Mnyororo wa thamani katika sanaa ni mdogo

Saturday February 9 2019

 

Mapema mwaka huu Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), iliitisha kikao cha wadau kufikia muafaka wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na miito ya simu. Waliokuwepo katika kikao hicho walikuwa wanamuziki na wawakilishi wa kampuni za simu na wasambazaji wa muziki kidijitali.

Kikao hicho kilianza kwa wasilisho fupi kuhusu mnyororo wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na biashara ya miito ya simu. Baada ya wasilisho hilo wajumbe walipewa fursa ya kujadili wasilisho hilo. Lilikuwa jambo lenye nia njema.

Wawakilishi wa kampuni za simu walitoa maelezo yao jinsi wanavyofikia na hata hatimaye kupanga namna wanavyogawana mapato hayo ya muziki na wenye muziki wao.

Kampuni hizo zilikuwa na viwango tofauti vya mgawo, nyingine zikigawana nusu kwa nusu na wenye muziki wakati kampuni nyingine zikiwa na kiwango tofauti hata kufikia mgao wa asilimia 70 kwa kampuni ya simu na 30 kwa wenye muziki.

Wanamuziki walipewa nafasi ya kutoa mapendekezo ya mgawo na wengi walipendelea kupata asilimia 70 ya mapato yatokanayo na nyimbo zao. Hatimaye TCRA ilitoa uamuzi kuwa kati ya sasa na Juni, wanamuziki wapewe asilimia 50 ya fedha zozote ambazo zimetokana na kazi zao zilizoingizia fedha kampuni za simu.

Pia, TCRA ilitaka wanamuziki wowote ambao walikuwa na mikataba ya muziki kutumika kidijitali, na hawajalipwa wapeleke mikataba hiyo, ili ionekane namna ya kulipwa stahiki zao. Hakika kwa juu picha inaonekana nzuri sana. Lakini kuna mambo ambayo haya kwenda sawa katika hadithi hii.

Pamoja na kuwa kulikuwepo na watu waliojaribu kuieleza TCRA kuwa kuna tatizo, lakini hakika ilionekana wazi haikuwa tayari kusikiliza mawazo hayo. Tuangalie mambo yaliyokuwa na matatizo.

Jambo la kwanza ambalo halikuwa sawa ni kukosekana kwa Cosota (Chama cha Hakimiliki Tanzania) katika mkutano huo.

Kwanza Cosota haikutajwa katika wasilisho la TCRA lililoanzisha mjadala na pili - hakukuwa na mwakilishi aliyealikwa kutoka Cosota, japo Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) liliwakilishwa.

Hilo ni tatizo kwani moja ya kanuni za sheria ya hakimiliki na hakishiriki inaeleza nafasi na majukumu ya Cosota katika suala la matumizi ya muziki kidijitali.

Kanuni hii inataja kuwa Cosota ndio mamlaka ya kutoa leseni kwa wafanyabiashara wa muziki katika eneo la dijitali na ina maelekezo mengine mengi kuhusu utekelezaji wa ulinzi wa kazi za muziki kidijitali.

Cosota ina uzoefu ambao ungetoa msaada mkubwa katika kutoa elimu ya ukusanyaji wa mirabaha katika eneo hili, na pia kuelezea changamoto na kujibu maswali ya utendaji wa chombo hicho kuhusiana na suala hili.

Jambo jingine kubwa lilikuwa ni kukosekana kwa wadau wengine muhimu katika mnyororo wa thamani yaa muziki.

Kwa bahati mbaya wasilisho na mtizamo wa waliotayarisha kikao ilionekana kuwa muziki ni mali ya mwanamuziki tu, hata hivyo angalizo lililotolewa kuwa muziki siyo lazima uwe wa mwanamuziki. Wazo hilo lilitupwa pembeni na wanamuziki waliokuwepo walishangilia kwa nguvu.

Ni kweli watu wengi hudhani muziki ni mali ya mwanamuziki tu, hasa katika zama hizi ambazo huimba peke yake na kupata umaarufu. Katika mazingira ya hakimiliki hali si rahisi hivyo.

Labda nitaje watu wengine muhimu mpaka wimbo na mwanamuziki akapendwa.

Kuna watunzi wa muziki ambao wanaweza kuwa si wanamuziki au watu maarufu kwa mfano watayarishaji, watunzi wa mashairi ambao si lazima wawe wanamuziki, waliogharamia kutengeneza, watanganzaji wa kazi (promoters) - wote hawa wanaweza wakahusika katika wimbo mmoja au sehemu ya utengenezaji wa wimbo.

Halafu kuna vikundi vya muziki ambavyo wanamuziki wake wameajiriwa kwa mikataba maalumu, kwa wanamuziki wa aina hii pale ambapo inalazimishwa kuwa mapato yote ya mirabaha yagawiwe wanamuziki, moja kwa moja ni kuanzisha ugomvi mwingine na hawa wadau wengine ambao mirabaha inayopatikana ama ni yao au wanastahili sehemu ya malipo hayo.

Kuanzia mwanzoni mwa mwaka 2000, ndipo zilipoanza kuonekana kampuni zilizoingia mikataba ya haki za kidijitali na wanamuziki.

Sehemu mojawapo ya mkataba ulikuwa unasema kuwa umeingia mkataba na mwanamuziki kwa kazi zote atakazozalisha kuanzia siku aliyoingia mkataba na miaka kumi baada ya hapo.

Lakini kampuni hii imekuwa ikipiga chenga kutoa malipo hata ya hiyo kazi moja ambayo imeipokea. Na kuna wanamuziki na vikundi vya muziki vingi vinavyolalamika kuona kazi zao zikitumika kwa biashara katika mitandao, lakini wahusika wakiwa hawajulikani.

Kumekuwa na usiri mkubwa wa mapato yanayopatikana kutokana na kampuni za simu kutumia kazi za muziki. Kwa nini kuwe na usiri?

Nimalize kwa ushauri, kwa kuwa TCRA imeonyesha nia ya kutaka kuwasaidia wanamuziki na hivyo kusaidia tasnia nzima ya muziki, ni vizuri ishirikiane kikamilifu na vyombo vilivyopo, hasa vilivyotajwa kisheria ili kupata njia sahihi ya kutekeleza jambo hili jema.

Kumbuka kati ya mambo yanayokwaza maendeleo ya sanaa nchini ni matamko na maelekezo yanayotoka kwa wanaodhani wanafahamu majibu ya matatizo ya sekta hii na hivyo wanaitendea haki, wakati hawajafanya utafiti wowote.

Advertisement