USHAURI WA DAKTARI: Ni mara ngapi unashauriwa kushiriki tendo la ndoa kwa wiki?

Sunday January 13 2019Dk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Kwani kuna ubaya wowote wa kushiriki mara nyingi zaidi au mara chache zaidi? Swali hili nimekuwa nikiulizwa mara nyingi sana na watu wanaotoka kwenye makundi yote. Walio kwenye mahusiano na walio nje ya mahusiano. Wana ndoa na wasio wanandoa lakini wanajijengea utamaduni wa kushiriki tendo la ndoa mara kadhaa. Lakini pia swali hili nimekuwa nikiulizwa na wale ambao hawapo kwenye mahusiano, na wala hawafikirii kushiriki tendo la ndoa kwa siku za karibuni japo wana uwezo huo ila kutokana tu na sababu nyingine za kimaisha.

Jibu langu mara zote limekuwa hili, “hakuna ubaya wowote” kwa kuwa jambo la kushiriki tendo la ndoa lipo kisaikolojia zaidi!

Kadri utakavyokuwa sawa kisaikolojia ndipo itakupelekea ushiriki tendo la ndoa kwa ufasaha na mara nyingi zaidi lakini pia itategemea zaidi na mshirika wako wa tendo la ndoa yaani mwenzi wako amekuvutia kwa kiasi gani, kuanzia muonekano wake, na hata namna anavyozipokea hisia zako vizuri.

Sawa! Mjadala uliopo sasa ni mara ngapi inashauriwa kushiriki tendo la ndoa kwa wiki? Nilifanya tafiti fupi ya kukutana na wanandoa na waliopo kwenye mahusiano kwenye idara ya afya ya uzazi katika kituo changu cha kazi, na zaidi ya asilimia 60 kati yao walisema kuwa wao wanashiriki tendo la ndoa mara tatu kwa wiki.

Huenda hii ni idadi inayotumika na wengi, lakini kwa ushauri wangu siwezi kukuambia kama idadi hii ni ndogo au ni kubwa.

Kisayansi, kufanya tendo la ndoa kunaimarisha mfumo wa afya ya akili na kuwafanya washiriki kujikinga na magonjwa yanayoshambulia mfumo wa akili na hasa sonona na msongo wa mawazo, hivyo kadri unavyoshiriki mara nyingi zaidi ndipo unapojiweka kwenye nafasi nzuri ya kujikinga na magonjwa haya ya akili.

Lakini ni vyema kuhakikisha kuwa unashiriki tendo la ndoa na mtu aliyekuvutia zaidi, mtu anayekuridhisha zaidi na zaidi awe mtu uliyetokea kumpenda.

Hapo ni nyie tu, hata mkifanya zaidi ya mara nne au tano kwa wiki. Ni maelewano yenu tu ili mradi ushiriki wenu hauathiri ratiba nyingine!

Advertisement