Ndoto ya upinzani kwenda ikulu inavyozaliwa, kufa

Wakati lengo la vyama vya siasa ni kushika dola ndoto ya wapinzani kuingia ikulu imeendelea kuwa ngumu kutokana na nguvu za vyama hivyo kupanda na kushuka tangu mfumo wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1992.
Baadhi ya vyama hivyo, ukiondoa Chadema ambacho sasa kinaongoza upinzani nchini, vimekuwa vikipania kuingia Ikulu na baada ya uchaguzi nguvu zake hupungua siku hadi siku.
Matumaini ya wapinzani kuingia ikulu yaliongozwa na NCCR-Mageuzi iliyomsimamisha Augustine Mrema mwaka 1995 na kupata asilimia 27.77 ya kura, nyuma ya  Benjamin Mkapa wa CCM aliyeshinda kwa asilimia 61.82.
Licha ya ushindani mkali uliokiwezesha chama hicho kupata wabunge 19, nguvu za chama hicho ziliendelea kupungua hadi sasa kikiwa na mbunge mmoja.
Chama kilichofuata kwa kukitikisa chama tawala CCM ni CUF wakati huo kikimsimamisha Profesa Ibrahim Lipumba. Baada ya kuongoza upinzani mwaka 2000 na 2005, baadaye nguvu zake zilizidi kupungua.
Chadema kimekuwa ni chama cha tatu cha upinzani kuwahi kutokea katika historia hiyo ya ushindani ambacho nguvu zake zimekuwa zikiongezeka tangu kilipoanza kusimamisha mgombea urais.
Chama hicho kilipomsimamisha Freeman Mbowe mwaka 2005 kilipata kura zaidi 668,756 (asilimia 5.8), mwaka 2010 kilipomsimamisha Dk Willibrod Slaa kikapanda na kufikia kuwa milioni 2.27 (asilimia 26.34)
Katika uchaguzi wa 2015, Chadema ikiwa na Edward Lowassa ilijisogeza karibu zaidi na ikulu ilipopata kura milioni 6.07 (asilimia 39.97). 
Ukiondoa Chadema, pengine swali la kujiuliza ni kwa nini vyama hivi vimekuwa vikipanda na kuporomoka.
Akijibu swali hilo, Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohammed Bakari anataja nadharia tatu za kuzaliwa na kufa kwa vyama vya upinzani katika nchi zinazotumia mfumo wa vyama vingi vya siasa ikiwamo Tanzania.
INAENDELEA UK 16
Anasema nadharia hizo ni ile inayohusisha sababu zote za ndani na nje (Systemic perspective).
Katika sababu za ndani, anasema uimara wa chama umejengwa kitaasisi au kiongozi mmoja. Pia tunaangalia aina ya viongozi wake, katiba, sera na uwezo wa kushawishi wanachama wapya.
“Nadharia hii imejitokeza ndani ya NCCR- Mageuzi na ikapotea, Chadema pia haikuanza vizuri kitaasisi ila baadaye ikaanza kujiimarisha kwenye mashina,” anasema Profesa Bakari.
Profesa Bakari anasema nadharia ya pili inahusisha sababu za nje ya chama, inayotokana na matatizo ya mfumo wa kitaasisi, kisheria na kikatiba chini ya chama tawala. Nadharia hii imeathiri zaidi upinzani nchini ukilinganisha na jirani kama Kenya na Malawi.
Anasema Tanu ilizaa CCM ambayo siyo chama cha siasa tena ila kimekuwa chama dola.
“Kwa hiyo mfumo uliopo una uwezo wa kudhoofisha chama chochote chenye nguvu. CCM imefanikiwa kudhoofisha CUF licha ya kujengwa kitaasisi,” anasema.
Anasema CUF ilishambuliwa kwa vita ya ‘chama cha udini’ kabla ya kukutana na vita ya ‘chama cha kutetea ndoa za jinsia moja’ huku Chadema ikishambuliwa kwa vita ya siasa za ukanda na ukabila.
Katika nadharia ya tatu, msomi huyo anasema inahusisha mazingira yote ya sababu za ndani na nje. Anasema kwa muktadha wa nadharia hiyo hapa nchini, kuna mazingira yanayonyesha sababu za nje kuwa na nguvu zaidi kuliko sababu za ndani. “Inategemea, kuna mazingira yanaonyesha kuathiriwa na sababu za ndani na mfumo na vingine vinaathiriwa na mfumo.

Vikwazo vya Chadema
Pamoja na nadharia hizo, Chadema imeendelea kujipenyeza na kupata nguvu zaidi kila uchaguzi.
Hata hivyo, safari hii ilikabiliwa na vikwazo zaidi kama kujiuzulu kwa wabunge na madiwani wakihamia CCM, vikwazo vya kisheria na zuio la mikutano na kesi kwa viongozi wake.
Katibu Mkuu mpya wa Chadema, Dk Vincent Mashinji anasema pamoja na yote hayo,  Chadema haitakufa kutokana na kuishi msingi wake unaoamini katika nguvu ya umma na mabadiliko ya kweli nchini.


“Hatujawahi kubadilika katika msingi huo, mwaka 1995 na 2000 tuliunga mkono vyama vingine, mwaka 2005 tukaingia kutambulisha nguvu ya chama na siyo kuingia Ikulu. Mwaka 2010 hadi 2015 tulikuwa tumejipanga kuingia Ikulu tukahujumiwa na mfumo uliopo, tunachoamini ipo siku Watanzania watatuelewa,” anasema Dk Mashinji.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akitambua mchango na umuhimu wa vyama vya upinzani nchini katika kukuza demokrasia huku akibeza baadhi ya vyama vinavyokosoa kila jambo linalotekelezwa ana serikali.