Mikoa hii hatari kwa ufaulu kidato cha nne

Tuesday February 12 2019

 

Inawezekana Mkoa wa Kigoma ukawa upo mwisho wa reli, lakini usichokijua ni kuwa mkoa huo sio wa mwisho kimatokeo.

Tangu mwaka 2015 Kigoma imeungana na mikoa ya Pwani na Shinyanga kutamba katika orodha ya mikoa 10 yenye ufaulu bora katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.

Mikoa hiyo haijawahi kutoka katika orodha hiyo ambayo imekuwa ikishuhudia baadhi ya mikoa ikiingia na kutoka. Ipo iliyotamba lakini sasa imepotea kabisa katika ramani ya ufaulu.

Lakini pia ipo mikoa inayokuja kwa kasi ukiwamo Mkoa wa Simiyu ambao pengine unaweza kuleta ushindani kwa namna ufaulu wake unavyopanda kila mwaka. Mkoa huo umepanda kutoka nafasi ya 14 katika matokeo ya mwaka 2015 hadi ya tisa mwaka huu.

Mikoa inayotamba kumi bora

Kuanzia mwaka 2015 hadi 2018, mikoa ya Kigoma, Pwani na Shinyanga imeendelea kushikilia nafasi katika orodha ya mikoa bora kumi.

Mkoa wa Kigoma kwa mfano mwaka 2015 ulishika nafasi ya tatu. Mwaka uliofuata ukapanda kwa nafasi moja na kuwa wa nne. Katika matokeo ya mwaka 2017 na 2018 ulishika nafasi za 10 na ya tano mtawalia.

Vivyo hivyo kwa Mkoa wa Pwani ulioshika nafasi ya kwanza mwaka 2015 na hvyo kuwa kinara wa mikoa yote. Mwaka 2016 ukaporomoka hadi nafasi ya saba. Mwaka 2017 ukarudi katika chati na kuwa mkoa wa pili. Katika matokeo ya mwaka huu umekuwa wa saba.

Mkoa wa Shinyanga nao umeendelea kung’ara tangu mwaka 2015 ulipokuwa nafasi ya pili. Mwaka 2016 ulikuwa wa tisa. 2017 nafasi ya nne na mwaka huu nafasi ya tatu.

Mikoa iliyopotea kumi bora

Ni kama vile mikoa ya Iringa na Ruvuma imekubali kushindwa safari ya 10 bora. Baada ya kutamba miaka ya 2015 na 2016, mikoa hiyo imepotea katika orodha.

Mkoa wa Ruvuma kwa mfano mwaka huu umekuwa wa 20, mwaka 2017 ulikuwa wa 25. Awali mwaka 2015 mkoa huo ulishika nafasi ya saba na kisha 2016 kuwa wa nane.

Kwa upande wake, Mkoa wa Iringa umetoka kutoka nafasi ya pili tano mwaka 2015 na ya pili mwaka 2016 hadi kuwa nafasi ya 17 mwaka 2017. Mwaka huu angalau umejitutumua kwa kushika nafasi tano na kuwa wa 12.

Ingia toka ya Njombe

Mkoa wa Njombe una rekodi ya kuingia na kutoka katika orodha hiyo, huku ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kuwa mkoa wa kwanza mwaka 2016, japo mwaka mmoja nyuma ilikuwa ya 10.

Ingia toka ya Njombe inajidhihirsiha kwa kuwa mwaka 2017 iliteleza na kuwa ya 15 kabla ya mwaka huu kujitutumua na kuwa mkoa wa 10 kitaifa.

Simiyu inavyokuja kwa kasi

Taja kila sababu ikiwamo ya uongozi bora na mikakati imara, lakini ukweli ni kuwa Simiyu inakuja kwa kasi kitaaluma.

Kutoka nafasi ya 14 kwa miaka miwili mfululizo (2015 na 2016), Simiyu unaosifika kwa kuwa na uongozi wenye dira ya maendeleo, umepanda kwa nafasi nne na hivyo kuwa mkoa wa tisa mwaka 2018.

Ndiyo mara yake ya kwanza kuingia katika orodha ya mikoa kumi bora. Je, italinda rekodi yake? Tusubiri mwakani!

Mkoa wa Dar es Salaam ‘wasusa’ kumi bora

Pamoja na umaarufu wake na kuwa jiji kubwa zaidi nchini, Dar es Salaam, ni kama vile imeamua kutotaka kuingia katika orodha ya mikoa yenye ufaulu bora.

Kinachovutia zaidi ni kuwa kwa miaka hiyo yote mkoa huo umekuwa ukicheza kati ya nafasi ya 15 na 18.

Mikoa hoi zaidi Tanzania Bara

Hii ni mikoa ambayo tangu mwaka 2015, haijawahi kuwa katika orodha ya shule 10 bora wala 20 bora. Ni mikoa inayopaswa kujichunga hasa ikiwa inahitaji kuvutia wawekezaji katika sekta ya elimu.

Katika orodha hii kuna ipo mikoa ya Lindi, Mtwara, Mara na Dodoma. Mikoa hii imekuwa ikishika nafasi kama mabano:

Lindi: 2015 ( 27 ), 2016 (31 ), 2017 (27) 2018 (27)

Mtwara 2015 (25), 2016 (25), 2017 (20), 2018 (25)

Mara 2015 (21), 2016 (22), 2017 (23), 2018 (22)

Dodoma 2015 (22), 2016 (24), 2017 (19), 2018 (21)

Mikoa ya Zanzibar yaongoza kushika mkia

Unapokuwa na shule nyingi za mwisho kutoka eneo moja la nchi kila mwaka, mamlaka husika zinapaswa kujiuliza. Shule za Zanzibar zimekuwa zikiongoza kwa kuwa na shule nyingi zinazoburuza mkia kila mwaka.

Hali hiyo huathiri nafasi ya mikoa ya Zanzibar ambayo tangu mwaka 2015 imeshajiwekea makazi ya kudumu katika nafasi za mwisho

Advertisement