Mambo yanayovuruga wananchi katika vyama vya siasa

Viongozi wa vyama vya upinzani nchini wakionyesha tamko lao linalopinga muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa, wakati wa mkutano wao hivi karibuni. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Katika warsha ya siku mbili iliyowakutanisha viongozi wa vyama na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Mkurugenzi mtendaji wa Kampeni ya Utawala Bora, Wallace Mayunga anataja mambo matano ambayo watu wanatarajia kuyaona katika vyama vya siasa lakini wanayakosa, na hapo ndipo hufikia uamuzi wa kuhama chama.

Katika miaka ya karibuni kumekuwapo na malalamiko mengi kutoka vyama vya upinzani juu ya baadhi ya viongozi na wanachama wake kuhamia vyama vingine.

Katika warsha ya siku mbili iliyowakutanisha viongozi wa vyama na Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Mkurugenzi mtendaji wa Kampeni ya Utawala Bora, Wallace Mayunga anataja mambo matano ambayo watu wanatarajia kuyaona katika vyama vya siasa lakini wanayakosa, na hapo ndipo hufikia uamuzi wa kuhama chama.

Mambo hayo ni umadhubuti wa chama, utambulisho wa kisiasa, umoja ndani ya chama, uwezo wa chama kuingia katika uchaguzi na demokrasia ndani ya chama.

Umadhubuti wa chama

Anasema kama chama kinapoanzishwa kinapaswa kuwa na nguvu ya kusimamia kile inachokiamini vinginevyo kinaweza kupotea ndani ya muda mfupi kutokana na watu kupoteza imani nacho.

“Kama chama hakina umadhubuti mtakuwa mnapoteza muda kwa sababu hakuna mtu anayeweza kuwavumilia kwa muda mrefu na kufurahia kitu kisichokuwa na mwelekeo,” anasema Mayunga.

Utambulisho wa Kisiasa

Katika utambulisho wa kisiasa yapo mambo mengi yanapaswa kuzingatiwa ikiwemo kuwa na nembo, bendera pamoja na ofisi.

Anasema endapo mtu anaamua kuanzisha chama anatakiwa kuhakikisha alama anayoweka katika bendera inakuwa ni rahisi kueleweka kwa watu wote na si ya kufikirika.

“Unaweka ngumi katika bendera unafikiri mtu akiona anawaza nini. Ofisi ya chama iko katika fremu ya duka nani atakuamini na kukupa kura yake,” anasema Mayunga.

Umoja ndani ya chama

Mayunga anasema kuna baadhi ya vyama vya siasa vinavurugika kutokana na migongano iliyopo baina ya viongozi kutokana na wao kushindwa kuheshimu madaraka ya mtu mwingine.

Anasema kuna wakati kila kiongozi anakuwa na mtu wake anayemuamini kuliko mwingine, jambo ambalo pia linavuruga uaminifu na kusababisha kutoaminiana

“Katika chama tunajua kila kitu kinaratibiwa na Katibu mkuu lakini unakuta mwenyekiti anataka uwe ndio kila kitu, kazi zote zipite kwake badala kwa yule aliye na mamlaka na akufahamishe pale unapohitajika, nani wa kukuvumilia ukifika huko,” anahoji Mayunga

Chama kwenye uchaguzi

Mayunga anasema dhumuni la kuanzishwa kwa chama ni kusimamisha wagombea katika chaguzi tofauti ili kupata wawakilishi bungeni na kushika madaraka.

Anasema kama chama kitapoteza uwezo wa kusimamisha wagombea katika uchaguzi hakuna mtu anayeweza kuendelea kujiita mwanachama kwa sababu matarajio ya kumpata mtu wa kufikisha kero zake sehemu husika yatakuwa yametoweka.

Demokrasia ndani ya chama

Mayunga anasema misingi bora ya demokrasia ndani ya chama inamwezesha mtu kuongeza uaminifu na ushiriki wake katika shughuli za kuimarisha chama.

anasema fukuza fukuza ndani ya chama imekuwa ikiua demokrasia ndani ya vyama kwa kiasi kikubwa.

“Hata kama unasimama masaa mawili unazungumzia ustahimilivu wa kisiasa, halafu matendo yako ni sifuri tutakushangaa,” anabainisha.

Anasema vyama ni lazima vihakikishe vinasimamia matarajio ya watu wanao waongoza ili kuondoa malalamiko pamoja na hamahama.