TUONGEE KIUME: Mwaka 2018 umemtia adabu kila mtu

Ukitembea mjini, tazama sana nguzo za umeme. Utaona matangazo madogomadogo yalitengenezwa kwa plastiki yananing’inia, yanasomeka.

‘TANGAZO! Mganga kutoka Nigeria. Anatibu Nguvu za kiume, pete ya bahati, kumrudisha mpenzi, mvuto, kazi, biashara, kufaulu masomo, uzazi, kumfunga mke/mume, kusafisha nyota, biashara, cheo kazini, kuongeza shepu. Kujiunga na Freemason, kuolewa. Pia tunatibu kwa njia ya simu. Namba ni hizo hizo hizo.

Ila kama kuna huduma hawa waganga kutoka Nigeria na Sumbawanga wanatakiwa kuongeza kwa kipindi hiki, ni dawa ya kuufupisha mwezi Januari.

Kwa sababu ingekuwa miezi mingine, leo isingekuwa tarehe 6, tungekuwa tuko tarehe 12 au 14. Huu mwezi una matatizo, kuna kitu kinatakiwa kifanyike.

Ila leo tuuongelee mwaka 2018. Bado hatujausahau.

Kama ni wa kisasa! Unakwenda na wakati, unatumia mitandao ya kijamii, utakuwa unafahamu ugonjwa wa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuweka maisha yao binafsi huko.

Mchana anakula nini, anapiga picha, anaweka (Lakini ikiwa tu anakula chakula ambacho sio cha kawaida.). Muda huu yuko wapi, anapiga picha anaweka! Kagombana na mwenzie, tutajua tu kwa maneno yake atakayokuwa anaandika , kimsingi ni ugonjwa wa wanawake sanasana, wanaume wa ukweli wachache sana wenye hayo mambo.

Sasa kama ulikuwa kwenye mitandao tangu mwaka 2017, utakumbuka ilivyokuwa Januari ya mwaka 2018. Watu walikuwa wanakuja kwenye mitandao ya kijamii na kuandika maneno ya mzuka kuhusu malengo yao na mwaka mpya utakavyokuwa.

Mtu anaandika ‘New Year, New Me’ yaani ‘Mwaka mpya, na mimi mpya’ halafu hapo mbele anatuandikia na malengo marefu kama reli ya SGR ambayo ndiyo amejiwekea kwa mwaka 2018.

Ila kwa sababu na sisi tuna mambo yetu ya msingi, hatujawahi kufuatilia kujua kama kweli walivyoviandika vilifanikiwa au laa.

Sasa hiyo ndiyo huwa tabia ya watu miaka yote. Kila mwaka ukiisha watu wanaonyesha mzuka wa mafanikio ya mwaka mpya. Lakini otea sasa; mwaka huu 2019, hayo mambo yamepungua kabisa kabisa kabisa.

Mwaka 2018 umenyoosha watu, umetutia mafunzo na kutuadabisha kisawasawa. Umetuonyesha namna ya kuishi bila makelele. Umetukomesha tabia ya kufanya maisha yetu kama wanasiasa, kutangaza karibu kila kitu tunachokifanya ili kutafuta ‘attention’. Huwezi kuamini huko mitandaoni kumepoa kama sio kuwa kimya kabisa kana kwamba mwaka jana, 2018 ndiyo ilikuwa mwisho wa maisha yetu.

Hakuna mtu anayetuambia malengo yake tena; nina uhakika sio kwamba watu hawana mipango na mwaka huu wa 2019, hapana. Ila walichowafinyiwa na mwaka 2018 wameacha mwaka huu kwanza uongozwe na neema za Mungu tu na si vinginevyo. Kama matangazo tutafanya mipango yetu ikikamilika.

Heri ya mwaka mpya.