Nguvu ya mama ilivyomwezesha Ismail kuibuka kinara shule za kata nchini

Muktasari:

Ana ndoto ya kuwa mhadhiri wa hesabu chuo kikuu

Unaweza kumshangaa Ismail Mtumwa ambaye kabla hata uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha tano haujatangazwa yeye ameshaanza kujiwinda kimasomo.

Tayari ameshaanza kujisomea masomo ya Hisabati, Kemia na Fizikia, ambayo ana uhakika ndiyo atakayokuja kuyasomea kidato cha tano na sita.

Hivi ndivyo alivyo siku zote Ismail mwenye utamaduni wa kujisomea, ndiyo maana haishangazi kuwa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha ne mwaka 2018 aliibuka na ufaulu wa kishindo wa daraja la kwanza kwa alama saba.

Alipata A katika masomo saba ukiondoa masomo ya Uraia na Jiografia aliyopata alama B na C. Ufaulu huo ukamweka Ismail kileleni akiwa mwanafunzi bora zaidi kutoka shule za kata nchini. Kwa wengi ufaulu huu ukawaaminisha kuwa hata shule za kata, ufaulu mzuri unawezekana hasa kukiwa na mazingira rafiki kitaaluma na wanafunzi wanaojitambua kama Ismail.

Safari ya masomo

Haikuwa safari rahisi kwake kupata ufaulu huo. Ismail aliyekuwa akisoma katika shule ya Sekondari Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani. Anasema mama yake mzazi ana mchango mkubwa katika mafanikio aliyoyapata.

‘’ Bila yeye mama hakuna chochote ambacho kingeweza kutokea. Anajitahidi kwa kila hali kuniwezesha nifanikiwe. Namshukuru mama kwa jitihada zake,’’ anasema.

Anasema alikuwa akiishi umbali wa kilomita 35 kutoka ilipo shule, hivyo alilazimika kuamka saa kumi alfajiri kila siku ili awahi usafiri wa kumfikisha shule. Kwa mashaka aliyokuwa akiyapata, alishawahi kutamani kuacha shule.

‘’Tunaishi Mbezi Malamba Mawili Mkoa wa Dar es Salaam ambapo umbali mpaka shule ni kilomita 35. Nilikuwa naamka saa kumi usiku na shuleni nafika saa moja na nusu asubuhi, muda ambao nakuwa nimechelewa maana tunatakiwa kufika saa 12 asubuhi,”anasema.

Anasema kuwa kitendo cha kuchelewa shuleni kiliamweka kwenye wakati mgumu, kwani baadhi ya walimu hawakuwa wakimwelewa japo anasema alikuwa akifanya jitihada za kuwaelewesha.

“Baada ya kuona nashindwa kufika shule kwa muda unaotakiwa, nililazimika kuomba kibali kwa Mkuu wa shule aniruhusu niwe nafika shule saa moja. Nilikubaliwa nikawa nafika muda huo”anasema.

Anasema kuwa hali hiyo aliendelea nayo mpaka alipofika kidato cha nne kabla ya mwalimu wake nmmoja kumshauri ahamie kwake ili awe jirani na shule.

Alisema kuwa baada ya wazazi wake kukubali ushauri huo, alihamia rasmi kwa kwa mwalimu huyo huku akiwa na faraja ya kuondokana na adha ya usafiri na pia kupata muda wa kutosha kujisomea.

Mama yake

Ukiondoa hamasa alizokuwa akimpa mara kwa mara mwanawe, mama yake mzazi aitwaye Kididi Hassan anakumbuka namna alivyokuwa akilazimika kukabiliana na mzigo wa kumpatia Sh 3,000 kila siku ikiwa ni gharama ya nauli na chakula.

“Hali ya uchumi wetu ni ya kawaida sana. Mimi ni mjasiriamali na mume wangu ni fundi wa vifaa vya umeme, hivyo gharama hizo zilikuwa zinatupa ugumu, lakini kwa kuwa elimu ni haki ya mtoto tulilazimika kumhudumia mpaka hapo alipofikia na tutaendelea kuwajibika,”anasema.

Anaongeza: “… hata kama hali ya uchumi ni ya chini kwa familia, bado kuna ulazima wa kujitahidi kujinyima ili mtoto asome. Sisi mtoto wetu tumemtumikia sana ikiwamo kumpeleka twisheni. Ni bora kula ugali na matembele lakini mtoto asome.”

Anasema kuwa jambo lingine lililokuwa linampa wakati mgumu ni hofu ya usalama wa mtoto wake, kwani awali alikuwa anamuamsha usiku saa kumi na nusu ili ajiandae na safari ya shule.

“Ingawa alikuwa anachelewa kurejea nyumbani lakini akifika kwanza anafanya kazi za nyumbani ndipo anaendelea kujisomea mpaka saa tano usiku na wakati mwingine mpaka saa sita,”anasema.

Kididi anaamini jambo lililosababisha mwanawe kufanya vizuri ni ushirikiano mzuri uliokuwepo kati yake na walimu.

“Unajua kwa sasa asilimia kubwa ya wazazi wanakuwa na harakati nyingi za maisha na wakati mwingine wanasahau kuwa wanapaswa kuwa karibu na walimu ili kutafuta njia ya kumsaidia mtoto,”anasema.

Kididi aliyesoma hadi kidato cha pili, anaamini kama mzazi ametimiza wajibu wake katika mafanikio ya mwanawe.

Mwalimu wake amzungumzia

Mkuu wa Shule ya Sekondari Tumbi, Fidelis Haule, anasema kuwa walimpokea mwanafunzi huyo mwaka 2015 akiungana na wanafunzi wenzake zaidi ya 100 katika darasa la mikondo miwili.

“Juhudi zake zilianza kuonekana alipofika kidato cha pili alipopata ufaulu wa daraja la kwanza kwa alama nane akiwa amepitwa na mwanafunzi mmoja aliyepata daraja la kwanza kwa alama saba.”anasema.

Akaendeleza moto huo wa ufaulu hadi kidato cha nne alipopata daraja la kwanza la alama saba ambalo ndilo la juu zaidi katika mfumo wa mitihani ya kidato cha nne nchini.

Maandalizi kidato cha tano

Mpenda elimu utamjua. Ismail anatamani hata kesho asikie kuwa amechaguliwa ili aanze masomo.

Anasema ameshaanza kujisomea masomo ya mchepuo wa PCM akiwa na ndoto ya kuja kuwa mhadhiri wa hesabu chuo kikuu.

‘’Nataka niwe mwalimu wa walimu; niwe nafundisha wanafunzi wa chuo kikuu somo la Hisabati. Naamini kabisa nitafika huko kwani juhudi nilizonazo ni kubwa ingawa hali ya uchumi kwa familia yetu ni wa chini, “anasema na kuongeza kuwa ameamua kubobea katika somo hilo ili asaidie kutatua tatizo la uhaba wa walimu wa somo hilo.

Kwa upande wao, wazazi wanasema wameshaanza kumfanyia maandalizi ikiwamo kumnunulia vitabu na kumwekea akiba ya fedha za matumizi.