Mbinu za kutatua changamoto za ufugaji kuku

Katika biashara yoyote ile changamoto ni lazima ziwepo. Hata katika kilimo biashara changamoto zipo nyingi. Vivyo hivyo hata katika ufugaji wa kuku changamoto zipo. Leo nitaangazia changamoto kadhaa muhimu ambazo ni vizuri kuzifahamu kabla hujaingia kwenye ufugaji wa kuku na utatuzi wake.

Mtaji

Mtaji wa kuanzisha shughuli hii ni miongoni mwa changamoto kubwa inayowatesa wafugaji wengi. Mfano gharama za mafunzo na miongozo ya ufugaji, vitabu ada za semina, gharama za utafiti wa masoko, kununua na kukodi eneo, vifaranga, chanjo na madawa pamoja na chakula cha kuku.

Swali kubwa hapa ni je, tunapataje mitaji? Unaweza kupata mtaji kwa kupitia mali binafsi kama vile mashamba, fedha, nyumba, gari, mazao.Pia, kwa kutumia wabia wa biashara (mtaji wa mali na mtaji wa mawazo na fikra tofauti.), wawekezaji wa biashara, mkopo kutoka kwenye vyama au vikundi, mkopo kutoka kwenye mashirika ya fedha na mkopo kutoka benki na taasisi kubwa za fedha.

Milipuko ya magonjwa

Wafugaji wengi wamepoteza kuku wengi kutokana na magonjwa; wengine wamekata tama na kuiacha shughuli hii. Magonjwa kama ndui hutokana na kutofuata taratibu za kitaalamu, uzembe wa wafanyakazi na uchafu katika banda.

Fuata kanuni zote za ufugaji kwa kuwapatia chanjo muhimu kuku wako; hakikisha banda lako ni safi muda wote na wapatie chakula na maji safi wakati wote kuku wako. Kumbuka kinga ni bora kuliko tiba.

Soko la uhakika

Changamoto hii imekuwa kama wimbo kwa wafugaji wengi wa kuku. Wamekosa ni wapi wanaweza kuuzia bidhaa zao. Jifunze tabia za wateja wako wanataka nini hasa. Katika nyakati hizi soko la bidhaa linaweza kuwa ni kwa njia ya mtandao.

Masoko ni kitu muhimu katika biashara au huduma. Ili uweze kupata wateja sharti utoe huduma au bidhaa zenye kukidhi mahitaji ya wateja wako. Na kamwe usitegemee soko moja tu. Usifuge kibiashara bila lazima kujua utaanzia wapi.

Bei kubwa ya vyakula vya kuku

Hii ni changamoto nyingine kubwa ambayo inaendelea kuwatesa wafugaji wengi wa kuku. Jifunze kutengeneza chakula cha kuku wako ili kupunguza gharama. Fuata nafaka mashambani tengeneza mwenyewe ni nafuu na rahisi kuliko kununua.

Upatikanaji wa chanjo halisi

Wafugaji wengi wamekua wakilalamika juu ya kupoteza kuku kutokana na kukosa chanjo halisi. Penda kutumia wataalamu wa mifugo na wenye uzoefu pindi unapowapatia chanjo kuku wako. Jifunze pia kutumia dawa bora zaidi usikwepe gharama kwenye tiba ya kuku wako.

Ukosefu wa mabanda bora ya kuku

Wafugaji wengi wamezoea kufuga kwa mfumo huria pasi na mpango. Ukiamua kufuga kuku utatakiwa kujenga banda lenye sifa zitakazokidhi mahitaji ya msingi.

Banda bora la kuku linatakiwa kuwa na sifa zifuatazo;

•Liwe jengo imara

•Liwe rahisi kusafisha

•Nafasi ya kutosha kwa kuku waliopo

•Liweze kuingiza hewa na mwanga wa kutosha

•Lisiwe na joto sana au baridi sana

Baadhi ya tabia za kuku

Kuna baadhi ya tabia za kuku ni changamoto kwa wafugaji mfano kuku kudonoana na kuku kula mayai. Penda kujifunza nini chanzo cha tabia hizo. Sababu inaweza kuwa, tabia ya kurithi kutoka vizazi vya nyuma.

Inaendelea safu juu