua, ila haiwezi kuzuia tusikinunue.

Gidion Obeid ni Mhadhiri wa Uhasibu na Usimamizi wa Fedha, Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na mwanafunzi wa Shahada za Uzamivu (PhD). 0625698050

Advertisement