KUTOKA LONDON: Matumizi ya dawa za kisasa kwa wingi si suluhisho la kiafya

Sunday April 14 2019Freddy Macha

Freddy Macha 

By Freddy Macha

Miaka mingi sasa madaktari wa Kizungu wamekuwa wagumu kutoatoa dawa ovyo kwa magonjwa madogo. Mfano mzuri ni mafua. Zamani ukiugua mafua unaandikiwa dawa kali za kuua vimelea ( Antiobiotics) ....baadaye ikagundulika virusi hugeuka sugu na mafua hurudi tena.

Pia wataalamu wakang’amua mafua husababishwa na kinga maradhi kuwa dhaifu. Mathalan usipopata usingizi wa kutosha kwa muda mrefu ni rahisi kushambuliwa na mafua.

Hapa somo nini?

Lazima tulale usingizi unaotakiwa wa saa 7-8 kila siku.

Na mafua ni moja tu ya maradhi yanayosababishwa na uchovu au ukosefu wa usingizi. Jingine ni fadhaa au mtafaruku wa maisha (“stress”)–yapo maradhi lukuki yanayotokana na kuhangaishwa mwili. Chunguza unapokumbwa na matatizo ya kikazi, kifamilia, kisaikolojia ni rahisi kuugua. Hivyo dawa ni mapumziko. Si kula dawa kali.

Wapo wanaoumwa umwa na vichwa.

Kama hakuna jeraha lililosababishwa na kitu cha nje (kipigo au ajali) maumivu ya kichwa si maradhi ya kula dawa. Wapo watu wanaobwia dawa kila wanapobughudhuliwa na kichwa. Ukikaa sana juani (au joto na baridi sana ) utaumwa na kichwa. Ukikosa usingizi, ukikumbwa na fikra na mtafaruku fulani wa kimawazo, bila shaka utaumwa na kichwa. Wanawake pia huumwa na kichwa siku zao.

Hili linaponywa si tu kwa kulala bali pia kwa vitu tunavyokula. Ukiwa na kiu usipokunywa maji utaumwa na kichwa. Kuumwa kichwa ni mawasiliano (au ujumbe) kutoka mishipa yako ya fahamu ikikuonya unatakiwa ufanye jambo fulani. Kama una usingizi wa muda mrefu lazima utaumwa na kichwa.

Ulaji chakula kama tulivyoona safu hii (mara kwa mara ) ni muhimu sana kiafya.

Ukiwa na kiu kunywa maji, madafu au juisi ya matunda. Ukinywa kahawa, pombe, au vinywaji vyenye gesi hatimaye utaumwa na kichwa shauri ile gesi haitakiwi mwili na inaudhalilisha mwili.

Vyakula huchangia sana afya ya miili na kutougua au kuugua hutegemea tuna kula nini.

Matokeo yake wanadamu tunakula ovyo, hatujali mazoezi, tukiugua kidogo tunakimbilia kwa waganga kutaka dawa kali.

Miaka minne iliyopita mganga mashuhuri wa Kidenish, Dk Peter Gotzsche, alishindwa kujizuia kushauri juu ya ubaya wa dawa za kisasa katika mahojiano yanayopatikana You Tube.

Dk Gotzsche ambaye pia ni mtafiti, na mkuu wa Kituo cha Cochrane Hospitali ya Rigshospitalet, Copenhagen, alidai maradhi mawili yanayoua wanadamu zaidi ni saratani na moyo. La tatu akaonya ni ulaji wa dawa za kisasa.

Akasema watu wanapokula dawa (na waganga wanapotoa dawa hizo) hawaangalii madhara yake (“side effects”).

Mganga huyu ambaye ni Profesa, alitoa mfano wa maradhi ya akili.

Unapopewa baadhi ya dawa unaambiwa ukila zitaweka uwiano katika ubongo wako. Ni sawa akaeleza kuwepo tiba ya muda mfupi lakini baadaye huwepo madhara katika huo huo ubongo.

Siri kuu ya dawa zinazotolewa, ni biashara. Waganga na mahospitali yanavyotumika leo yako ubia au hushirikiana na makampuni makubwa yanayouza dawa.

Hata baada ya kupingwa na baadhi ya Serikali na waganga wenzake, Profesa Gotzsche alisisitiza kuwa ni lazima tuwe waangalifu tunapotumia dawa. Tusizitegemee sana.

Advertisement