Mbatia: Elimu yetu isiwe maabara ya majaribio

Tuesday January 22 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Mjadala wa ubora wa elimu nchini umekuwepo kwa muda mrefu na bado unaendelea. Wakosoaji wanadai kutokuwepo kwa sera bora ya elimu, vifaa vya kufundishia na muundo wa mitaala ya elimu kwa ngazi mbalimbali pamoja na masilahi ya duni ya walimu kuwa ni miongoni mwa mambo yanayorudisha nyuma sekta hiyo.

Miongoni mwa wakosoaji wa mfumo wa elimu nchini ni Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia ambaye mwaka 2013 alitoa hoja binafsi bungeni akitaka mfumo wa elimu upitiwe upya.

Katika mahojiano yake na Mwananchi hivi karibuni, Mbatia ameendelea kusisitiza haja ya mfumo wa elimu kufumuliwa na kuundwa upya. Mahojiano kati ya mwanasiasa huyo na mwandishi wetu yalikuwa kama ifuatavyo:

Swali: Kwa muda mrefu umekuwa ukipigia kelele ubora wa elimu nchini je, kwa sasa unaona hali imefikia wapi?

Jibu: Elimu ninayoipigia kelele ni ile ya kujitambua tu, kutambua haki za msingi. Mfumo rasmi wa Tanzania ni wa kibaguzi, ni mfumo ambao tunajichimbia kaburi sisi wenyewe.

Januari 2013 niliwasilisha hoja binafsi kuhusu udhaifu katika sekta elimu nchini. Nilikuwa nakosoa sera ya elimu ya mwaka 1995. Niliuliza sera yenyewe imeshirikisha watu kiasi gani je ilisema miaka 20 ijayo tunafanyaje au 30 au 40?

Baada ya kutoa hoja ile, ikavunjwa Emac (Kamati ya kusimamia vifaa vya elimu) Juni 2013, baada ya hapo ikaandikwa sera nyingine ya elimu ya 2014 iliyozinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Lakini baada ya kuandikwa sera ile, leo hii sera hile haifai licha ya kugharimu mabilioni ya fedha, wanataka kuandika sera mpya. Nani anaiandika?

Kwa nini nasema hivyo? Ukienda kwa daktari ndiye atakuandikia dawa unayotakiwa kuitumia kwa tatizo aliloliona kwako. Halikadhalika kwenye elimu walimu na wadau wa elimu wangeachwa wakaja na sera iliyo shirikishi na waseme tuwe na mikataba kwenye elimu iwe vipi kwa miaka 20 au 30 ijayo.

Swali: Kutokana na hoja yako bungeni ulitaka sera ya elimu iweje?

Jibu: Ukiangalia nchi kama Finland wadau wa elimu ndiyo wanaoshauri mitalaa iwe vipi kwa sababu wanajua sera na pia kama nchi wanajua nini waliamua miaka 20 hadi 40 nchi iweje. Hawana ubaguzi.

Sisi siyo kisiwa, tufanye utafiti duniani kujua wengine wanafanyaje. Angalia Finland mfumo wake wa elimu na jinsi watu wake walivyo na furaha na kujitambua wanashika nafasi ya kwanza duniani.

Njoo Tanzania kwenye watu kuwa na furaha tumeshika nafasi ya 153 kati ya nchi 156 dunaini na hii inaanzia huko kwenye elimu. Yaani tumewashinda tu Burundi, Yemen na Syria.

Somalia pamoja na kupigana kote vita na Sudan huko wako juu yetu, kwa hiyo hatujitambui, na hii ni sababu ya elimu.

Swali: Umesema elimu iliyopo Tanzania inafanya majaribio, ni majaribio gani hayo?

Jibu: Mfumo wa elimu ulio rasmi yaani shule za msingi, sekondari mpaka vyuo vikuu, bado uko hoi bin taabani, kwa sababu tumeamua kuubinafsisha na kuuweka kwa mtu mmoja. Waziri anayekuwepo ndiye mwenye mamlaka ya kuamua lipi lifanyike na lipi lisifanyike. Akija waziri huyu anakwambia hili, akija huyo anakwambia hili.

Nakumbuka Januari 31, 2013 nilitoa hoja binafsi bungeni kuhusu udhaifu katika sekta ya elimu, sera, mitalaa na vitabu. Tumewafanya watoto wetu wa shule za msingi, sekondari na hata vyuo vikuu kama ni sampuli ya maabara ya kufanyia majaribio.

Kwa mfano, ukiangalia sera ya mwaka ya 1995 ilikuwa hoi. Wamekuja kuandika sera nyingine ya 2014 na imekuja kuzinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete Februari 13, 2015 kabla ya kuondoka madarakani.

Sera ile imeishi miaka miwili tu sasa ni mbovu inatakiwa iandikwe upya.

Rai yangu ni kwamba tuzungumzie katika misingi ya ubora na shirikishi kwa wote. Neno shirikishi ni muhimu kwamba wadau wa elimu washirikiane.

Swali: Una maoni gani kuhusu kauli ya Naibu Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mwita Wairata ya kuzitaka shule binafsi kutowafukuza wanafunzi ambao wazazi wao wameshindwa kukamilisha ada zao

Jibu: Tunafanya kosa kuweka ubaguzi katika elimu kwa kuweka madaraja. Lakini ubaguzi mkubwa ni kufanya Serikali ishindane na shule binafsi, badala kuwafanya kuwa washirika wa pamoja wa kuhakikisha kuwa elimu yetu ni bora zaidi.

Tunaona changamoto, badala ya Serikali kuwapatia moyo, badala ya kuwapatia ruzuku shule binafsi, kwa sababu ni jukumu la Serikali kuelimisha Taifa lake. Serikali inatoa matamko ya namna hiyo.

Halafu je, kila waziri akitamka neno inakuwa ni kanuni au sheria? Hakuna utaratibu wa namna hiyo, ndiyo maana nasema elimu yetu tusiifanye elimu yetu kama ni sampuli ya maabara au tuanze kutishiana.

Tutaifanya Tanzania elimu yetu iwe ni ya ovyo tu na hapa tulipofika. Naomba Waitara na wengine turejee katika lengo la nne la Malengo Endelevu ya Dunia, linalosema elimu bora, shirikishi kwa wote.

Advertisement