Mwaka 2012 ulikuwa mwaka wa tabu Yanga

Monday October 1 2018

Haruna Niyonzima wa Simba akimpigia hesabu

Haruna Niyonzima wa Simba akimpigia hesabu Andrew Vicent 'Dante'wa Yanga. 

By Oliver Albert, Mwananchi

Achana na matokeo ya jana ya watani wa jadi lakini mwaka 2012 bado utabaki katika kumbukumbu za muda mrefu kuwa ulikuwa mwaka wa tabu kwa Yanga katika miaka 10 iliyopita ya mechi za timu hizo.

Katika kipindi hicho cha miaka 10 ukiondoa mchezo wa jana, Yanga na Simba kila mmoja zimecheza mara 21 lakini kila mmoja amemfunga mwenzake mara tisa.

Mwaka huo wa 2012, Yanga ililala kwa kipigo kikubwa cha mabao 5-0, kiasi cha kuwasononesha viongozi na mashabiki wa klabu hiyo ambao hadi sasa wanaumizwa na matokeo hayo japo ni miaka sita sasa.

Bado mashabiki wanaumizwa na matokeo hayo na wanataka kikosi chao siku yoyote kilipe kisasi ili angalau wapate kupumzika na maneno kutoka kwa wapinzani wao Simba.

Mwaka uliofuata iliaminika kuwa Yanga ingelipiza kisasi kwani hadi mapumziko matokeo ya 3-0. Mashabiki wa Simba walikuwa kimya wakijua tano zinarudi. Hata hivyo, hadi dakika 90 matokeo yalikuwa 3-3.

Mei 6, 2012 ndio pambano hilo lilifanyika na Yanga kuchapwa mabao 5-0 yaliyofungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 6 na 62, Felix Sunzu (dakika ya 56) Juma Kaseja (penalti dakika ya 67 na marehemu Patrick Mutesa Mafisango aliyefunga dakika ya 72 pia kwa mkwaju wa penalti.

Hata hivyo, kipigo hicho inasemekana kuna kitu nyuma ya pazia baada ya kudaiwa kuwa wachezaji waligoma kabla ya mchezo wakishinikiza kulipwa kwa malimbikizo yao ya mshahara.

Matokeo mengine ya Simba na Yanga ndani ya miaka 10 ni kama ifuatavyo:-

April 27, 2008

Timu hizo zilitoka suluhu katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa jijini Dar es Salaam.

Oktoba 26, 2008

Yanga iliyokuwa na wachezaji nyota kama Boniface Ambani, Benny Mwalala na Mrisho Ngassa iliichapa Simba bao 1-0 lililofungwa na Mwalala dakika ya 15.

April 19, 2009

Timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, mabao ya Yanga yakifungwa na Ben Mwalala dakika ya 48 na Jerry Tegete dakika ya 90 wakati ya Simba yalifungwa na Ramadhan Chombo’Redondo’ dakika ya 23 na Haruna Moshi’Bobani’ dakika ya 62.

Oktoba 31, 2009

Mussa Hassan ‘Mgosi’alifunga bao pekee dakika ya 26 lililoipa Simba ushindi wa bao 1-0.

April 18, 2010

Katika mchezo wa Simba na Yanga uliozalisha mabao mengi,Simba ikishinda mabao 4-3. Mabao ya washindi yalifungwa na Mussa Hassan’Mgosi’ dakika ya 53 na 74,Uhuru Seleman dakika ya 3 na Hillary Echesa dakika ya 90 wakati ya Yanga yalifungwa na Athuman Idd’Chuji’ dakika ya 30 na Jerrson Tegete aliyefunga dakika ya 69 na 89.

Oktoba16,2010:

Pambano la watani wa jadi lilichezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba. Bao la Yanga lilifungwa na Jerry Tegete dakika ya 70.

Machi 5, 2011

Timu hizo zilitoka sare ya kufungana bao 1-1. Bao la Yanga lilifungwa na Stephano Mwasika kwa penati dakika ya 59 na Simba ikasawazisha kupitia kwa Mussa Hassan ‘Mgosi’ dakika ya 73.

Oktoba 29, 2011

Yanga iliichapa Simba bao 1-0 lililofungwa Mzambia, Davies Mwape dakika ya 75.

Mei 6, 2012

Simba ikiwa chini ya Kocha Mserbia, Milovan Cirkovic ilipata ushindi mnono dhidi ya Yanga kwa kushinda mabao 5-0. Mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 1 na 65, Felix Sunzu dakika ya 74,Patrick Mafisango dakika ya 58 na kipa Juma Kaseja dakika ya 69.

Oktoba 3, 2012

Katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Simba ilitangulia kufunga kupitia Amri Kiemba dakika ya tatu na Yanga ikasawazisha dakika ya 65 kupitia kwa Said Bahanuzi.

Mei 18,2013

Yanga iliichapa Simba mabao 2-0, mabao ya washindi yalifungwa na Mrundi Didier Kavumbagu dakika ya tano na Mganda Hamis Kiiza dakika ya 62.

Oktoba 20, 2013

Katika mchezo huu Simba ilitoka nyuma kwa mabao 3-0 na kusawazisha yote na kuifanya mechi hiyo kumalizika kwa mabao 3-3.

Hadi mapumziko Yanga iliongoza kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 15 na mawili ya Hamis Kiiza dakika ya 36 na 45 kabla ya Simba kusawazisha kupitia kwa Betram Mombeki dakika ya 54,Mganda Joseph Owino dakika ya 58 na Mrundi Gilbert Kaze dakika ya 85.

April 19, 2014

Simba na Yanga zilitoka sare ya bao 1-1.Bao la Simba lilifungwa dakika ya 76 na Haruna Chanongo wakati la Yanga lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 86.

Oktoba 18,2014

Timu hizo zilitoka suluhu

Machi 8, 2015

Simba iliitandika Yanga bao 1-0 lililofungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 52.

Septemba 26,2015

Mabao ya Amissi Tambwe dakika ya 44 na Malimi Busungu dakika ya 79 yalitosha kuipa ushindi Yanga wa mabao 2-0.

Februari 20, 2016

Yanga iliendeleza ubabe kwa Simba kwa kuifunga mabao 2-0,Donald Ngoma akifunga dakika ya 39 na Amiss Tambwe akifunga dakika ya 72.

Oktoba 1, 2016

Mchezo huu uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 utakumbukwa baada ya mashabiki wa Simba kung’oa viti wakidai mwamuzi Martin Saanya amekubali bao la mkono lililofungwa na Amissi Tambwe dakika ya 26.

Hata hivyo furaha ya Simba ilirejea baada ya Shiza Kichuya kusawazisha bao dakika ya 87 akifunga kona iliyokwenda moja kwa moja wavuni.

Februari 25, 2017

Simba ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa na Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 66 na Shiza Kichuya dakika ya 81 wakati bao la kufutia machozi la Yanga lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Simon Msuva dakika ya tano.

Oktoba 28,2017

Timu hizi zilitoka sare ya bao 1-1 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru.Simba walianza kufunga kupitia kwa Shiza Kichuya dakika ya 57 kabla ya Mzambia Obrey Chirwa kusawazisha dakika ya 60.

April 29,2018

Simba iliichapa Yanga bao 1-0 lililofungwa na Erasto Nyoni dakika ya 37.

Advertisement