Mazinyungu ilivyoona fursa katikati ya changamoto ya elimu bure

Penye changamoto ndipo penye fursa. Ni wachache wanaoweza kukubaliana na msemo huu, kwa kuwa wengi wamezoea kulalamika wanapokumbwa na changamoto.

Mpango wa elimu bila malipo ulioanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano, umejaa changamoto. Kwa mfano, wazazi hawataki tena kuchangia elimu kwa kuwa wanaamini kila kitu kinapaswa kufanywa na Serikali.

Hali hii imerudisha maendeleo katika shule nyingi. Shule zilizokuwa zikitoa chakula kupitia michango ya wazazi, sasa hazifanyi hivyo na wanaoumia ni watoto.

Hata ndivyo, ndani ya changamoto na nyinginezo, Shule ya Sekondari ya Mazinyungu iliyopo Kilosa Mkoani Morogoro, imeng’amua fursa. Badala ya uongozi wa shule kubaki kulalaama kama ilivyo kwa shule nyingine, umejiongeza na kuwa shule ya mfano.

Mkuu wa shule hiyo ya kata, Ngamba Manegese, anasema pamoja na ruzuku inayotolewa kutotosheleza mahitaji yote ya shule yake, jambo hilo halijawahi kuwaathiri.

“Ubunifu ndio unaosaidia kuendesha shule, huu unatufanya tusonge mbele bila wasiwasi wowote, kama hivi umeme umekatika lakini utawaka kwa sababu fedha ya kununua ipo,” anasema Manegese na kuongeza;

“Serikali inajitahidi kwa upande wake nasi tunawajibika katika upande wetu. Hapa sijapata shida kuendesha shule kwa kweli.”

Manegese anasema ndani ya changamoto za elimu bila malipo, wao wanaona fursa lukuki zinazoweza kubadilisha historia ya shule hiyo.

Katika kipindi hicho wameweza kujenga zaidi ya matundu 16 ya vyoo kikiwamo chumba cha kubadilishia watoto wa kike, chakula cha shule na huduma nyingine shuleni ikiwamo ulinzi, maji na umeme.

Anasema wameweza pia kukarabati baadhi ya miundombinu muhimu kama milango ya shule na wamefanikiwa kuajiri walinzi wawili na mhudumu ambao wanamudu kuwalipa mishahara yao kila mwezi.

Wamewezaje?

Manegese anaeleza kuwa mara baada ya kutangazwa elimu bila malipo, walikaa na viongozi wengine wakiwamo walimu na kubungua bongo jinsi ya kuendesha shule.

“Basi tukaamua kubuni mradi wa duka na tukajua duka hili litaziba pengo kubwa la michango ya wazazi,” anasema.

Anasema kwenye duka hilo zinauzwa bidhaa zinazotumiwa zaidi na wanafunzi kama vifaa vya shule, maji, soda na sharubati.

“Wanafunzi wananunua bidhaa zilizo kwenye duka lao na faida ndiyo kama ulivyoona mwenyewe, tumelipia umeme. Pia tunamudu kulipa ulinzi na matumizi mengine madogo madogo,” anasisitiza.

Mbali na duka la shule, biashara ndogondogo kama vitafunwa vinaruhusiwa na wale wanaoleta wamekuwa wakilipia ushuru kidogo kwa ajili ya kuendesha shule.

Chakula shuleni

Manegese anasema mara tu elimu bila malipo ilipotangazwa baadhi ya wazazi walitaka kwenda

kubeba chakula chote walichochanga wakiamini elimu ni bure.

“Niliwarudisha na vikapu vyao, nikawauliza aliyewaambia chakula kitagawanywa kwa sababu elimu ni bure nani? Lazima watoto wale kila siku,’ anasema.

Anasema ilibidi wazazi waanze kueleweshwa kuhusu jambo hilo.

“Hivi tunavyoongea stoo kuna magunia 30 za mahindi, tunachotafuta ni maharage na fedha ya mpishi ambayo haitakosekana,” anasema.

Marafiki ulaya

Anasema kwa sababu inawezekana wanafunzi kuwa na marafiki wa shule yoyote ile kwenye nchi zilizoendelea alifanikiwa kuwaunganisha na wenzao nchini Sweden kupitia mpango wa ‘Students Learning Exchange’.

Anasema aliandika andiko akaliwasilisha akiielezea shule yake na wakapata marafiki.

“Hivyo wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi kila mtoto ana rafiki Sweden. Hii imeongeza mashindano katika kujisomea kwa sababu wanapenda kuwa na marafiki kwa maana ya kujifunza zaidi,” anasisitiza.

Vyoo vya shule

Licha ya michango kutoruhusiwa, anasema kwa sababu ya hali mbaya waliyokuwa nayo, walilazimika kukaa kitako na wazazi na kukubaliana.

‘’Ilibidi tuwaeleze wazazi ukweli na wao wenyewe wafikirie nini wanaweza kufanya kusaidiana na Serikali katika kufikia malengo,” anaeleza.

Anasema kati ya wazazi zaidi ya 750 wa shule hiyo, wazazi 250 walikubali kuchangishana na kuamua kujenga vyoo kwa ajili ya watoto wao.

“Hivi ninavyokuambia shule hii ina vyoo bora kabisa vyenye maji, watoto hawapati tabu,” anasema na kuongeza:

“Elimu bila malipo haimaanishi wazazi hawapaswi kushiriki elimu ya watoto wao, Serikali imewapunguzia mzigo lakini wanalo jukumu kubwa tu.’’

Ofisa elimu Sekondari wa wilaya ya Kilosa, Paula Nkane anasema wanaandaa utaratibu wa kuwapa motisha walimu wabunifu wanaofanya vizuri katika kuendesha shule na kuongeza ufaulu.

“Wanaoweza kufanya ubunifu ni walimu wenyewe kwenye shule yao kwa hiyo ili kuongeza ufaulu wa wilaya walimu wabunifu tutawatambua,” anasema.

Mkakati wa ufaulu

Shule hii haina historia nzuri ya ufaulu na ndio maana Manegese anahaha kuhakikisha inaingia katika orodha ya shule zinazofanya vizuri kimkoa na kitaifa kwa jumla.

Katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017, wanafunzi 12 walipata daraja la pili, 38 daraja la tatu, 51 la nne na 30 walipata sifuri.

“Natamani kusiwe na sifuri kabisa, nimeanza kuwazoesha kufanya mitihani kama chuo kikuu, yaani wanafanya mitihani kwa kuchanganyika ili kila mmoja afaulu kwa uwezo wake,” anasema.

Anasema kila wiki wanafunzi wanafanya mazoezi huku kila mwezi kukiwa na mitihani ambayo, matokeo yake yanajumulishwa kwenye mitihani ya mwisho wa muhula.

Anataja mikakati mingine ya kukuza ufaulu kuwa ni pamoja na walimu kujitolea kufundisha hata kwa muda wa ziada hasa kwa madarasa yenye mitihani.

“Nimeboresha nidhamu; mfano watoto walikuwa wanavaa sketi fupi nyuma na mbele ndefu wakazitungia jina kabisa. Nilipiga marufuku na sasa hivi sare ni sketi ndefu hadi miguuni,” anaeleza.

Anasema wanafunzi wake kike wameandaliwa utaratibu maalum wa kuwapima mimba mara kwa mara, ili kuwapa hofu wasijiingize kwenye vishawishi.