Muswada Sheria ya vyama vya siasa umekwaza wengi kwa mengi – (2)

Wednesday February 13 2019

 

By Deus Kibamba, Mwananchi

Katika makala iliyotangulia Jumapili nilianza kuandika maoni yangu juu ya mchakato uliopelekea kupitishwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992.

Nilisema kuwa mchakato ulikuwa na mapungufu hadi kupelekea zao la mchakato kuwa na maudhui yaliyosononesha na kukwaza wengi kwa mengi. Nilitaja mambo manne yenye kasoro kwa jinsi mchakato ulivyokwenda. Ukiacha mambo hayo manne, kuna mengine mawili ya kimchakato ambayo natamani kama taifa tungekuwa tulifanya vema zaidi tofauti na ilivyotokea.

Kwanza, natamani muswada huu ungekuwa uliletwa kama Muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2019. Wadau wa masuala ya Siasa na Demokrasia walikuwa wameshauri na kukubaliana kuwa kwa kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa inakaribia miaka 30 tangu kutungwa kwake kwa mara ya kwanza mwaka 1992; na kwa kuwa tayari imekwishafanyiwa marekebisho mara kadhaa miaka iliyopita, ingekuwa jambo jema kuleta Muswada mpya wa Sheria ambao ukipita utabatilisha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na marekebisho yake yote ya miaka iliyopita.

Kwa kutambua hili, kuliandaliwa Muswada na Jedwali ambao mwaka 2017 ulisambaa mitandaoni ukiwa na vifungu 71, huku kifungu cha 71 kikibatilisha Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka Na. 5 ya Mwaka 1992.

Hii ni muhimu sana katika kuzifanya sheria za Tanzania kuwa rafiki kwa wasomaji badala ya kuwa na sheria yenye marekebisho mara tano au sita kiasi cha kuwapoteza hata wanasheria na mawakili kwa kuwa ili kuisoma sheria ni lazima kupata sheria yenyewe, pamoja na marekebisho yake yote.

Vilevile, kuna jambo jingine limesikitisha kimchakato. Tangu muswada umesomwa kwa mara ya kwanza na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali mnamo tarehe 16 Oktoba 2018, kulikuwepo muda mfupi sana hadi muswada ulipokuja kusomwa mara ya pili na kupitishwa na Bunge Januari 2019.

Hivi tuna haraka ya nini? Kwa nini hatukuruhusu wadau wauchambue kwa kina, waandae mikutano ya kuujadili na kukaribisha maoni na mapendekezo kutoka kwa Watanzania kwa upana wake? Hivi miezi miwili au mitatu inatosha kuratibu utoaji wa maoni kuhusu muswada wa sheria muhimu kama ya vyama vya Siasa?

Na kwa nini msajili alifanya jaribio la kushirikisha vyama vya Siasa tu kana kwamba ndio wadau pekee wa muswada huu? Ile elimu ya uraia inayozungumzwa katika muswada itatolewa kwa vyama na nani?

Vipi kuhusu vyama na asasi za kiraia ambazo ndizo hujitokeza mara kwa mara kuandaa shughuli za kuelimisha na kujadiliana na vyama vya siasa pamoja na umma kwa mapana yake?

Vipi kuhusu wadau wengine kama vyama rafiki na washirika wa vyama vilivyoko nchini kokote waliko duniani? Tumetoa muda wa kutosha kuruhusu tafakari ya kutosha miongoni mwa makundi yote hayo? Kwani wadau wa demokrasia ya vyama vingi ni vyama vyenyewe pekee?

Kuhusu maudhui yaliyokosekana, kuna maeneo mengi lakini nijikite katika masuala matatu tu kwa sasa.

Kwanza, ni kukosekana kwa lengo na vifungu vya kukomesha siasa zinazoendeleza mfumo dume na ukatili wa kijinsia nchini. Watanzania watakubaliana nami kuwa vyama vya siasa nchini viko katika orodha ya taasisi zinazoongozwa kibabe kama ilivyo kwa sekta nyinginezo katika nchi yetu.

Kutamalaki kwa mfumo dume nchini kumemaanisha na kupelekea wanaume kushika nafasi zote muhimu katika uongozi wa vyama vya siasa. Matokeo yake ni kuwa katika vyama 18 vilivyopo sasa kwenye daftari la vyama nchini, zaidi ya asilimia 90 vinaongozwa na wanaume katika nafasi zake zote za juu kitaifa.

Kwa mfano, kuna wenyeviti wangapi wa vyama vya siasa Tanzania ambao ni wanawake? Kuna makamu wangapi? makatibu wakuu je? wahazini? Ni jambo la kusikitisha sana.

Vivyo hivyo, mfumo dume umewanyima vijana fursa ya kuongoza vyama vya siasa Tanzania. Kwa mfano, vijana kwa ujumla wako pembezoni mwa uongozi wa vyama huku wazee walewale walioanzisha vyama mwaka 1992 wakiendelea kuwa katika nafasi za juu za uongozi.

Hivi tumefika mahali tunamwachia Mungu mwenyewe kuamua nani ataondoka katika uongozi wa chama cha siasa?

Mbaya zaidi, hata katika baraza au umoja wa wanawake katika chama, maamuzi juu ya nani atapata au kuendelea kushikilia nafasi ya uongozi yanategemea kukubalika kwa mwanamke huyo miongoni mwa jopo la wazee wanaume.

Je haikuwa fursa muhimu kupiga marufuku vyama kupanga safu nzima ya uongozi kwa kutumia wanaume pekee? Ikiwa kuna masharti kuwa itakuwa marufuku kwa chama kuwa na wanachama na viongozi wa kitaifa kutoka upande mmoja wa Muungano pekee, kwa nini isiwepo kuhusu uwiano kijinsia na makundi mengine kama watu wenye ulemavu?Tujitafakari na tujisahihishe!

Deus Kibamba ni mtafiti, mchambuzi na mhadhiri katika masuala ya siasa, uchumi na uhusiano wa Kimataifa. Ameshiriki mazungumzo ya hali ya baadaye ya Sudani. Simu: 0788 758581 ; email: [email protected]

Advertisement