Najivunia miaka tisa ya Mimi na Tanzania

Sunday March 18 2018

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi

Mwaka 2011 Hoyce Temu alianzisha kipindi cha ‘Mimi na Tanzania’ kinachorushwa na Channel 10 akiwa na lengo la kuyaibua matatizo ya watu wenye uhitaji ili waweze kupata msaada.

Siyo kwa maana ya kuwapa fedha, wapo wanaohitaji faraja na vivyo ndivyo amekuwa akifanya kwa miaka saba.

“Kupitia kipindi hicho mpaka hivi sasa tumeweza kusaidia zaidi ya watu 1,000 na bado tutaendela kuwafikia watu katika mikoa yote nchini,” anasema Hoyce.

Anasema Watanzania wameweza kumuamini na kukubaliana na kazi ya kusaidia jamii anayoifanya jambo ambalo limeweka urahisi kwao kumtumia fedha kwa ajili ya kuwafikishia wahitaji.

“Ni jambo ambalo sikuwahi kulifikiria nimewahi kukusanya hadi Sh1 bilioni kutoka kwa Watanzania ili tuweze kuwasaidia watu wenye mahitaji katika matibabu na matatizo mengine,kwa sababu nisingeweza kufanya hayo yote peke yangu sina mshahara mkubwa wa kuweza kuwasaidia watu wote,” anasema Hoyce.

Anasema kutokana na maisha aliyoyaishi awali anatamani ufike wakati wanawake wote wanaoishi vijijini wawe na sauti katika kujadili mambo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.

“Ifike mahali kila mwanamke awe na ujuzi, ari ya kujaribu kufanya kitu chochote kinachoweza kuleta mafanikio na hata kusaidiana, kuongozana na kuelimishana katika vitu tofauti,” anasema Hoyce.

Kuhusu mitandao ya kijamii

Katika kutafuta maendeleo vijana wanapaswa kutumia mitandao ya kijamii katika kuwaletea maendeleo na sio katika kushabikia mambo yanayowapotezea muda wa kufanya kazi.

“Huwezi kukwepa kupita katika mitandao ya kijamii lakini jaribu kuangalia kitu gani ukikisoma na kukifuatilia kitaongeza tija kwako, kitakufundisha na kukuletea matokeo chanya,” anasema.

Kuhusu Miss Tanzania

Anasema aliamini ushiriki wake katika mashindano ya Miss Tanzania mwaka 1999 ndiyo ingekuwa njia pekee itakayompatia urahisi wa kukutana na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi jambo ambalo lingemfikisha kule anakotakata kufika.

“Kwa wakati huo Miss Tanzania ilikuwa na watazamaji wengi hivyo nikaamua kuitumia fursa ipasavyo ili niweze kusaidia kina mama wa kijijini na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na nilifanikiwa,” anasema Hoyce aliyeibuka mshindi.

Baada ya kutwaa taji hilo mawazo aliyokuwa nayo kichwani yalianza kuwa kweli na alipata fursa ya kufanya kazi na mashirika tofauti ndani na nje ya nchi.

“Nimefanya kazi nyingi za kijamii baada ya kutwaa taji la Miss Tanzania ikiwemo kuwaelimisha kinamama juu ya umuhimu wa Vicoba, kutoa misaada mbalimbali kwa jamii jambo ambalo naendelea nalo mpaka leo na sitakuja kuiacha maishani mwangu,” anasema Hoyce.

Anasema misaada ambayo amekuwa akiipeleka kwa watu wenye uhitaji imekuwa ikitoka kwa Watanzania na wakati mwingine amekuwa akifanya mambo makubwa ambayo yako nje ya uwezo wake.

Advertisement