Matatizo mabasi ya mwendokasi hayajaanza leo, yamekomaa sasa

Thursday October 18 2018

Rais John Magufuli akimuuliza maswali dereva

Rais John Magufuli akimuuliza maswali dereva Seif Simagofu (mwenye tai) wa mabasi ya mradi wa mabasi ya haraka muda mfupi baada ya kuuzindua. Picha ya Maktaba. 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Wakati Serikali inakopa zaidi ya Sh300 bilioni kutoka Benki ya Dunia ili kujenga mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart) ilikusudia kumaliza adha ya usafiri jijini Dar es Salaam.
Kuukamilisha mradi huo wenye kilomita 20.9 kutoka Kimara mpaka Kigamboni, Sh403 bilioni zimetumika zikiwamo Sh307 bilioni (Dola 290 milioni za Marekani) ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na kiasi kilichobaki kilitolewa na Serikali.
Lakini kwa siku za karibuni, tofauti na malengo yaliyokuwapo kipindi cha uasisi wake, abiria wanaoutegemea mradi huo wanapata kero zilizotarajiwa kumalizwa.
Suala la msongamano vituoni ambako abiria anapoteza muda mwingi ni baadhi ya sababu zilizomfanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuwaomba radhi wananchi kwa niaba ya Serikali kutokana na usumbufu wanaoupata.
Wiki iliyopita, Makonda alilazimika kutembelea kituo cha mabasi hayo kilichopo Kimara na kuwaomba radhi wananchi kutokana na kero wanayopata wakati lengo la mradi huo ilikuwa kuwapunguzia usumbufu wa kufika mjini lakini hali imekuwa tofauti.
Lakini, kupata suluhu ya kudumu na kuondoa kero zilizopo jambo la ziada linapaswa kufanywa kwenye mradi huo ambao miundombinu yake inasimamiwa na kampuni ya Serikali, Dart ambayo imeipa leseni kampuni ya Udart kutoa huduma ya usafiri.
Wakati Dart inamiliki miundombinu, Udart inamiliki mabasi. Migogoro ya muda mrefu ya kampuni hizi mbili ni suala linalohitaji utulivu kuishughulikia kwani ina historia yake.
Mabasi 70 yakwama bandarini
Wakati mradi huo unazinduliwa Mei 2016, ulikuwa na mabasi 140 ya Udart iliyosema itaongeza mengine. Katika mipango iliyowekwa, ilielezwa kuwa mradi utakuwa na mabasi 305 ambayo yataingizwa kwa awamu.
Lakini mpaka sasa mabasi 70 yaliyoingizwa Februari 16 na Udart yamekwama bandarini kutokana na mvutano uliopo kati ya Dart na Udart.
Ofisa uhusiano wa Dart, William Gatambi anasema utata uliopo unatokana na  Udart kuagiza mabasi hayo kinyume na makubaliano.
“Kulikuwa na malengo mawili ya Udart kupewa ruhusa ya kutumia miundombinu iliyopo. Kwanza ni kuangalia kama kuna kasoro zozote ili zirekebishwe, pili ni kuanza kuitumia miundombinu baada ya ujenzi wake kukamilika ili isiharibike,” anasema Gatambi.

Katika kufanya hivyo kwa kipindi cha mpito, anasema Udart walipewa kibali cha kuagiza mabasi 140 na hawajui 70 yaliyoingizwa yanatokana na kibali kipi.

“Hata Serikali haijui. Hatujajulishwa chochote mpaka sasa,” anasema.

Tofauti na msimamo wa Dart, msemaji wa Udart, Deus Bugaywa anasema mabasi hayo bado yapo bandarini ila “yanasubiri kibali cha Dart.”

Kuondolewa Maxi Malipo

Miezi sita iliyopita, Udart ilisitisha mkataba wa kukatisha tiketi na kampuni ya Maxi Malipo Africa na kubainisha kuwa kazi hiyo litapewa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Tangu kusitishwa kwa mkataba huo abiria wanapewa tiketi za mkono huku kukiwapo mkaguzi badala ya kutumia mashine zilizopo kuthibitisha malipo. Matumizi ya kadi za Udart yanapungua kila siku.

Bugaywa anasema, “Anayekusanya malipo ni Udart kwa kutumia mfumo wa Serikali (GePG). Mkataba wa TTCL haukuwa wa kukusanya nauli.”

Hata hivyo, Gatambi anasema baada ya Udart kuanza kutoa huduma walimtafuta mtu wa kuwasaidia kukusanya mapato na wakatoa mkataba huo kwa Maxi Malipo, lakini sasa hivi utaratibu unaandaliwa kumpata mzabuni mwingine atakayefanya kazi hiyo.

“Mchakato wa kumpata unaendelea vizuri,” anasema.

Mafuriko Jangwani

Mvua kubwa zilizonyesha Aprili, 2017 na kusababisha mafuriko maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, zilisababisha uharibu wa miundombinu na magari ya Udart.

Kutokana na mafuriko hayo katika eneo la Jangwani, usafiri ulisitishwa baada ya njia na kituo kikuu kujaa maji na kuharibu mabasi kadhaa. Umeme ulikatika kwenye vituo vya mradi huo hivyo kukwamisha mfumo wa ukataji tiketi.

Mafuriko hayo yaliisababishia Udart hasara ya Sh400 milioni zilizotumika kuyatengeneza mabasi yaliyoharibika.

Hata hivyo, hakuna kilichofanywa kuhakikisha hasara hiyo inaepukwa endapo mvua kubwa zitanyesha tena na jambo lililo wazi ni kuwa zikinyesha tena, huduma itasimamishwa.

Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc), Dk Vedasto Makota anasema mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kumechangia kuharibu kingo za Mto Msimbazi na hivyo kuongeza athari za mafuriko.

“Wakati mradi unajengwa ulifanyiwa tathmini ya mazingira na ukaonekana unatekelezeka. Dart walipewa cheti cha tathmini,” anasema Dk Makota.

Mkakati uliopo ni kutekeleza mradi unaopendekezwa na Benki ya Dunia kutokana na utafiti uliofanywa kuliboresha bonde la mto huo ili yawepo majengo ya biashara, kuongeza kina cha mto, kutunza uoto wa asili na kuongeza shughuli nyingine.

“Kukabiliana na changamoto za bonde hili kunahitaji uwekezaji mkubwa utakaowahusisha wadau wa maendeleo, Serikali na wananchi.”

Udart kuorodheshwa DSE

Kwa kushirikiana na wamiliki wa daladala, Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) waliunda kampuni ya Udart inayotoa huduma ya usafiri kwa wananchi.

Miezi michache baada ya kuzinduliwa, uongozi wa Udart ulisema unatarajia kujiorodhesha katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) ili kuwapa fursa wananchi kuumiliki mradi huo, lakini mpaka sasa suala hilo halijatekelezwa.

Menejimenti ya Udart ilisema mpango huo ungetekelezwa kati ya Oktoba na Novemba, 2016.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, meneja mawasiliano wa Mamlaka ya Masoko na Mtaji (CMSA), Charles Shirima alisema yuko nje ya ofisi, hivyo hana taarifa za uhakika.

“Nipo kwenye semina kwa wiki nzima. Sina uhakika mchakato huo umefikia hatua gani ingawa najua ulianza,” alisema Shirima.

Hisa za UDA

Mwaka 2000, Serikali kupitia bodi ya wakurugenzi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) iliuza hisa zake zote ilizokuwa nazo kwenye shirika hilo kinyume na utaratibu.

Kwenye ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014 ilibainishwa kutolewa kwa ushauri wa kitaalamu kuhusu kukiukwa kwa utaratibu huo lakini bodi hiyo haikuuzingatia.

CAG alisema uuzaji wa hisa hizo ulipaswa kufanywa na Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) na sio bodi ya Uda, lakini ushauri wake haukuzingatiwa.

Kutokana na ukiukwaji wa utaratibu ulioimilikisha kampuni ya Simoni Group hisa zote za Uda, malipo ya muamala huo yaliyofanywa mwanzoni mwa 2017, kiasi cha Sh5.8 bilioni hazikuridhiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Jiji lilikataa lakini Rais John Magufuli akalipa wiki mbili baraza la jiji hilo kuzipangia matumizi. Hata hivyo hapakuwa na mabadiliko.

Katibu mkuu wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ramadhan Iyombe anasema fedha hizo hazikuchukuliwa na Serikali, bado zipo halmashauri ya jiji.

“Muulize Spora (Liana, mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam) atakuambia wamezifanyia nini fedha hizo. Hawakunyang’anywa, bado wanazo,” alisema Iyombe.

Alipotafutwa Spora alisema yuko nje ya ofisi, hivyo atafutwe atakaporudi kueleza kuhusu suala hilo. Taarifa za uhakika kutoka ofisi za jiji hilo zinasema mazungumzo yaliyofanywa kati ya baraza na menejimenti yameanza kutoa mwanga wa kutumika kwa fedha hizo.

“Mwanzo baraza la jiji lilikataa kuzitumia fedha hizo lakini sasa hivi limekubali zitumike. Mapendekezo yaliyotolewa ni zinunue mabasi ya wanafunzi pamoj ana ya mwendokasi. Sasa hivi wanatafuta mzabuni kufanikisha mchakato huo,” kilisema chanzo hicho.

Watoa huduma

Mapema Mei, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliliambia Bunge kuwa kuna mpango wa kukishirikisha Chama cha Wamiliki wa Daladala (Uwadar) kuwa miongoni mwa watoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart) ili kupunguza kero za usafiri zilizopo.

Majaliwa alisema kuna haja ya kuongeza watoa huduma ili kuondoa changamoto zilizopo na baadhi ya wawekezaji wa ndani na nje wakiwamo Uwadar wanao uwezo wa kufanya hivyo kwa ufanisi.

Majaliwa alisema Serikali inajua makao makuu ya mabasi (Jangwani) kuna mgogoro wa undeshaji kutokana na muungano wa taasisi zilizopo.

Kukabiliana nazo, alisema: “Tunaingia awamu ya pili, tutakuwa na mdau mwingine ili kuwa na ushindani zaidi ili mwendeshaji mmoja akipata tatizo mwingine anaendelea.”

Kampuni ya Udart ilifungua kesi mahakamani dhidi ya Serikali kupinga kuongezwa kwa mtoa huduma mwingine. Waziri mkuu alisema iwapo itabainika mwendeshaji wa sasa atakuwa na matatizo basi ataondolewa.

Gatambi amesema mchakato wa kumpata mzabuni mpya unaendelea na sasa hivi menejimenti inazipitia nyaraka kabla ya kukaribisha kampuni zinazotaka kushindana.

“Kwa sasa nyaraka za RFQ (mchanganuo wa maombi ya zabuni) zinachambuliwa na tangazo litakapotolewa, kanuni zitaka likae kwa siku 75 za kazi. Tunatarajia kumpata mtoa huduma mwingine Machi mwakani,” anasema.

Anasema mchakato huo unaendelea na utakuwa wa kimataifa ukihusisha kampuni za ndani na nje ya nchi. Suala linawezekana sasa kwa sababu, anasema Udart walishindwa kwenye kesi waliyoifungua kuzuia mzabuni mwingine kutoa huduma.

“Hakuna mkataba unaosema Udart atakuwa ndiye mtoa huduma pekee.”

Strabag International GmbH

Changamoto za mradi wa mabasi yaendayo haraka hayajaanza baada ya kuzinduliwa utoe huduma kwa wananchi kwani baadhi yapo siku nyingi.

Oktoba mwaka 2014, kampuni iliyokuwa inaujenga mradi huo, Strabag International GmbH ilitajwa kutowasilisha taarifa zake za hesabu za mwaka kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).

Licha ya kampuni hiyo kutoka Ujerumani kukiuka kanuni hizo, ilitekeleza mradi, ikaukamilisha na kuukabidhi na kuondoka.

Alipoulizwa kaimu mkurugenzi mtendaji wa Brela, Emmanuel Kakwezi kama kuna hatua zozote zilichukuliwa dhidi ya Strabag, alisema hana uhakika.

“Njoo ofisini nitakukutanisha na ofisa atakayekusaidia kupata kumbukumbu sahihi za kilichofanywa,” alisema Kakwezi.

Advertisement