Mbinu za kumsaidia mwanao kuchagua ajira aipendayo

Friday February 8 2019

 

By Christian Bwaya, Mwananchi [email protected]

Watu wengi hufanya uamuzi wa ajira kwa kuchelewa. Kwa chuo, kijaana anamaliza chuo lakini bahati mbaya anakuwa hana uhakika afanye kazi ya aina gani.

Katika mazingira kama haya, kijana anajikuta kwenye wakati mgumu kwa sababu uamuzi wake unaweza kuwa na gharama kubwa.

Kwa upande mwingine, ushauri wanaoupata vijana wetu, mara nyingi, huwapotosha.

Kwa mfano, huwaelekeza vijana kuchagua kazi zenye heshima katika jamii hata kama kimsingi haziendani na matakwa ya vijana wenyewe.

Ingawa ni kweli wazazi wengi hutoa ushauri kwa vijana wao kwa nia njema ya kuwasaidia kufanikiwa, si mara zote wazazi huwa na taarifa sahihi zitakazowawezesha kuwasaidia vijana.

Katika makala haya, nitaelezea masuala manne yanayoweza kumsaidia mzazi kuelewa namna bora ya kuwezesha ajira ya mwanaye.

Usimwamulie cha kufanya

Ulimwengu wa sasa ni tofauti kabisa na ule uliokuwa nao wewe ukiwa kijana. Mazingira ya ajira za sasa yamebadilika na ajira nyingi zilizopo hivi sasa hazikuwapo nyakazi zilizopita.

Kwa mfano, ajira za kudumu zilikuwa muhimu zamani. Hivi leo, ajira nyingi si za kudumu na usalama wa ajira unategemea zaidi ujuzi, uwezo wa kutatua matatizo, ubunifu, bidii na nidhamu ya kazi.

Kufikiri uamuzi wa kijana wa leo utakuwa sawa na yale uliyoyafanya wewe miaka 30 iliyopita ni kukosea. Usipokuwa makini, inawezekana kabisa ukajikuta ukimtumia mwanao kufikia ndoto ambazo wewe hukuzifikia jambo ambalo si sahihi.

Kumbuka kijana wako ni binadamu mwenye ndoto na haki ya kuishi maisha yake bila kuingiliwa. Hata pale unapoamini kijana wako anapaswa kuchukua uelekeo fulani, bado unahitaji kuwa na tahadhari usionekane ‘unamwendesha.’

Msaidie kufahamu wito wake

Wakati mwingine wasiwasi ulionao wewe kama mzazi unakuwa na ukweli fulani. Vijana wengi, hata wale wanaofanya vizuri darasani, hawana uelewa wa kile wanachokitaka maishani.

Wajibu wako kama mzazi ni kumsaidia kijana wako kuuelewa wito wake. Kama mwanao, mathalani, anaonekana kutamani kufanya kitu kisichoendana na uwezo wake, hiyo haimaanishi hawezi kufanya kitu hicho moja kwa moja.

Wakati mwingine ile shauku tu ya kutaka kufanya kitu fulani kisicho cha kawaida, huchochea uwezo usio wa kawaida ndani ya mwanao na hatimaye kumpa mafanikio makubwa.

Msaidie kijana kupanua uelewa wake aone ndani yake kumejificha uwezo gani unaoweza kukuzwa.

Kupitia mambo anayopenda kuyafanya mara kwa mara, changamoto anazoziona kwenye jamii, anaweza kuanza kuelewa wito alionao katika maisha.

Pia, unaweza kufikiri kumpeleka mwao kuonana na wanasihi (career counsellors) watakaomsaidia kujua kitu gani kiko ndani yake.

Badala ya kumshinikiza kuwa kama vile unavyotaka awe, mnasihi atamsaidia mwanao kujua ana uwezo gani, anataka kufanya nini na kumpa mwongozo wa namna ya kufikia kule anakotaka kwenda.

Msaidie kukuza mtandao wake

Siku hizi, mtandao wa watu ni kete muhimu ya mafanikio wakati mwingine kuliko ufaulu na wasifu mzuri anaokuwa nao kijana.

Mtu mwenye ufaulu wa kawaida lakini mwenye mtandao madhubuti anakuwa kwenye nafasi ya kupata taarifa muhimu zitakazomwezesha kupata ajira kuliko mtu asiye na mtandao wa maana.

Ili kukuza mtandao wake, msadie kijana wako kujitolea kila inapowezekana, mwezeshe kuhudhuria makongamano mbalimbali aweze kukutana na watu wanaoweza kuwa amana muhimu kwake kwa siku za mbeleni.

Pia, kutegemeana na nafasi uliyonayo, mkutanishe na watu unaofikiri anawahitaji, mathalani, wale wanaoweza kuwa wadhamini wake.

Marafiki na watu unaofahamiana nao wanaweza kuwa mahali pazuri zaidi pa kuanzia.

Sambamba na jitihada za kupanua mtandao wake, msaidie kijana wako kujifunza namna ya kuandika wasifu (curriculum vitae) wenye kuwashawishi watu kuwa anao ujuzi na uzoefu unaotakikana.

Kama alishawahi kufanya kazi kwa vitendo mahali, hiyo ndiyo fursa ya kuhuisha wasifu wake.

Mkutanishe na waliofanikiwa

Vijana wanahitaji kujifunza kwa watu waliowatangulia. Msaidie kijana kupata mtu anayeweza kuwa mfano kwake (role model).

Kama mwanao anaonyesha dalili za kuchukua uelekeo fulani katika maisha, msaidie kupata watu waliofanikiwa kwenye eneo hilo ili ajifunze kwao.

Kijana wako anapokuwa mtu mzuri anayeweza kujifunza, hamasa yake ya kupambana inaongezeka.

Kule kuona mtu anayefanya kitu anachotamani kukifanya baadaye kunamwongezea motisha ya kujitahidi.

Kwa mfano, kama mwanao anapenda kuwa injinia au mwanasiasa, mkutanishe na injinia au mwanasiasa aliyefanikiwa. Kumkutanisha na watu walio mbele yake kunaweza kumchochea kujitahidi zaidi.

Sambamba na hilo, mpe nafasi ya kujaribu vitu vipya.

Mpeleke kwenye maeneo mbalimbali akutane na sayansi asilia, sayansi jamii, sanaa na kila aina ya fursa za kazi.

Kupitia fursa hizo atakazoziona, kijana wako anaweza kuanza kuonyesha mapenzi na fani fulani. Mtie moyo akue kwenye fani anayoipenda.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU); mawasiliano 0754870815, twitter: @bwaya

Advertisement