Nguvu ya Fifa: Stromme Foundation yaingia jumla jumla soka ya wanawake

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) liko kwenye program mbalimbali za soka na zaidi ikihamasisha soka ya wanawake duniani.

Hata fedha ambazo zimeongezwa kwenye mashirikisho, soka ya wanawake ina mafungu yake. Eneo lingine ambalo Fifa inakomalia ni soka ya vijana kuanzia miaka 14 hadi 23, mafunzo kwa waamuzi hasa wanawake.

Na ili kutoa motisha, fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia Fifa imeongeza zawadi kwa bingwa, kutoka Dola15 million na sasa atapata Dola30 milioni.

Pia alisema kuwa ili soka ya wanawake isionekane masikini, maandalizi kwa jumla yametengewa Dola20 milioni na kila taifa litapata sehemu ya Dola50 milioni zitakazogawanywa miongoni mwa mataifa 24.

Fifa imefanya hivyo, lengo ni kuinua soka ya wanawake. Mgawo wa fedha za Fifa, ni kwamba Tanzania imepewa muda hadi kufikia mwaka huu kujirekebsiisha ili ianze kupata mgawo wa Fifa kwa maendeleo hayo.

Mbali na Fifa, kuna baadhi ya program zinaendelea Shirika lisilo la liserikali la Norway (Stromme Foundation na timu ya Bongo inayosimamiwa na shirika lisilo la kiserikali la OCODE hapa nchini.

Kwa kuanza ikiwa ni pamoja na msaada wa Fifa, taasisi hiyo imeanza kutengeneza wasichana waliokosa fursa ya kunufaika na elimu kuanzia shule za msingi kupata fursa ya kunoa vipaji vyao kupitia soka.

Wawakilishi wa Stromme Foundation na timu ya wasichana ya Norway ya Start Life iko nchini kuonyesha dhamira ya kuinuo Bonga kama eneo moja. Timu hiyo inashiriki Ligi Daraja la Pili.

Mshauri Mkuu wa Stromme Foundation, Lars Saaghus alisema wameichagua Tanzania kupitia OCODE ili kuendeleza vipaji vya wasichana kusakata soka katika eneo hili la Afrika Mashariki.

“Tumefurahi kuona wasichana wengi hapa wana hamasa ya kucheza soka na kushiriki kuendeleza vipaji vyao vingine.

Tunataka kuendeleza elimu zao na vipaji mbalimbali kupitia soka,” anasema Saaghush.

Kiongozi huyo wa Stromme Foundation anasema alikutana na viongozi wa TFF na Chama cha Soka mkoa Dar es Salaam (DRFA) ili kupanga namna ya kutekeleza mradi huo kabambe.

Anasema mradi huo unatarajiwa kutekelezwa hapa nchini kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya kusambaa katika nchi za Sudan Kusini, Uganda na Kenya.

“Nimefurahi sana kuona wasichana wachangamfu na waliotayari kucheza mpira wa miguu kwa ufanisi mkubwa ingawa wana umri mdogo,” Bw Saaghus amesisitiza.

Alipoulizwa juu ya bajeti ya mradi huo, alisema watakuwa wanagharimia Krona za Norway 400,000 ambazo ni sawa na Dola za Marekani 46,817 kwa kila mwaka.

Hii ina maana kuwa kwa kiwango hicho cha fedha kilichotajwa ni sawa na Dola za Kimarekani 468,168 au Sh3.38bil kwa miaka 10.

Hivyo kila mwaka OCODE itakuwa inafadhiliwa zaidi ya Sh 300 milioni kwa ajili ya kuendeleza kabumbu na vipaji kwa wasichana.

Naye mkurugenzi mtendaji wa OCODE Joseph Jackson anasema: “Wanorway wamevutiwa na mradi wa timu ya Bonga kutokana na mafanikio waliyopata kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita.

“Kuna wasichana wengi takriban mamia wamejitokeza kushiriki katika mradi huu.

Wengi wameanzisha miradi ya kiuchumi na wanashirika katika mchezo wa mpira wa miguu.

Katika kata ya msongola matokeo ya mradi ni mazuri sana,” amesema Bw Jackson.

Katika ugeni huo wa Norway, Mwananchi ilipata kuhojiana na Daktari wa timu ya mpira ya Start Life (Physiotherapist), Marianne Lislevand, ambaye anasema amefurahishwa sana na wasichana wa Tanzania wenye vipaji vya sokau ambavyo vinakosa mbinu za kuendelezwa.

Anasema ataendelea kuwasiliana na OCODE ili kutafuta njia za kunoa vipaji vya wasichana wengi hapa nchini.

OCODE imejenga madarasa kadhaa katika shule mpya ya Msingi ya Msongola na inaendesha mradi kabambe wa kuwashirikisha wasichana katika shughuli za uchumi na michezo ili waweze kujiamini baada ya kukosa fursa za kuendelea na masomo.

Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimeshirikiana na BONGA ili kutafuta njia za kunoa vipaji vya wasichana na wanatarajia kushiriki Ligi Daraja la Kwanza mkoa wa Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa DRFA Daudi Kanuti anasema mpango utasaidia kuinua soka ya wanawake hasa mkoa wa Dar es Salaam na taifa kwa jumla.