Mume wangu ni mzuri wa sura lakini mbaya wa mambo

Sunday February 10 2019

 

By Anti Bettie

Nashukuru nimepata mume mzuri ninaweza kumbusu hadharani, anajali na ananipenda. Tatizo lake hanifanyii ninavyovipenda.

Sitaki kuzungumza Anti nitakuwa muongo, mume wangu mzuri wa sura mbaya wa mambo.

Nimevumilia nimechoka na sitaki kufanya dhambi kwa kutafuta wa kutii kiu yangu.

Nifanyeje?

Usikubali mumeo awe wa maonyesho, anatakiwa awe mkali wa vitendo hususani kukata kiu yako. Anayepaswa kumpa hayo makali ni wewe, kama hakuridhishi unakaa kimya na kukubali kufa Kizungu na tai shingoni hawezi kujua.

Kuanzia sasa usipotosheka mwambie, asipofika unakotaka ahirisha tukio...kaa pembeni kabisa, akikuuliza kwa nini mueleze wewe unapenda dansi yeye anakupigia mnanda, ukifanya hivyo mara mbili atakuelewa.

Usikubali kujipunja, huyo ni mumeo mweleze akikugusa wapi unaridhika, usijilazimishe furaha usiyokuwa nayo mbele yake. Akikununulia baga, askrimu ukila hakikisha unalalamika...ungekuwa unanipa vitu vitamu kama hivi faragha...Hapo atajua ni kwa namna gani una kiu na bado hajaifikia hata robo.

Hataki kujishughulisha

Anti habari, pole na kazi. Nimebahatika kuoa na nina watoto wawili. Mke wangu ananipasua kichwa kwa sababu hataki hata kusikia neno kufanya kazi au biashara.

Kibaya zaidi amesoma na ana ujuzi. Nifanyeje?

Pole sana. Inawezekana unampa fedha nyingi za kujikimu ndiyo maana haoni haja ya kujishughulisha, au kwao kuna fedha hivyo hana majukumu.

Pia angalia uwezo wa akili yake katika kufikiri, kwa sababu kuna watu wana vitu vyote hivyo na bado wanatafuta namna nyingine ya kuingiza fedha.

Zungumza naye kwa kituo inawezekana ana matatizo ya kisaikolojia kuhusu kufanya kazi au biashara, mweleze faida za kutafuta kipato chake binafsi kwa maisha ya sasa na yajayo.

Ukishindwa kuzungumza naye wewe, mtafutie mtaalamu wa masuala ya uchumi na fedha ili ampe darasa.

Nakukumbusha angalia pia uwezo wake wa kuelewa mambo, kabla hujamtafuta mtaalamu wa kuzungumza naye, mfahamishe ajue anazungumza na mtu wa aina gani.

Advertisement