HOJA BINAFSI: Mungu wa Bongo na mambo yake

Sunday September 9 2018

 

Hamwamini kwamba Mungu bado anaongea na watu wake? Au anaongea na hata wasio wake? Basi hebu angalia hii barua nyie washambenga. Jana nilipoamka asubuhi nikaikuta inapeperushwa na feni. Sasa baada ya kuikamata, ikabidi nitetemeke kidogo, lakini hebu niwaambie kweli, hata nyinyi mnaojidai mnaongea na Mungu kumbe mnaongea na nafsi zenu. Utasemaje umepokea barua kutoka kwa Mwenyewe.

Mwanzoni sikuamini lakini nilipoangalia nikakuta kwamba mlango na madirisha yote yamefungwa. Nikamuuliza mama watoto kama ameamua kunitania lakini alivyotetemeka nilipomwonyesha hii barua nikajua hatanii. Hapo kwenye bahasha iliandikwa waziwazi kabisa, kwa maandishi kama yale tuliyofundishwa zamani.

WARAKA KUTOKA KWA MWENYEZI MUNGU KWA MDHAMBI MAKENGEZA

Duh! Hata mimi nilitetemeka lakini ikabidi niifungue na kusoma.

Wewe Makengeza, usijidai kwamba nimekuandikia wewe. Wewe si mtakatifu lakini nimegundua pia kwamba si mtakavitu pia. Nimependa hii. Pili, naona hujapenda kujiunga na Wafarisayo wanaodai kutenda mema kumbe wanatenda noma.

Hapo ikabidi mama watoto aingilie:

‘Hivi kweli huyu ni Mungu? Mbona lugha yake …’

Mke wangu akacheka.

‘We Bwana unafikiri Mungu ni mrasimu au mrasumu? Anaishi na watu, anatumia lugha ya watu. Nadhani angekuja leo, warasumu wala wasingemtambua.’

Akatabasamu.

‘Labda ndiyo maana amekuandikia wewe maana anajua lugha yako pia ni sumu ya urasimu. Lakini itabidi uniambie haya madhambi anayosema ni yapi.’

‘Ohoo mke wangu, nimeletewa barua na Mwenyewe mwenyewe wewe unajisumbua na mambo madogo. Sisi sote ni wadhambi. Ila wengine wanajiona wateule badala ya wadhambi.’

Tukaendelea kusoma.

Makengeza nakuandikiwa kwa sababu nimechoka! Nimechoka na kuchokaga. Yaani binadamu wakitaka kufanya maovu, nawaelewa, ndiyo hulka yenu, lakini kunihusisha na maovu haya … sikubali kabisa.

Sitegemei kwamba wewe utanielewa na macho yako ya ajabuajabu lakini angalau hunisingizii mimi, eti macho yako hayana ushirikiano kwa sababu mimi nilipanga hivyo. Na hujidai mbele yangu kama wengine ambao kila siku wanaona ninawapendelea ha ha ha.

Ndiyo maana ninakwambia Makengeza, nimechoka! Yaani kweli watu wanafikiri kwamba mimi nina muda wa kuangalia kila upumbavu wa binadamu na kuamuru iwe hivi au vile? Kuna hao wamekuwa mafisadi wa kubuhu, wengine wanapiga, na kutesa na hata kuua, au kuamuru kuua, lakini kila Ijumaa au Jumapili wanajileta mbele yangu kwa unyenyekevu wa kifedhuli eti kunishukuru kwamba nimewaletea baraka. Nibariki ufisadi. Nibariki utesaji na uuaji? Wana akili timamu? Au hawaoni hata haya? Kweli ni bahati yao kwamba, kinyume cha wanavyofikiria wao, siingilii katika maisha ya wanadamu, vinginevyo wangekuta radi inawagonga kichwani huku wakinishukuru kwa ‘baraka’ zao. Duh! Kwa wale ambao wanafikiri mwanangu ni Mzungu kwa kuwa njia yao ilishamiri huko uzunguni, hawasomi kitabu changu? Hawajui Wafarisayo walikuwa akina nani? Kutwa kujisifu, kujikweza, kujiona bora huku wakiwanyanyasa watu. Hata wao hawakuonja radi ingawa niliwalaani kila siku.

Na kinyume chake ndiyo mbaya zaidi ndiyo maana nimeamua kuandika barua hii kwa wadhambi kama wewe. Kwa kweli nimevumilia mengi lakini niliposikia kwamba Wabongo wananisingizia hata kifo cha mtoto baada ya kutwangwa kikatili, nilikata tamaa kabisa. Eti ‘ni bahati mbaya’. Kuchukua gogo na kuendelea kumtwanga mtoto huku damu inatoka, ni bahati mbaya? Eti ni ‘mpango wa Mungu’. Mpango wangu? Mimi ninapanga mtoto asingiziwe kisha atwangwe kama gunia la mahindi?’ Kufuru kufuru kufuru.

Lakini nawaelewa. Mimi ni kimbilio la wakosefu. Wafanye makosa wao, kisha wanisingizie mimi. Tuchukue huu mfano. Kwani sioni kwamba Wizara yenu ya mashule inatengeneza kanuni kisha inanunia kanuni zake. Lini wamehakikisha kwamba kanuni hizi zinafuatwa? Lini wakaguzi na maafisa elimu, na walimu wakuu wamekumbuka kwamba kanuni hutengenezwa ili kuhakikisha ule ubaya wa kibinadamu haujitokezi? Lini wamefuatilia?

Tena nakwambia Makengeza, niko tayari kufanya kama nilivyofanya kwa Lutu katika Biblia. Alinibembeleza, je nikipata watu wachache wenye maadili nitaacha kuangamiza mji wake. Nikakubali. Akapunguza idadi, nikakubali, akapunguza tena, nikakubali lakini wapi. Hawakuwepo. Na sasa nasema, kwako, tafuta shule ambazo zimefuata kanuni za adhabu, nitabaki nanyi. Punguza idadi za shule, nitakubali, punguza tena, nitakubali lakini vinginevyo ninaachana na Bongo kabisa. Fleva yenu imechina moja kwa moja.

Lakini wakati unatafuta hizi shule, hebu nikuulize swali moja ya mwisho. Labda, labda mara mojamoja naingilia kati. Unaonaje? Mwaka jana niliingilia kati? Ha ha ha ha ha. Kweli mwenzenu aliokoka mbele ya uovu uliokithiri. Risasi zote hizi. Lakini unafikiri kwamba waovu walijifunza? Ndiyo maana nakuambia nimechoka. Hata kuvaa fulana inayowaambia watu waombe kwangu ni kosa la jinai? Halafu mnajidai ni taifa la Mungu. Msinichekeshe jamani.

Ndiyo maana nakupa siku moja tu Makengeza. Usipopata shule zile zinazofuata kanuni badala ya kunisingizia mimi eti napanga matokeo ya ukatili wao, naondoka. Nawaachia nchi yenu.

Mungu.

Tulipomaliza kusoma, mimi ni mke wangu tukabaki tumeduwaa. Sasa tufanye nini? Tupate wapi hizi shule? Kweli Wizara imetoa tamko lingine tena lakini tutakuta tofauti yoyote? Tutaweza kupata hizi shule mia, au hamsini au ishirini ambazo zinafuata kanuni za nani apige viboko, viboko vipigwe vingapi, wakati gani na kwa watoto wa umri gani? Na tusipopata, itakuwaje?

Na je, tutangaze barua hii? Wenye nia mbaya wataipokeaje? Au hata wenye nia njema maana wanaona kwamba wao wanamjua Mungu kuliko anavyojijua mwenyewe. Watasikia na kutafakari. Iwapo hata kuvaa fulana ni kosa la jinai, barua ya Mwenyezi mwenyewe itakuwaje. Tukaanza kutetemeka tean.

Advertisement