UCHAMBUZI: Mdomo wa Manara na ubora wa Chama vinakosa kitu kimoja

Monday December 31 2018

 

By Nicasius Agwanda

Kwenye Uwanja wetu wa Taifa, nje kidogo kuna Uwanja wa Uhuru, pembeni kiasi kuna maduka na wapishi wengi wanaonufaika na uwepo wa michezo kadhaa ya ligi hususani michezo mikubwa. Upande mwingine ni uwanda wa wilaya ya Temeke unaokwenda mpaka Mbagala na kwingineko.

Hawa wote kwa pamoja huwa jirani kabisa na kelele za uwanja wa Taifa ambapo mabao mengi ufungwa na washabiki wenye matarumbeta na vuvuzela husikika wakiwa katika hali ya shangwe la kipekee.

Desemba 23 kwenye uwanja huo kulikuwa na tukio ambalo ungeweza kuliita la kitaifa kutokana na namna ambavyo liliteka hisia za watu wengi. Simba walikuwa wanacheza na Nkana Red Devils wakiwa nyumaya mabao mawili kwa moja waliyofungwa kule Zambia.

Na baada ya muda mfupi walikuwa nyuma kwa mabao matatu kw amoja baada ya Bwalya kfunga bao la kuongoza kwa upande wa Nkana. Hata hivgyo mechi ilimalizika kwa stori moja kubwa tu, nayo ni Claotus Chama maarufu kama “Triple C”.

Huyu ni mwanaume pekee kwa sasa Tanzania ambaye miguu yake ina akili inayojitegemea tofauti na ile iliyopo kichwani. Miguu yake inawaza kwa kasi kuliko vichwa vya watu wengi katika kufanya maamuzi akiwa ndani ya uwanja, na huyu anaweza kuupa amri mpira na ukampigia saluti mara moja. Ni mchezaji wa kiwango cha kipekee kabisa na ambaye anaweka mfano wa namna gani vilabu hivi inabidi vifanye “homework” vizuri kabla ya kusajili wachezaji.

Chama amekuwa mchezaji bora wa Simba akiwa kwenye eneo la kiungo na amewafunika mbali Emmanuel Okwi ambaye alikuwa ndiye mfalme wa Simba kwa karibu miaka nane sasa, na hata MK14 yaani Meddi Kagere naye hayupo katika uzungumzwaji sawa na chama.

Huyu ambaye aliwafanya Mbabane Swallows waamini walikuwa wamekutana na mchezaji anayeishi Pluto na kucheza soka Tanzania, anapatikana katika klabu ya Simba.

Nilikuwa bado najiuliza ubora wa goli lake na namna ambavyo sio tu kuwa aliwanyanyua vitini waliokuwepo uwanjani, bali Taifa zima kwa namna ambayo alikuwa amefunga goli lake.

Goli ambalo iwapo ungekuwa upande wa Nkana, unaweza kuamini umetoka kishujaa kwa sababu umefungwa goli lililojaa sifa za fizikia na ambalo linahitaji mazoezi yanayokiuka tabia mwili za binadamu, wazee wanaopenda kahawa wangeweza kukwambia kuwa yoyote mwingine akijaribu basi “Mtu asiyekuwa na kipaji na mazoezi angeteguka nyonga au kifundo cha mguu.”

Naam kuna vitu viwili vikubwa ambavyo viliambatana na goli hili la Claotus Chama, mdomo wa Haji Manara pamoja na halaiki ya wanasimba uwanja wa Taifa. Kila kimoja kina faida kwa kingine.

Kuna namna Manara anafanya kazi yake ambayo ni matokeo ya mdomo wake ambayo washabiki wengi wa Simba wanapenda. Na kuna picha kubwa ya wingi wa watu ambayo ilinijia kichwani siku hiyo.

Ukweli ni kuwa wachezaji wanauza, na unapokuwa na usajili mzuri kama waliofanya Simba ni wazi utajaza washabiki uwanjani na ni wazi pia kuwa Manara anaweza kuzungumza anavyotaka.

Kuna jambo moja tu linalokosekana kuunganisha mdomo wa Manara, Chama na mashabiki wa Simba nalo ni biashara. Sifikirii kumfundisha biashara MO Dewji ama kumfundisha kazi Sued Nkwambi au Magori lakini ile ilikuwa picha kubwa kuwa iwapo watakuwa makini utajiri kwenye vilabu upo.

Unapokuwa makini mtu kama Chama, Okwi pamoja na Kagere wanakupa biashara nzuri ambayo haikuwahi kufanyika kabla. Utauza jezi, skafu mpaka vikombe vyenye picha yao lakini pia kama utakuwa makini zaidi wachezaji pamoja na klabu zinaweza kunufaika kupitia haki za matangazo ya sura yao au matangazo ya biashara kupitia wao.

Kwenye mitandao ambako Manara anatamba kunaweza kutumika kuwakuza vilivyo pamoja na wenzao akina Manula, Nyoni, Ndemla na Mkude. Kipindi hiki Simba ambacho ipo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni kipindi ambacho washabiki wana hamu na klabu yao kuliko wakati wowote ule na wataendelea kujaza uwanja. Watumieni hawa, chumeni fedha zao za mfukoni kwa sababu wanachohitaji wao ni burudani na Simba inahitaji biashara.

Itakuwa ni jambo la ajabu iwapo kama ubora wa chama, magoli ya Kgere, Okwi na pasi murua za mkude kwenye klabu bingwa Afrika pamoja na mdomo wa Manara vitaendelea kukosa biashara ndani na nje ya uwanja. Simfundishi Mo ama mtu yoyote Simba biashara lakini nasema wasije kujisahau.

Advertisement