Mtandao wa Whatsapp ulivyowarudisha shule kina Magda

Machi 15 asubuhi Magdallena Julius na mdogo wake Hellena Julius waliungana na wanafunzi wengine wa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Serengeti kuanza safari ya kutimiza ndoto zao za kuwa walimu.

Safari hiyo ya miaka minne wameianza ikiwa ni siku tatu tangu gazeti la Mwanachi la Machi 12 kutoa taarifa ya hali ngumu ya familia yao iliyowalazimu watoto hao kushindwa kuanza masomo.

Hata hivyo, kilio cha familia hiyo cha kuomba kusaidiwa kiasi cha sh 500,000 kwa ajili ya mahitaji ya shule ikiwamo matengenezo ya viti,meza,michango ya mahindi,sukari sare na vitu vingine kiliwagusa wasomaji wa gazeti la Mwananchi na kuamua kuwasaidia.

Ni wasomaji waliohamasishana kupitia mtandao wa kijamii wa Whatsapp na siku mbili baadaye fedha zilichangwa na kupelekwa kwa watoto hao wanaoishi Serengeti mkoani Mara.

Magda kama walivyozoea kumwita kwa sauti ya utulivu anasema:”Naanza kuona mwanga mbele yetu, nawashukuru walioguswa na matatizo yetu na kutuchangia. Zawadi kubwa tunayoahidi ni kufanya vizuri katika masomo,”anasema.

Anasema licha ya kuchelewa kuanza masomo lakini anaamini watafanya vizuri kwa kuwa hata shule ya msingi hawakuwa na muda mzuri wa kusoma kutokana na matatizo mengi ya kifamilia.

“Pamoja na ugumu wa maisha ikiwamo kutumia kibatari kujisomea, tutakuwa tunajisomea ingawa suala la twisheni litakuwa gumu “anasema kwa sauti ya kugugumia.

Kwa upande wake, Hellena huku akisita sita anasema:”Mungu amesikia kilio chetu,baba atapata amani kila siku tulipokuwa tunamuuliza lini tutaanza masomo alionekana kuumia kutokana na kutokuwa na uwezo.

Bweni ingependeza

Pamoja na kushukuru kwa msaada mkubwa walioupata, Magda mwenye uwezo mkubwa wa kujieleza, anatamani kama watawezeshwa kusoma katika mazingira ya bweni ili wapate muda mzuri wa kujifunza.

“Tunashukuru mwandishi wa habari aliyefika kutuona na kuandika leo tunapata msaada kutoka kwa watu tusiowajua. Kama walivyoanza waendelee kutushika mkono ili tuweze kumaliza shule,”alisema.

Mmoja wa walioguswa na kilio cha watoto hao ambaye hakutaka kutaja majina yake, anasema mchango huo umefanikiwa kupitia kundi lao la Whatsapp.

‘’ Tumefanikiwa kurejesha nuru ya watoto hawa maana hatujui kesho watakuwa nani,”anasema na kuongeza kuwa waliguswa na habari hiyo hivyo hawakuona ajizi kuwasaidia.

Baba azungumza

Alikuwa na huzuni lakini sasa anatabasamu. Akiwa na uso wa bashasha baba wa wanafunzi hao Nyangie Mataro anasema:”Amani nyumbani imerejea, nilifikia ukomo wa kufikiri. Nashukuru walioguswa na tatizo langu na gazeti Mungu awabariki sana.’’

Anasema maswali ya mara kwa mara ya watoto wake kutaka kujua lini wataenda shule yalimfanya kufikia hatua mbaya na kuanza mipango ya kuuza eneo pekee analolimiliki.

‘’…kama kukopa sikopesheki kwa kuwa sina dhamana; nilijipanga kuuza eneo tunalolima bustani ili watoto waende shule,”anasema.

Licha ya ugumu wa maisha lakini dhamira yake ya kuwaendeleza watoto wa kike iko wazi ndio maana awali alijitahidi kusomesha dada zake kina Magda.

Mdau wa elimu, Byabato Wincheslaus, anasema kilichofanywa na wadau hao kinapaswa kuwa utamaduni wa Watanzania.

Anaiasa jamii kuwa na tabia ya kuchangiana nje ya michango iliyozoeleka ya harusi, siku ya kuzaliwa na ubarikio.

Mkuu wa shule Baraka Sabi akiwapokea watoto hao, aliwashukuru walioguswa na matatizo ya watoto hao na kudai pamoja na kuchelewa kuripoti anaamini watafanya vizuri.

“Wengine wameishamaliza hatua za mwanzo na wameishapata mitihani ya majaribio ili kupima uwezo wao,hawa tunawapokea na kuwachukulia kwa uzito wa pekee maana tunao wenye changamoto kama hizo,”anasema.

Magda na familia yake ni sehemu ya familia zilizohamishwa kutoka eneo la Nyamuma mwaka 2001. Wazazi wamekuwa wakiishi maisha magumu huku watoto wao wakijikimu kimaisha kwa kuchunga ng’ombe na kuvuta mikokoteni.