Mkulima anavyotakiwa kupambana na sera ya gesi nchini

Muktasari:

  • Gesi ni rasilimali muhimu ambayo inatarajiwa kuubadili uchumi wa Tanzania. Ili kuwashirikisha wananchi wote,

Uandaaji wa sera ya ushirikishaji na uwezeshaji wazawa Tanzania (LCP) ya mwaka 2014 una masharti ambayo mkulima inabidi ajipange ili kushiriki kwenye fursa za miradi ya gesi nchini.

Sera hiyo sanjari na Sheria ya Petroli ya mwaka 2015 na kanuni zake za mwaka 2017, inazielekeza kampuni za kigeni kushirikiana na za ndani pale zitakapohitaji huduma au ununuzi.

Sera hiyo inayolenga kuwawezesha Watanzania kiuchumi, haikuzingatia changamoto za ubora, uwezo wa kimitaji na elimu ndogo ya ushiriki wa fursa hizo kwa kusajili kampuni rasmi.

Kutokana na mazingira hayo, miradi ya gesi itakayoanza kutekelezwa miaka mitano ijayo, itawaweka kando wakulima wengi wasiokuwa na kampuni, mitaji ya kutosha pamoja na ubora hafifu wa mazao yao hatua itakayotoa mwanya kwa kampuni za kimataifa kuchukua nafasi hiyo.

Katibu mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa anasema kutokana na changamoto walizozibaini wameweka utaratibu kwa kampuni za kimataifa zinapokuja nchini kufanya kazi na wazawa na ikibidi kuwajengea uwezo kama hawana uwezo unaohitajika.

“Bila kufanya hivyo…nchi yetu haikuwa tayari ukilinganisha na Kenya lakini lazima tusukumane hivyo hivyo, huwezi kusema tutengeneze wafanyabiashara wakae tayari, lazima iendane na msukumo wa hali iliyopo,” anasema.

Mazingira ya kutengwa kwa mkulima yanaonekana kwa Saum Rufo, mmiliki wa kampuni ya Sageru Enterprises inayojihusisha na usambazaji wa matunda na mbogamboga.

Kanuni zinaelekeza kwamba kampuni ya ndani itakapothibitika kukosa uwezo basi ya kigeni itakayokuwa na mtaji wa kutosha kufanya biashara eneo hilo itaungana nayo kwa 7ya ndani kuchangia asilimia 25.

Endapo kampuni ya Sageru itakosa mtaji wa asilimia 25, kanuni zinaelekeza ipewe walau asilimia 5 hadi 15 ya mtaji wote unaohitajika kutekeleza zabuni iliyopo.

Lakini Saum anasema hana uwezo wa kufanya kazi inayohitaji mtaji mkubwa. “Nina ekari mbili tu na mtaji wangu ni Sh3 milioni, itabidi Serikali ituwezeshe ili tuzitumie fursa hizo,” anasema.

Mkulima wa nyanya katika Kijiji cha Igunda mkoani Iringa, Zubery Mwachulla anasema kwa uzoefu wa miaka kumi katika kilimo, anaamini mtaji ndiyo tatizo litakalowaweka kando wakulima wengi nchini kunufaika na fursa za uchumi wa mafuta na gesi.

Beng’i anasema ili kumsaidia mkulima, inatakiwa kutumia wafanyabiashara wa kati watakaonunua mazao yao kutokana na changamoto ya mitaji kidogo waliyonayo.

Meneja biashara wa kampuni ya Pan African Energy Tanzania Limited (PAT), Bizmana Ntuyabaliwe anasema kabla ya sheria na sera hiyo wamekuwa wakiwatumia wazalishaji wa ndani kupata huduma tofauti.

“Kama kuna akampuni ya Kitanzania imeshinda zabuni, tumeridhika na ubora wa huduma zake, tunaipatia hata asilimia 50 ya fedha ili ifanye kazi, lengo ni kuwawezesha wakue zaidi kimtaji,” anasema.

Hofu ya kampuni bandia

Kutokana na changamoto ya ukosefu wa mtaji wa kutosha kwa wazawa wengi, mkurugenzi mkazi kanda ya Afrika wa Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang’i anasema upo uwezekano wa kuanzishwa kwa kampuni ‘feki’ hapo baadaye.

“Sheria itawalazimisha lakini kitakachofuata watajaribu ku-manipulate (kughushi), hakutakuwa na uhalisia. Watatumia kampuni tanzu zao zilizopo nje na watazisajili kama suppliers wa ndani kwa jina la Kitanzania, zitazalisha na kuuza kwa viwango vinavyotakiwa, baada ya muda fedha zitarudi nje na wataondoka na maarifa yao bila kujenga kampuni za ndani,” anasema Olang’i.

Kapuni hizo, anasema zitaungana na wazawa zikisema zimewapa asilimia 50 ya hisa kumbe kiuhalisia ni asilimia moja tu.

Katika muda wa miaka mitano iliyobakia kabla ya kuanza kwa miradi hiyo ya gesi, Olang’I anashauri Serikali na wadau wanatakiwa kuanzisha vituo vya kutoa mafunzo.

Tahadhari ya Benki ya Dunia

Athari ya changamoto ya ubora na mitaji inajitokeza katika ripoti ya Benki ya Dunia (WB) kuhusu ushiriki wa kampuni za ndani katika ujenzi wa LNG, inayoonyesha takriban Dola 1.4 bilioni tu kati ya Dola 17 bilioni ndizo zitabakia nchini kwa ajili ya ununuzi wa huduma na bidhaa.

Novemba mwaka jana, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alikiri kukosekana kwa tija kwenye kilimo nchini kwa sababu wakulima wengi hawana elimu ya kutosha.

Kaimu mtendaji mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Edmund Massawe anasema kuna takriban wakulima 800,000 wanaozalisha matunda na mbogmboga ambao wengi huzalisha kwa kuongeza viwatilifu hali inayafanya yasikubalike kwenye masoko ya kimataifa.

“Tunachokifanya kwa sasa ni kuwafundisha ili wazalishe kwa njia bora bila kutumia dawa ili kukuza na kuongeza ubora wa mazao,” anasema.

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Jacquiline Maleko anasema ubora wa mazao unaanzia kwenye maandalizi ya shamba kabla ya kulima mazao husika.

“Mtu anahitaji nyanya zinazofanana rangi, zenye content moja na uzito sawa, usipofanya hivyo, huwezi kuwa na nyanya zenye ubora, huwezi kushindana na waliotumia teknolojia sahihi, tatizo wakulima wanaona ni gharama kutumia teknolojia, hatutaweza kushindana,” anasema.