Mwenyekiti Chama cha Soka Kinondoni afariki dunia

Muktasari:

  • Mbali ya kuwa mwenyekiti wa Kifa, pia marehemu Lupiana alikuwa mjumbe wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Kinondoni (KIFA), Michael Simon Lupiana (72) maarufu kwa jina la Mzee Lupiana amefariki dunia baada ya kugua muda mfupi.

Mbali ya kuwa mwenyekiti wa Kifa, pia marehemu Lupiana alikuwa mjumbe wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kwenye mkutano mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mtoto wa marehemu, Lupiana Lupiana alisema kuwa baba yake alilazwa Hospitali yaTaifa ya Muhimbili Ijumaa Kuu akisumbuliwa na shinikizo la damu (pressure) na kisukari maradhi yalisababisha matatizo ya figo na kufariki dunia saa 5.30 usiku wa Sikukuu ya Pasaka.

Lupiana alisema kuwa msiba kwa sasa upo nyumbani kwao, Kimara Stop Over na wanatarajia kuzika keshokutwa Jumatano kwenye makaburi ya Kinondoni.

“Kwa sasa tupo katika harakati za kukamilisha masuala mbalimbali ya msiba wa mpendwa baba yetu na matarajio ni kumpunzisha katika nyumba yake ya milele siku ya Jumatano kwenye  makaburi ya Kinondoni, taratibu nyingine zitatolewa baadaye,” alisema Lupiana.

Hiki kilikuwa kipindi cha pili cha uongozi cha marehemu Mzee Lupiana ambapo mwakani alikuwa anamalizia muda wake.

Mbali ya kuwa kiongozi wa mpira, marehemu pia alikuwa mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wa wadogowadogo madini ya kujengea (DACOREMA) na aliwahi kuwa diwani wa Kata ya Kinondoni.