Mbedule; Mtanzania mwenye ndoto za mbali huko Norway

Monday January 7 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Muda mwingine unatakiwa ukubaliane tu na uhalisia wa mambo ulivyo, ukiwa mbishi kwa kupingana na hali ilivyo unaweza ukajikuta mwisho wa siku inakula kwako.

Amani Dickson Mbedule ni mmoja wa watu ambao wanaimani kwamba maisha ni popote huku akiwa na mawazo ya kuwa penye nia siku zote pana njia hivyo anachoendelea kukiwekeza kwenye majukumu yake ni juhudi na ubunifu.

Amani ni winga wa Kitanzania anayecheza soka la kulipwa Norway kwa mkopo kwenye klabu ya daraja la pili, Notodden akitokea Sarpsborg 08 ya Ligi Kuu nchini humo.

Mtanzania huyo anayeishi na baba yake mazazi Norway, anasema hakuna kipindi kigumu kwa wachezaji kama kile cha kupigania nafasi ya kuingia kikosi cha kwanza, ukiwa unatokea kwenye timu ya vijana.

Winga huyo aliyezaliwa Septemba 19, 1996, anasema ugumu unatokana na vile ambavyo timu nyingi zimekuwa na tabia za kununua wachezaji wengine kutoka sehemu nyingine na hilo limekuwa likijitokeza mara nyingi kwenye timu kubwa za madaraja ya juu.

“Mpira ni mchezo mgumu sana. Msione mtu anakuwa staa huwa kuna mambo mengi magumu ambayo amepitia hadi kufika kwenye kilele cha mafanikio. Kuna stori za maumivu nyuma ya wakina Messi na hata Ronaldo ambao wanatamba kwa sasa.

“Hakuna njia ya mkato, Nipo kwa mkopo Notodden FK, nikitokea Sarpsborg 08. Iko hivi, sikuwa napata muda wa kucheza kabisa nikiwa na timu yangu, nilijiona nimekomaa na pia mwenye uhitaji wa kupata uzoefu.

“Mawazo yangu yaliendana na matakwa ya timu yangu ambayo na yenyewe ilikuwa na mpango wa kutaka kunitoa kwa mkopo baada ya kupokea ofa kutoka kwenye timu ambayo naichezea kwa sasa.

“Sikuwa napingamizi na nilijiandaa kukabiliana na changamoto mpya sehemu nyingine, nilitambua kuwa natakiwa kwenda kuonyesha ili niwe mchezaji wa kikosi cha kwanza,” anasema.

Uhamisho wa Amani kwenda kwa mkopo Notodden FK, ulifanyika Agosti 2 mwaka jana na mkataba wake huo wa mkopo unatarajwa kumalizika Desemba 31 mwaka huu.

Nyota huyo wa Kitanzania anasema mara baada ya kutua kwa mkopo Notodden FK akakutana na nyota wanne ambao wanauwezo wa kucheza kwenye nafasi ambayo amekuwa akipendelea kucheza ya winga wa kulia na kushoto.

“Kutoka kwenye kutopata nafasi kidogo nikaanza kucheza japo sio muda mrefu lakini nilijikuta nikiwe muda mchache ambao umenijenga na taratibu naanza kuingia kwenye kikosi cha kwanza.

“Nimejifunza vitu vingi kutoka kwa kaka zangu Martin Brekke, Erik Midtgarden na André Bakke ambao wamekuwa wakicheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza, najivunia kuwa nao na wamesaidia kwa kiasi chake uwezo wangu kuongezeka,” anasema.

Msimu huu, Amani amecheza mechi 10 Ligi Daraja la Kwanza Norway, ametumia jumla ya dakika 339 na katika michezo hiyo hajafanikiwa kufunga wala kutengeneza bao hata moja.

Akizungumzia mipango yake, anasema ni kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha timu yake ya Sarpsborg 08 inayoshiriki Ligi Kuu Norway ambayo inafahamika zaidi kama Eliteserien.

Amani anadai kuwa ndoto yake ni kucheza Eliteserien na michuano mbalimbali ya Ulaya. Timu ya Mtanzania huyo huwa inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na muda mwingine Europa Ligi.

Msimu huu wa 2018/19 Sarpsborg 08 ipo kwenye michuano ya Europa Ligi tena kundi moja na KRC Genk ya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kama Amani angekuwa kikosi cha kwanza inaama michezo baina ya timu hizo mbili ingewakutanisha Watanzania hao.

Advertisement