TUONGEE KIUME: Mwanaume kutunza watoto wa kimada nalo ni tatizo

Sunday November 18 2018

 

Labda haikuwa tabia yako ya ndani ulivyokuwa mtoto, lakini kwa sababu uliwahi kuwa mdogo kuna uwezekano mkubwa kwamba kuna kipindi ulijikuta una hamasa sana kufanya majukumu ya familia za watu kuliko familia yako.

Mfano nyumbani kwenu wanakutuma kwenda sehemu, mathalani gengeni, lakini unakataa. Kisha unazunguka mitaa miwili mitatu, unatokea nyumba ya jirani— huko mama mmoja anakutuma cha kufanana na ulichokataa nyumbani — unakubali haraka haraka utadhani mchuzi utakaokuja kuungwa kwa ndimu ulizotumwa na wewe unakuhusu.

Tabia hiyo ya kujitoa kwenye visivyokuhusu, wengine tulipokuwa tuliachana nazo lakini kuna wenzetu bado wanaendelea nazo.

Mtu ana familia yake, mke na watoto wawili watatu. Wanawe wanasoma kwenye shule alizotuahidi Magufuli kabla hajawa Rais; za elimu bure, hilo sio tatizo.

Wanapolala watoto haparidhishi sana, kuna kitanda kidogodogo na godoro lililonunuliwa miaka kama 10 hivi iliyopita, limekuwa jembamba, limelegea kama ulimi wa mbwa — pia sio shida sana kwa sababu watoto wenyewe kila siku wanaamka na furaha.

Wakiugua, wanatibiwa kwenye hospitali za kawaida. Pia sio tatizo sana, ndiyo maisha yetu. Kwenye msosi nako ndio vile vile. Watoto hata wakila wali na maharage mwezi mzima ‘hawanaga’ shida.

Nguo ndiyo majanga matupu, zina matundu kama chandarua. Ila ni sawa tu kwa sababu watoto wenyewe hata hawajali, kwanza wakiwa kwenye michezo hata mashati hawataki kuvaa. Maisha yanakwenda.

Lakini sasa baba wa watoto hawa hawa, kakamatwa na mwanamke huko nje. Mwanamke ambaye unakuta kwa bahati nzuri kama sio mbaya naye ana mtoto wake mmoja — kimombo wanaitwa ‘Singo Maza’.

Mwanamke anajua Baba ana mke na familia huko lakini yeye hajali. Kinachotokea. Baba huyu huyu mwenye watoto wanaolala watatu kwenye kitanda kimoja cha futi tatu kwa tatu, anamuhudumia huyu mtoto wa mchepuko kama ndiyo mwanae wa kumzaa — mtoto wa kimada anaishi kifalme.

Anasomeshwa shule za Santi nani kwa pesa za baba huyu huyu ambae wanae wanasoma shule ya msingi Darajani Tandale kwa Mtogole.

Mtoto wa kimada anavaa nguo za bei mbaya, nguo za maduka ya vioo anazonunuliwa na baba huyu huyu mwenye watoto wanaovaa nguo zimechanika kama wako Sudan Kusini.

Mtoto Jumapili anatolewa ‘out’ mabaharini huko akachezee maji kama samaki. Na ni kwa pesa za baba huyu ambaye wanawe kuogelea ni hadi mvua zinyeshe, dimbwi la nyuma ya nyumba ya mzee Matola lijae, wajirushe humo kwenye maji yaliyochanganyika na maji taka yaliyotapishwa kwenye vyoo.

Hatusemi tusisaidie watoto wengine huko nje. Ila habari za kuchipulisha mbegu za wenzako wakati zako zinaharibika kama haijakaa sawa sawa hivi. Tujichunguze wazee wenzangu.

Advertisement