Mfungo wa Ramadhani kwa wenye kisukari

Mwezi mtukufu wa Ramadhani umeanza. Waislamu wote duniani wapo katika mfungo huu, ibada ambayo pamoja na mambo mengine inawataka wafunge kwa kutokula chakula kuanzia asubuhi na kufungulia (kula) jioni.

Hata hivyo, kuna watu wanaishi na kisukari na wangependa kufunga, funga ni dawa na wanatamani sana kushiriki katika hii ibada ila wanajiuliza watawezaje kufunga ilhali wanaishi na kisukari.

Yafuatayo ni mambo kadhaa muhimu sana ya kuzingatia kabla ya mfungo na wakiwa ndani ya mfungo na maisha baada ya mwezi wa Ramadhani.

Mosi, hakikisha ulijiweka tayari kwa mfungo miezi mitatu au minne kabla ya mfungo kuanza na ulifuata mfumo sahihi wa ulaji. Pia, hakikisha kama ulifanya mazoezi na kutumia dawa kama ulivyoshauri na daktari.

Pili, mshirikishe daktari wako kabla ya hujaamua kufunga; ni muhimu kushauriana na daktari wako, ufanye vipimo vyote vya sukari ili kujua kama hali yako na kiwango chako cha sukari kinaruhusu kufunga.

Kama kuna maradhi yanayotokana na kisukari, baada ya hapo daktari ataweza kukushauri kulingana na majibu ya vipimo vyako.

Pia, ni muhimu kuzingatia ushauri wa daktari, kama majibu ya vipimo vinaonyesha kufunga kutasababisha hatari kwa mfano sukari inaweza kushuka au kupanda sana na kusababisha matatizo makubwa kama kupoteza fahamu ni vyema ukafuata ushauri wa daktari.

Kipindi cha mfungo hasa wakati wa kufuturu ni muhimu kuzingatia ulaji sahihi, mara nyingi futari inahusisha aina mbalimbali ya vyakula na vingi huwa ni wanga na huwekwa sukari, kuwa makini sana wakati wa kufuturu, baada ya hapo pima kiwango cha sukari.

Hapo unaweza kutumia dawa kama daktari ameshauri, chagua aina ya futari ambayo haitapandisha sukari yako, kwa mfano upawa mmoja wa muhogo, kachumbari au mboga za majani na chai inaweza kuwa ya rangi au maziwa pasipo kuweka sukari, usitumie uji sababu ni wanga; muhogo pia ni wanga ni rahisi kupandisha sukari.

Mwandishi wa makala haya anaishi na kisukari, muelimishaji na mshauri lishe kwa wagonjwa wa kisukari