Msaada wa mzazi kwa mtoto aliyefeli

Tuesday February 5 2019

 

By Christian Bwaya, Mwananchi

Siku chache zilizopita, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka 2018.

Kwa mujibu wa uchambuzi wa kitakwimu uliofanywa na gazeti hili Januari 29, watahiniwa 113,825 wamefaulu kwa kuanzia daraja la kwanza hadi la tatu hivyo kujihakikishia nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tano.

Watahiniwa 170, 301 sawa na asilimia 47.5 walipata daraja la nne huku waliofeli kabisa wakiwa 74, 301 sawa na asilimia 20.7. Hawa wamekosa fursa ya kuendelea na kidato cha tano kwa kuwa wameshindwa kufikia ufaulu wa japo kuwa na alama C katika masomo matatu ya msingi.

Wakati wazazi wengine wakifanya sherehe kwa kuona fahari watoto wao kuongoza kwenye mitihani, labda wewe hujui ufanye nini baada ya matokeo hayo kutangazwa hasa ikiwa mwanao ni mmoja katika maelfu ya watahiniwa waliofanya vibaya..

Makala haya yanalenga kukutia moyo wewe mzazi mwenye mtoto aliyefanya vibaya na kukusaidia kuona kile unachoweza kukifanya katika nyakati ngumu kama hizi.

Usimkatie mtoto tamaa

Inawezekana ulifanya jitihada nyingi kumsaidia mwanao afanye vizuri kwenye masomo. Pengine ulimtafutia shule ya gharama kubwa, na huenda ulimfanyia mpango apate masomo ya ziada.

Huenda hukukaa kusubiri akuletee ripoti ya maendeleo yake nyumbani, uliwasiliana na walimu wake kufuatilia mwenendo wake.

Inawezekana wakati mwingine ulipita kipindi kigumu kimaisha katika kuhakikisha mtoto anaenda shule. Ulisimamisha mipango mingine na labda ulikopa pia. Lengo lilikuwa kumtengenezea mwanao maisha yake.

Pamoja na jitihada zote hizo, mwanao amefanya vibaya. Inaumiza. Unapotafakari juhudi zote ulizofanya unaweza kujikuta unamkatia tamaa mtoto. Usifanye hivyo.

Mtoto anapofeli, hayo tayari ni maumivu ya kutosha kihisia. Anapojilinganisha na wenzake waliofanya vizuri anajisikia ni mtu dhalili asiye na thamani kama wenzake. .

Katikati ya maumivu kama haya, inapotokea na wewe mzazi wake unamrushia lawama, hali inaweza kuwa mbaya zaidi na ikaharibu kabisa maisha yake.

Nafasi yako kama mzazi katika kipindi kama hiki si kukoleza moto unaowaka tayari hata kama ni kweli kuna uzembe mwanao alifanya.

Fanya wajibu ambao pengine hakuna mtu mwingine anaweza kuufanya. Wajibu huo ni kumuonyesha mwanao kuwa bado una imani naye.

Mpe nafasi ya kujipanga upya

Kuna mtu mmoja mwenye hekima aliwahi kunieleza: “Katika maisha wakati mwingine unahitaji kupita kwenye tanuru liwakalo moto ili uweze kupiga hatua moja mbele.” Wakati huo sikumwelewa lakini baada ya kushuhudia mengi tangu wakati huo, nimekubaliana naye.

Kufeli kwa mwanao kunaweza kuwa tanuru linaloweza kumchonga apate akili za maisha. Wakati mwingine unaweza kuwa unaongea na mtoto kuhusu umuhimu wa kujituma na hakuelewi kwa sababu haoni kama kuna uwezekano wa kufeli.

Inapotokea amefanya vibaya, maumivu yale yanakuwa kichocheo cha kumfanya auone ukweli uliomweleza siku zote. Pengine alijihesabu kuwa mtu mwenye akili nyingi asiyehitaji kusoma kwa bidii ili kufaulu. Sasa anaweza kuelewa kumbe hakuna mafanikio yasiyoambatana na jitihada.

Tumia kufeli kwake kama fursa. Wakati anaendelea kuona aibu kwa kufanya vibaya, msaidie kujipanga upya. Muonyeshe fursa alizonazo ikiwa atakuwa tayari kujifunza upya.

0754870815

Advertisement