Munalove kumuenzi mwanaye Patrick kwa filamu

Saturday October 12 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Mwigizaji filamu, Rose Alphonce maarufu kwa jina la Munalove,baada ya kusononekana kutokana na kufiwa na mwanaye Patrick ameamua kumuenzi kwa filamu.

Patrick alikua maarufu katika mitandao ya kijamii kutokana na mavazi ya aina mbalimbali aliyokuwa anavaa, alifariki Julai 3, 2018 nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya miguu aliyoanza kuugua tangu mwaka 2016. Katika uhai wake alifanyiwa operesheni tano akiwa amelazwa Taasisi ya Mifupa (Moi), kabla hali haijabadilika tena na kupelekwa nchini Kenya kwa matibabu zaidi ambako alifikwa na umauti.

“Najipanga kufanya usaili ili kumpata mtoto wa kiume atakayeigiza nafasi ya Patrick,” alisema Muna.

Alisema kwenye filamu hiyo kutakuwa na baadhi ya picha za marehemu mwanaye alipokuwa hospitali kwenye chumba cha uangalizi maalum jijini Nairobi, Kenya. Alifafanua kuwa ataitumia filamu hiyo kueleza magumu aliyopitia hadi kufikia uamuzi wa kuokoka na namna alivyomuuguza mtoto wake kwa matumaini hadi anafikwa na umauti.

Kuhusu kushutumiwa kufanya mambo yasiyoendana na ulokole Munalove aliyewahi kuigiza filamu za ‘Born to Suffer’, ‘Siri ya Mapenzi’ na ‘Hukumu ya Tunu’ alisema:

“Wokovu si mavazi ni moyo na nitaendelea kupendeza na kumtukuza Mungu ilimradi sitoki kwenye kusudi lake. “Hao wanaosema na kuonyesha shaka na maisha yangu wanapaswa kuelewa kwamba imani yangu ni kubwa mno kuliko wanavyofikiria na hata waliokuwa wanasubiri niishie njiani katika safari yangu ya wokovu watasubiri sana,” alisema Munalove mwenye michoro mitano mwilini mwake.

Advertisement

Kuhusu ndoa alisema, “Sihitaji ndoa wala mwanaume, kwa sasa ninamtumikia Mungu kwa sababu sijamlipa kwa mema aliyonitendea.”

Advertisement