Nditi, Mtanzania aliyeshindwa kutimiza ndoto Chelsea, Ulaya

Mbali na kipaji cha kusakata soka, lakini juhudi, uvumilivu na kujituma ni miongoni mwa vitu vinavyoweza kumbeba mchezaji kupata mafanikio.

Bila shaka unakumbuka jina la beki wa kushoto wa zamani wa timu ya vijana ya Chelsea, Adam Nditi mwenye asili ya Tanzania. Hakuna aliyefikiri anaweza kupotea kwenye ramani ya soka.

Nditi alizaliwa kwenye familia ya mpira kutokana na baba yake mzee Erick Nditi kucheza soka kipindi chake cha ujana akiwa na klabu ya Kikwajuni na timu ya Taifa ya Zanzibar. Mzee huyo aliondoka Tanzania mwaka 1995, inatajwa alizamia Uingereza baada ya kukutana na mrembo wa Kiingereza Marina ambaye ana asili ya Italia na Uingereza. Alifikia katika Kitongoji cha Basingstoke.

Wakati huo tayari alikuwa ameacha mtoto Zanzibar ambaye ni Adam aliyezaa na mwanamke mmoja wa Tanzania mwaka 1994 wakati akikaribia kuacha soka katika klabu ya Kikwajuni.

Nditi alimfuata baba yake Uingereza na baada ya kuwasili nchini humo alijihusisha na soka na baadaye alipata nafasi ya kujiunga na akademi ya Chelsea.

Kinda huyo alijiunga na akademi hiyo mwaka 2016 akicheza timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 ambako alikutana na akina Charly Musonda Jr, Andreas Christensen na Reuben Loftus-Cheek.

Umri ulivyosogea alipandishwa hadi kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 21 cha Chelsea ambacho kinashiriki ligi kwa vijana wenye umri huo.

Akiwa na kikosi cha Chelsea alipata nafasi ya kucheza mara kwa mara na moja ya mchezo ambao alicheza ni ule wa nusu fainali ya Kombe la FA, Aprili 10, 2011 kati ya timu yake iliyokuwa ikichuana na Manchester United.

Man United kilikuwa na Paul Pogba ambaye kwa sasa ni tegemeo la kikosi hicho. Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa amewahi kutamba na Juventus kabla ya kurejea Old Trafford. Maisha yaliendelea kwa Nditi na mwishowe akaingia katika kikosi cha kwanza cha Chelsea akipewa jezi namba 47, lakini kwa bahati mbaya ndiyo ukawa mwanzo wa kupotea.

Kinda huyo alijikuta akitemwa baada ya kutoonyesha kiwango bora kwenye mazoezi ya kikosi hicho cha matajiri wa London na alipoondoka Chelsea alikaa muda mrefu bila ya kupata timu ndipo alipoibukia Fleetwood, iliyokuwa daraja la pili (League One).

Kinda alicheza kwa muda mfupi na baada ya mkataba kumalizika alitemwa na akatimkia mcahngani kujiunga na Farnborough, Julai Mosi 2015 ambako nako alidumu kwa miezi minne tu. Msimu 2016/17, mchezaji huyo alijiunga na Guildford City na baadaye akapotea kabisa kwa kuishia mchangani. Huyu ndiye Adam Nditi ambaye alikuwa anapigiwa chapuo la kuitumikia timu ya Taifa, Taifa Stars.

Nditi aliibua mzozo baina ya wadau wa soka na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), waliokuwa wakiwatuhumu viongozi wa taasisi hiyo kushindwa kumuita kinda huyo katika kikosi cha Taifa Stars.

Salama ya vigogo wa TFF ilikuwa ni kupotea kwa Nditi ambaye alikuwa gumzo baada ya kujiunga na Chelsea.

Nditi ana wadogo zake watatu Roberto (18) na mapacha wawili, Zion na Paolo (13) wanaocheza timu za vijana za klabu ya Reading.

Pengine kama Nditi angekaza msuli angekuwa mmoja wa mastaa wakubwa pale England kama ilivyo kwa Pogba ambaye alicheza naye ligi ya vijana nchini humo. Pogba alikaza buti na hata pale ambapo alikosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza Man United mbele ya kocha mstaafu, Alex Ferguson aliongeza kasi na sasa ni mchezaji staa duniani.

Mfaransa huyo alirejea kama staa na siyo mchezaji wa kawaida kutokana na namna alivyopambana kupigania ndoto yake akiwa Juventus ambako alijifunza vitu vingi kutoka kwa fundi wa Kitaliano Andrea Pirlo.

Kupotea kwa Nditi inaweza kuwa funzo kwa wachezaji wetu wa Tanzania wenye ndoto ya kutaka kucheza soka la kulipwa kujifunza aina ya maisha aliyokuwa akiishi kinda huyo hatua iliyozima ndoto yake ya kuwa mchezaji tegemeo duniani kama akina Pogba au Kylian Mbappe wa PSG.