Ndoa yenye utulivu inaongeza fursa ya kufanikisha biashara

Thursday January 3 2019

 

By Wakili Justine Kaleb

Ni ngumu kutenganisha mafanikio ya kibiashara na uhusiano mzuri ndani ya ndoa.

Japo wapo waliopambana na kufanikiwa wakiwa na uhusiano mbovu lakini ndoa yenye furaha ina nafasi kubwa ya kufanikiwa kwani kuna mstari mwembamba sana kati ya uhusiano mzuri wa ndoa na kufanikiwa katika biashara.

Misingi mizuri ya ndoa inajengwa na, ufahamu na uelewa wa Sheria ya Ndoa kwa sababu uhusiano usio halali kisheria huweza kuyumbisha mambo huko mbeleni.

Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 inatoa muongozo wa kila kitu kuanzia sifa za wenza na wafungishaji, mahali ndoa inaweza kufungwa na namna wanandoa wanavyopaswa kuishi na umiliki mali baina yao.

Ndoa ni mkataba hivyo vigezo vinavyoufanya mkataba uwe halali hutumika kuhakikisha vimezingatiwa.

Kutofikisha umri, uhusiano uliokatazwa kisheria kama kuoana ndugu vinaipa mahakama au baraza la usuluhishi sababu ya kuagiza kutofungwa kwa ndoa husika.

Sababu nyingine ni mmojawapo kutoridhia ndoa, mwenza kutokuwapo wakati wa kufunga ndoa au kufungishwa na mtu ambaye hana mamlaka kisheria.

Kutokuwapo kwa mashahidi wawili au zaidi au kufunga ndoa ya muda mfupi na si ya maisha yote ni sababu nyingine zinazoibatilisha.

Ndoa zinaweza kuwa halali kisheria lakini mahakama au chombo chochote cha sheria zikazibatilisha.

Sababu zinazoweza kubatilisha ndoa ni endapo wakati kufunga mmojawapo hakuwa na uwezo wa kufanya tendo la ndoa au ana matatizo ya akili au hakuwa na akili timamu.

Endapo mwenza ni mgonjwa wa maradhi ya zinaa, mke kuwa na mimba ya mtu mwingine wakati ndoa inafungwa ni sababu nyingine.

Jambo la msingi kwa mfanyabiashara ni kuwa makini kabla hujaanzisha uhusiano wowote wa ndoa kuzingatia kuhusu anayetaka kufunga naye, mazingira ya uhusiano wenyewe na hatua kuihalalisha kisheria na kuwatengenezea mazingira mazuri kibiashara na kisheria.

Ukiwa na ndo tulivu, uhakika wa kufanikisha biashara zako ni mkubwa.

Advertisement