SIMULIZI ZA MUZIKI: Miaka 40 bila Mbaraka Mwinshehe Mwaruka

Jumanne 27 Juni, 1944, vita ya pili ya dunia ilikuwa bado inaendelea sehemu nyingi za dunia huko Morogoro siku hiyo alizaliwa mtoto wa pili wa Mzee Mwinshehe Mwaruka.

Mzee Mwinshehe Mwaruka alikuwa karani katika mashamba ya mkonge na hatimaye alikuja kupata watoto 12. Mzee Mwaruka alikuwa Mlugulu lakini mke wake alikuwa Mngoni.

Mtoto aliyezaliwa siku hiyo alipewa la Mbaraka. Kutokana maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa kabila la Wadoe wa Bagamoyo na alipelekwa Mzenga akawe Jumbe wa huko na wakoloni.

Alipofika huko mzee huyo alioa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo baba yake Mbaraka, Mzee Mwinshehe Mwaruka.

Mbaraka Mwinshehe alilelewa vizuri na kupelekwa shule, talanta yake ya muziki ilijitokeza zaidi alipoanza sekondari. Alianza kushiriki katika maonyesho ya Morogoro Jazz tangu akiwa shule, wakati huo alikuwa akipiga filimbi wakati bendi hiyo ikipiga nyimbo za mtindo wa ‘kwela’.

Mtindo huu wa kwela ulitoka Afrika ya Kusini, na ulipata umaarufu kutokana na wapulizaji mahiri wa filimbi na saxaphone kama Spokes Mashiyane.

Uchezaji wa muziki huu wa kwela uliitwa Jiving. Vijana walitengeneza makundi mengi ya kucheza jiving wakati huo na hasa katika shule za sekondari. Jiving ilikuwa ni mtindo wa kundi kuimba na kucheza kwa ‘steps’ zilizoigwa kutoka kwa wasanii wa Afrika ya Kusini zikisindikizwa na muziki wa filimbi.

Kwa zama hizi unaweza kulinganisha jiving na Kwaito.

Kila wikiendi Mbaraka alishiriki katika maonyesho ya Morogoro Jazz Band akiwa anapiga filimbi, wakati huo akiwa bado shule.

Ili kuhudhuria maonyesho haya Mbaraka alilazimika kutoroka bwenini kwake usiku siku za maonyesho. Hatimaye siku moja iligundulika kuwa yeye na wenzie kadhaa walikuwa wametoroka usiku, kesho yake walipewa adhabu ya kupigwa viboko mbele ya wenzao. Mbaraka aligoma adhabu hiyo na siku moja baadaye aliacha shule. Hiyo ilikuwa mwaka 1965. Mbaraka aliacha shule na mawazo yake yakiwa ni kuondoka Morogoro na kuelekea Dar es salaam kutafuta bendi ya kujiunga, lakini alipopita kwenye jengo la klabu ya Morogoro Jazz Band ili kuwaaga, wanamuziki waliokuwepo walimshawishi apumzike kwanza pale kwenye klabu ajifikirie uamuzi wake wa kuhamia Dar es Salaam.

Kesho yake wanamuziki walipofika klabu walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa wakimfahamu kama mpiga filimbi. Kwa kuwa wakati huo walikuwa na shida ya mpiga gitaa la rhythm walimsihi aachane na mipango ya safari ya Dar es Salaam na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm, akakubali.

Wakati huo katika bendi ya Morogoro ni wapiga tarumbeta, saxaphone na gitaa la solo pekee ndio waliokuwa wanalipwa mshahara kwa mwezi, wengine wote walipewa posho kidogo kila lilipopigwa dansi, hivyo Mbaraka nae akaingia katika mfumo wa kupewa posho kwa kazi yake. Siku moja Moro Jazz walialikwa Dar Es Salaam kwa ajili ya mashindano na bendi ya Kilwa Jazz, kulikuwa na utamaduni wakati huo wa bendi kualikana kufanya mashindano, lakini kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi mshahara, wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, mpiga solo ambaye alikuwa akilipwa shilingi 150 akaja juu na akagoma kwenda Dar kwa kusisitiza kuwa kwa taratibu za bendi hiyo, mpiga rhythm hastahili malipo. Bendi ikawa katika sintofahamu na hasa kwa kuwa kulikuwa na huo mwaliko wa mashindano.

Hatimaye Mbaraka akasema safari iendelee yeye angepiga solo, basi bendi ikaamua kwenda Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni bendi maarufu yenye nyimbo nyingi zilizopendwa nchini, na wao walikuwa wakienda bila mpiga solo.

Kwenye mpambano huo Mbaraka alilipiga vizuri sana gitaa la solo na Moro jazz ikashinda. Mbaraka akapandishwa mshahara hadi shilingi 250 kwa mwezi, kiwango ambacho kilikuwa juu sana wakati huo. na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo mkuu wa Morogoro Jazz Band Upigaji wake wa gitaa, mpaka leo bado ni darasa zuri sana kwa mpigaji anayetaka kujiendeleza katika upigaji wa gitaa la solo. Hata kwa kufanya mazoezi nyimbo zake nyingi alizorekodi ni zoezi kubwa sana kwa mtu anayetaka kujiendeleza katika upigaji wa gitaa la solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super Volcano alipitia staili nyingi za upigaji wa gitaa lake la solo, baadhi ya staili za bendi ya Morogoro kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika, zote zilionyesha upigaji tofauti kwa kila mtindo, haikuwa kubadili jina tu la staili, tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili muziki wenyewe. Hivyo staili ya upigaji wa solo katika staili ya Likembe ilikuwa tofauti na Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki walikuwa wakifunga safari kwenda Morogoro kufaidi wikiendi ya muziki kutoka kwa mojawapo ya bendi kubwa zilizokuwa katika mji huu, aidha Cuban Marimba, au Morogoro Jazz.

Januari 12, 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikisika kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha Mbaraka Mwinshehe, mpiga gitaa mwimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga kila wilaya ya nchini Tanzania. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia katika hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari. Siku hiyo ya tarehe 12 Januari 1979 mchana muda wa saa saba, Mbaraka akiwa katika mitaa ya Mombasa ndani ya gari aina ya Peugot 404 nyeupe iliyokuwa katika spidi kali gari lake liligongana na lori. Watu wakakimbilia kuangalia ajali, na mara moja watu wakamtambua Mbaraka aliyekuwa kiti cha mbele upande wa abiria. Maelezo ya baadaye yalimtambulisha dereva huyo kuwa alikuwa rafiki wa Mbaraka na mkazi wa Moshi aliyeitwa Omari Abdi, kuna maelezo mengine kuwa Abdi pia alifariki hospitalini, na abiria aliyekuwa kiti cha nyuma alifariki palepale. Mbaraka alikuwa amebanwa miguu na lile gari lililokuwa limebonyea, lakini alikuwa bado hai, baada ya kuondolewa alikimbizwa hospitali. Wanamuziki wa Kitanzania waliokuweko Mombasa, wakiwemo wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ya Mbaraka mwenyewe na wale wa Jamhuri Jazz Band walitaarifiwa kuhusu ajali ya mwenzao, ambaye baada ya kutolewa alipelekwa katika Makadara. Mbaraka alifariki masaa machache baadaye kutokana na kuvuja mno damu

Muda si mrefu Mbaraka Mwinshehe akafariki. Mbaraka alifariki 12 Januari 1979 akiwa na umri mdogo wa miaka 35 tu. Kwa kuwa mpaka wa Kenya na Tanzania ulikuwa umefungwa wakati huo kutokana na mgogoro kati ya serikali za nchi hizi mbili, mwili wa Mbaraka ulisafirishwa mpaka mpakani na kupokelewa na ndugu marafiki na Maafisa wa Wizara ya Utamaduni. Leo tumetimiza miaka 40 toka kifo cha nguli huyu aliyezikwa Mzenga Kisarawe. Nyimbo zake bado zinaendelea kufurahiwa na watu wengi.

Album yake ya mwisho ambayo aliihangaikia akiwa na ndoto ya kumaliza shida zake kwa kupata vyombo vipya ilikuwa na wimbo ulioitwa Shida. Kati ya maneno katika wimbo ule ni… Kila siku shida shida mpaka siku ya mwisho…. Mungu amlaze pema Mbaraka Mwinshehe Mwaruka

Mbaraka Mwinshehe hatimaye alizikwa Mzenga Kisarawe na alikuwa na watoto 12, ni yeye na wadogo zake Zanda na Matata ndio walikuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia nyimbo za kizungu katika bendi ya Morogoro na Matata alikuwa mpiga drum kwenye bendi hiyohiyo.