Mohamed: Kutokuwapo CUF hakujazuia nguvu zetu Barazani

Muktasari:

Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi imejinasibu kwa kufanya mambo kadhaa ikiwamo kupandisha mapato ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti wao, Dk Mohamed Said Mohamed wiki iliyopita walitembelea ofisi za Mwananchi na kufanya mahojiano kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi. Endelea

Swali: Kamati unayoongoza haina muda mrefu katika Baraza la Wawakilishi, imeanza lini na nini malengo yake?

Mwenyekiti: Kweli, Kamati ya Bajeti haina muda mrefu imeingia huu mwaka wa pili, mwanzo haikuwepo. Awali bajeti ilikuwa inajadiliwa na wenyeviti wa kamati zote, katika wenyeviti wale anachaguliwa mmoja anakuwa ni mwenyekiti wa wenyeviti na ilijadiliwa kwa siku moja. Ikaonekana haiwezekani bajeti nzima kujadiliwa siku moja.

Ikaundwa kamati hii, ina wajumbe saba na makatibu wanne. Umuhimu wake ni kuichambua bajeti na kuishauri Serikali kuhusu bajeti na kuhusu kodi.

Swali: Kwa kipindi cha miaka miwili mambo gani muhimu mmefanya katika Baraza yanayoonyesha umuhimu wa kamati yenu kuliko mfumo wa zamani?

Mwenyekiti: Tumefanikiwa kuishauri Serikali kuhusu kodi na bajeti ya Serikali kuweka bajeti ya maendeleo iwe bajeti hali kwa wananchi. Unajua kuwa bajeti ya mwananchi ikifika asilimia 45 au 50 kwenda moja kwa moja kwa wananchi, ndiyo tunasema ni ya wananchi.

Tunafuata ilani ya CCM kuona bajeti ya Serikali ya Mapinduzi inatekelezeka katika zile hatua zinazofaa, tunakagua bajeti ya Serikali kila baada ya miezi mitatu kuona yale tuliyoyapitisha yamefika vipi kwa wananchi.

Swali: Katika taarifa ya kamati ya 2017/18 mlizungumzia tofauti kati ya mapato ya Serikali na matumizi ikaonekana matumizi yanakuwa makubwa kuliko mapato. Mfano, katika kipindi cha Oktoba - Desemba makusanyo yalikuwa Sh182.29 bilioni lakini matumizi yalifika bilioni 204, Serikali iliwaelewa?

Mwenyekiti: Ndio ilituelewa na ndio maana sasa mapato na matumizi yanakuwa sawa. Mwanzo matumizi yalikuwa makubwa sana kuliko mapato. Baada ya kuundwa kwa kamati hii mapato yameongezeka kuliko ilivyokuwa mwanzo. Mafanikio hayo yametokana na ushauri na umahiri wa kamati yake, ikiwamo kuziba mianya ya kupotea kwa mapato.

Swali: Moja ya kazi za kamati ya bajeti ni pamoja na kuongeza mapato ya Serikali kwa kubuni vyanzo vipya, ya kwako imefanyaje katika hilo?

Mwenyekiti: Tumeanzisha vyanzo vipya vya mapato ikiwamo wanaoagiza magari wanapobadili nyaraka kuwa kwenye umiliki wao kwa kulipa gharama kiasi.

Mbali na hilo kuweka namba binafsi kulipia kutoka Sh5 milioni hadi Sh15 milioni na watalii kulipia gharama za mazingira ambapo kila anayeingia hulipa dola moja. Ndiyo maana umeona tumeanza kuimarika zaidi .

Swali: Mmefikia wapi kuhusu wazo la kuwa na eneo moja la kuhudumia wawekezaji katika Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (Zipa)?

Mwenyekiti: Kila kitu kipo sawa, bado mambo mawili matatu kutoka Zipa, lakini wawakilishi wa idara zote zinazohusika na biashara wana wawakilishi wao pale, ili mwekezaji anapokuja asipate taabu ya kuhangaika kukusanya nyaraka, badala yake kila kitu akipate katika eneo moja.

Swali: Suala la kuwa na eneo huru la uwekezaji, mmekuwa mkiligusiagusia mmefikia wapi?

Mwenyekiti: Kuhusu kuwa na eneo huru la uwekezaji Zanzibar bado ni changamoto kutokana na bidhaa zinazoingia Tanzania Bara zilizozalishwa Visiwani zinatozwa ushuru, ilihali za Bara zinaingia bila kutozwa.

Tumekuwa tukilijadili sana na kwa sasa wamewaachia mawaziri wawili wa Bara na Visiwani kulijadili na kuja na jibu lenye tija.

Swali: Suala la sukari ya Zanzibar kutouzwa Bara lipoje?

Mwenyekiti: Kiwanda cha Mahonda kinauza sukari vizuri na wamepangiwa mpango maalumu wafanyabiashara wa sukari Zanzibar wanunue kwanza ya kiwanda hicho kabla ya kuleta kutoka nje. Hivyo kama ya ndani ipo, ukileta ya nje hauruhusiwi kuuza.

Swali: Mara kwa mara Zanzibar kunaibuka upungufu wa mafuta, nini tatizo?

Mwenyekiti: Tatizo ni meli kwa sababu zilizopo zina leyer moja. Kama inavyofahamika meli ya mafuta yenye leyer moja hairuhusiwi kuingia bandarini kwa sababu ikitoboka mafuta yanakwenda moja kwa moja baharini, hivyo kuhatarisha usalama wa bahari.

Lakini yenye leyer mbili moja ipo kerezoni, nyingine iliyobaki ikifanya kazi imeharibika kabla iliyokuwa kerezoni haijalirudi.

Tulikuwa tunatumia meli ya Kenya ZP ambayo nayo ina leyer moja, hairuhusiwi kuingia bandarini.

Suluhisho la kudumu la mafuta ni kuwa na akiba ya kutosha ikiwamo kuwa na miundombinu ya kuhifadhia itakayowezesha hilo.

Swali: Hamjafikiria kuifanya biashara ya mafuta kuwa huria Zanzibar?

Mwenyekiti: Hata tukiruhusu, kwa sasa hivi haitaweza kwa sababu hakuna miundombinu ya kutosha ya kuhifadhia mafuta.

Swali: Hamuoni nguvu yenu ya kuishauri Serikali imepungua baada ya kukaa pembeni kwa CUF tangu 2015?

Mwenyekiti: Sidhani kama imepungua ukifanya tathmini ni kama imezidi zaidi watu wanachangia bila ya woga na vyama vitatu vilivyopo vinachangia kuisukuma Serikali.

Swali: Kwa hiyo wewe binafsi unaonaje, mbaki kama mlivyo au kuwepo na CUF muendelee kushindana?

Mwenyekiti: Vyovyote sawa, hata wakija tunaweza tukafanya kazi, lakini hata kikiwepo chama kimoja tunaweza tukafanya kazi zaidi.