Miamba 8 ya Afcon U17 hii hapa

Oliver Albert, Mwananchi

Fainali za Afrika (Afcon) kwa vijana chini ya miaka 17 zitafanyika hapa nchini kuanzia Aprili 14 hadi 28 kwenye viwanja viwili; Uwanja wa Taifa na Azam Complex, Chamazi.

Mashindano hayo yanashirikisha timu nane ambazo ni mweyeji Tanzania, Senegal, Cameroon, Guinea, Angola, Uganda, Nigeria na Morocco.

Ifuatayo ni miamba hiyo ya vijana itakayotoana jasho:

Tanzania, Serengeti Boys

Imepata fursa ya kushiriki fainali hizo ikiwa mwenyeji kwani katika mashindano ya kuwania kufuzu mashindano hayo kutoka Cecafa ilimaliza nafasi ya tatu kwa kuichapa Rwanda penalti 4-3 baada ya sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90. Katika mashidnano hayo Uganda ilitwaa ubingwa.

Angola

Ilifuzu kucheza Afcon baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya kuwania kufuzu yaliyoshirikisha nchi zinazosimamiwa na Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (Cosafa).Angola ilianza kuifunga Malawi bao 1-0, iliichapa eSwatin mabao 4-0 na ilimaliza hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zimbabwe.

Katika mchezo wa nusu fainali iliichapa Namibia mabao 7-0 kabla ya kuichakaza Afrika Kusini kwenye fainali kwa ushindi wa bao 1-0. Imeshiriki fainali hizi mara tatu; 1997, 1999 na 2017.

Cameroon

Imeshiriki fainali hizo mara sita na mafanikio makubwa katika ushiriki wake ni kutwaa ubingwa mwaka 2003 nchini Swaziland (eSwatini) wakiichapa Sierra Leone kwa bao 1-0 katika fainali.

Mwaka huo pia walishiriki Fainali za Dunia na kuishia hatua ya makundi wakishindwa kupenya mbele ya vigogo Brazil na Ureno ambazo ziliongoza Kundi C .

Imefuzu Fainali za mwaka huu kupitia Kanda ya Afrika ya Kati kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Congo kwenye fainali.

GUINEA

Guinea imefuzu fainali baada ya kumaliza nafasi ya pili kupitia Shirikisho la Afrika Magharibi (WAFU). Iliifunga 3-1 Mauritania na ikatoka sare ya 1-1 na Cape Verde. Kwenye nusu fainali iliifunga Mali penalti 5-2 lakini ikafungwa 4-0 kwenye fainali na Senegal.

Imecheza mara sita fainali hizi mwaka 1995, 1999, 2003, 2009, 2015 na 2017.

MOROCCO

Morocco imefuzu Afcon kupitia Kanda ya Kaskazini mwa Afrika. Timu hiyo iliongoza kundi hilo baada ya kuibuka na ushindi kwenye michezo yote mitatu iliyocheza ikianza kushinda 5-2 dhidi ya Algeria, ikaifunga Libya bao 1-0 na mechi ya mwisho ikawachapa wenyeji kwa bao 1-0. Morocco haina mafanikio makubwa mashindano ya vijana ya U17 kwa Afrika na Dunia kwani wameshiriki Fainali za Afrika mara moja tu, mwaka 2013 na kuishia nafasi ya nne.

NIGERIA

Ni bingwa wa Kanda B wa mashindano ya kufuzu kwa nchi zinazounda Kanda ya Soka ya Afrika Magharibi.

Iliifunga Niger kwenye nusu fainali mabao 2-1 na mchezo wa fainali ikabuka na ushindi wa penalti 3-1 dhidi ya Ghana baada ya kutoka nayo sare ya bao 1-1 kwenye dakika 90.

Nigeria imeshiriki Afcon ya vijana mara nane ambapo kati ya hizo, imetwaa ubingwa 2001 na 2007 na kumaliza katika nafasi ya pili mara mbili na nafasi ya tatu mara moja.

UGANDA

Imefuzu baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.

Timu hiyo ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Ethiopia, iliifunga mabao 5-1 Sudan Kusini, iliichapa Kenya 3-0 kabla ya kuitandika Djibouti 8-0.

Timu hiyo ilitinga fainali kwa kuifunga Serengeti Boys mabao 3-1 katika nusu fainali na kutwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa kuinyuka Ethiopia 3-1 katika fainali.

Uganda haina mafanikio katika Afcon kwa kuwa ndio mara ya kwanza inashiriki fainali hizo.

SENEGAL

Inashiriki Afcon kwa mara ya pili. Ni moja ya timu imara katika fainali hizo kwani ina wachezaji wengi wenye vipaji vya soka wanaotamba duniani.

Senegal ilikata tiketi ya kushiriki Afcon mwaka huu baada ya kutwaa ubingwa kupitia Kanda B ya Chama cha Soka Afrika ya Magharibi (WAFU).

Senegal ilianza kuifunga Guinea Bessau bao 1-0, baadaye iliilaza Sierra Leone mabao 4-0. Nusu fainali iliifumua Cape Verde mabao 6-0 halafu ikainyuka Guinea 4-0 katika mchezo wa fainali.