SIMULIZI ZA MUZIKI: Mzee Majengo na Shikamoo Jazz Band Wana Chelachela

Saturday April 13 2019

 

By Anko Kitime

Leo nimemkumbuka rafiki yangu, mzee wangu na mwanamuziki mwenzangu marehemu Bakari Majengo. Mwishoni mwa maisha yake Mzee Majengo alikuwa mwanamuziki wa Shikamoo Jazz Band ‘Wana Chelachela’. Bendi hii ilianzishwa na Shirika la Kusaidia Wazee la Helpage kwa kununua vyombo vya muziki na kulilea kundi hili kwa miaka yake ya mwanzoni mara baada ya kuanzishwa mwaka 1993.

Bendi iliwakusanya wanamuziki nguli na wazee kutoka bendi mbalimbali nchini.

Nguli hao ni Salum Zahor, marehemu Kepten John Simon, Ally Adinani, Athuman Manicho, marehemu Ally Rashid, marehemu Kassim Mapili na wengine ni Mohammed Tungwa, Kassim Mponda, Mariam Nylon na Bakari Majengo ambao wote ni marehemu.

Mzee Majengo ambaye alikuwa mpulizaji wa Saxophone alizaliwa mwaka 1943, Kariakoo, jijini Dar es Salaam na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Mchikichini kwa miaka miwili ya 1949 na 50.

Mwaka 1955 ilipoanzishwa Shule ya Magomeni Mzimuni, alilazimika kuanza tena darasa la kwanza hadi la nane na kumaliza mwaka 1962. Majengo alianza rasmi shughuli za muziki alipojiunga na Dar es Salaam Jazz akiwa mkung’utaji wa tumba.

Kabla ya hapo alikuwa akipiga ngoma kwenye vibendi vya watoto na kutumbuiza katika sherehe mbalimbali.

Advertisement

Baadhi ya wanamuziki waliompokea Dar es Salaam Jazz Band, ni pamoja na Edward Salvu na Grey Sindo waliokuwa mahiri kwa upulizaji Sax, ambao kwa nyakati tofauti walichangia kumfundisha chombo hicho. Mwaka 1963, marehemu Michael Enock, aliyekuja kujulikana kwa jina la King Enock alijiunga na Dar es salaam Jazz Band na huyu pia alikuja kumuongezea ujuzi wa kupuliza Sax kwa kiwango kikubwa.

Mwaka 1968 Mzee Majengo aliondoka Dar es salaam Jazz Band akiwa ameshashiriki kupiga Sax kwenye vibao vingi, kikiwamo kile maarufu, ‘Mtoto Acha Kupiga Mayowe’, akajiunga na bendi iliyokuwa na wanamuziki Wakongo watupu iliyoitwa King Afrika, mwaka 1969 alihamia bendi nyingine ambayo nayo pia ilikuwa ya wanamuziki Wakongo tu , iliyoitwa 60 Zaire, na mwaka 1970 akajiunga na bendi ya Nova Success iliyokuwa ikiongozwa na Papaa Micky.

Humo alipiga nyimbo nyingi, na saksafoni katika nyimbo kama Bolingo Chlorida ni kazi ya marehemu Bakari Majengo. Mwaka 1974 Nova Success, ilipata safari ya kwenda nchi za Kusini mwa Afrika, Mzee Majengo akashindwa kusafiri na bendi hiyo kwani alikuwa ameajiriwa katika kiwanda cha viatu cha BATA Shoes, jijini Dar es Salaam. Ajira aliyokuwa nayo tangu mwaka 1963.

Mwaka 1975 alijiunga na Orchestra Maquis du Zaire ‘Wana Kamanyola’ wakati huo ikiwa chini ya mpulizaji Sax hodari, Chinyama Chiaza. Katika bendi hii pia alishiri kurekodi nyimbo nyingi zilizokuja kupendwa sana, katika uhai wake mwenyewe alikuwa akijisifu kwa kazi aliyoifanya katika wimbo ‘Nimepigwa Ngwala’.

Akiwa Maquis, mwaka 1986 alilazimika kusimama kwa muda kupiga Sax kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifua lakini alipopata nafuu, alikwenda kujiunga na mwanamuziki Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kikii’ aliyekuwa kaanzisha bendi yake ya Orchestra Double O.

Chinyama alipobaini hilo, alimfuata na kumuomba arudi Maquis, ambapo siku aliyorejea kazini alikuta bendi iko chini ya Tshimanga Kalala Assosa ambaye wakati huo walikuwa hawajuani.

“Nilisalimiana naye kikawaida lakini nilipotaka kupanda jukwaani alinizuia baada ya majibizano nilisusa na kusimama bendi,” aliwahi hadithia Mzee Majengo.

Majengo anasema kuwa, alipokuwa kasimama kuitumikia Maquis, siku moja alitembelea onyesho la Orchestra Safari Sound wakati wa awamu ya ‘Power Iranda’ na mmiliki wa bendi hiyo Huggo Kisima, alipomuona akamvuta kwake, na Septemba 1986 alianza kazi rasmi na wanamuziki Muhidin Gurumo, Skassy Kasambulla na Abdallah Kimeza ndani ya OSS na kushiriki kurekodi nao vibao vingi.

Mwaka 1990 alirudi tena Marquis na kudumu katika bendi hiyo hadi mwaka 1993 alipoachia ngazi rasmi na kuwa mmoja wa waanzilishi wa Shikamoo Jazz.

Tofauti na wanamuziki wengi wanaotupa lawama kwa vyombo vya habari kuhusi kudidimia kwa dansi, Majengo aliamini kuwa ubinafsi wa wanamuziki wenyewe ndio chanzo kikuu cha kudidimia kwa muziki wa dansi.

Majengo aliona kuwa kila mmoja kwenye muziki wa dansi anajijali yeye mwenyewe au bendi yake tu, hivyo kukosa ushirikiano katika mambo yanayowahusu wote, na kubakiza ushirikiano wa mdomoni tu.

Labda kutokana na kadhia alizozipata katika maisha yake ya muziki, Mzee Majengo alifurahia kukosa mrithi wa kazi yake ya muziki japo alikuwa na watoto watano. Bakari Majengo alifariki dunia Septemba 16, 2017.

Advertisement