Ni mwaka wa Ulaya Fainali za Kombe la Dunia 2018

Monday July 9 2018Allan Goshashi

Allan Goshashi 

Fainali za Kombe la Dunia 2018 zinazoendelea nchini Russia tangu Juni 14 mpaka Julai 15, 2018 baada ya Russia kupewa nafasi hiyo tarehe 2 Desemba 2010 zinafikia ukingoni na kuna masomo mengi tumepata ya kujifunza.

Nina mengi ya kuzungumzia kuhusu fainali hizi, lakini ngoja zimalizike wiki ijayo. Leo ninataka kuzungumzia kwa kifupi fainali hizi kufanyika Ulaya na timu zake zimeingia hatua nzuri, Ufaransa, Ubelgiji, England, Russia wenyewe na Croatia yote ni mataifa ya Ulaya, wameitendea haki nafasi yao.

Ikumbukwe kwamba hizi ni fainali za kwanza za Kombe la Dunia kufanyika Ulaya tangu mwaka 2006.

Mwaka 1974, mwanasheria kutoka Brazil, Joao Havelange alimshinda Stanley Rous raia wa England aliyekuwa rais wa Fifa katika uchaguzi na hivyo kuwa rais mpya wa Fifa na ndipo alipoanza kufanya mageuzi mengi makubwa ndani ya Fifa.

Havelange alisaidia kuongeza idadi ya timu katika Fainali za Kombe la Dunia kutoka timu 16 mpaka 32 na hivyo kuongeza idadi ya timu nyingi za Afrika na Asia kushiriki katika fainali hizo ambazo zilikuwa na timu nyingi za Ulaya, pia alianzisha mashindano ya dunia ya vijana kwa umri tofauti na kuifanya Fifa kuwa shirika kubwa linaloongoza mchezo wa soka.

Mwaka 1998, Havelange akiwa na miaka 82 aliacha kuiongoza Fifa na kumpendekeza Sepp Blatter (raia wa Uswisi) kuwa ndiye anafaa kuliongoza Shirikisho hilo wakati huo Blatter alikuwa katibu mkuu wa Fifa. Wakati huo Ulaya ya Kaskazini ilikuwa ina mpango wa kutaka kupata tena nafasi ya kuiongoza Fifa kwa hiyo ilikuwa ikiona rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Lennart Johansson ndiye anayefaa kuiongoza Fifa, lakini alishindwa na Blatter.

Blatter baada ya kushinda uchaguzi huo aliamua kuvunja utawala wa Ulaya na Amerika katika kuandaa Fainali za Kombe la Dunia na kuipa Japan na Korea Kusini kuandaa Fainali za Kombe la Dunia 2002.

Ugomvi wa Blatter na nchi za Ulaya ulianza alipotangaza kwamba anataka kuzipeleka Fainali za Kombe la Dunia barani Afrika na alikaribia kuzipeleka mwaka 2006, lakini hata hivyo mjumbe wa bara la Oceania, Charlie Dempsey alijitoa katika dakika za mwisho za upigaji kura hivyo Ujerumani kuishinda Afrika Kusini.

Baada ya hapo Blatter alikuja na mpango kwamba Fainali za Kombe la Dunia zitafanyika kwa mzunguko katika mabara yote kwa hiyo Fainali za Kombe la Dunia 2010 akachagua zifanyike Afrika. Hivyo zikapigwa kura kati ya Morocco na Afrika Kusini, katika kura hizo Afrika Kusini iliibuka mshindi.

Baada ya Fainali za Kombe la Dunia 2010 kumalizika nchini Afrika Kusini, rais wa klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, Uli Hoeness alisema kwamba uamuzi wa Fifa kuzipeleka fainali hizo Afrika ulikuwa wa makosa makubwa na kudai uamuzi huo ulifanyika kwa rushwa.

Hata hivyo Blatter alimjibu Hoeness kwa kusema,”Kuna ule mtazamo wa kizamani kwa nchi za Ulaya kwamba kwa nini Afrika iandae Fainali za Kombe la Dunia, unajua wakoloni kwa zaidi ya miaka 100 walienda Afrika na kuchukua vitu vyao vizuri vingi na mpaka sasa wanachukua wachezaji wao bora, hakuna heshima kabisa.”

Baada ya Afrika kupewa nafasi ya kuandaa fainali za 2010, fainali hizo zilipelekwa Amerika Kusini, kwa hiyo Brazil ndiyo iliziandaa mwaka 2014. Baada ya hapo fainali hizo zilitakiwa kufanyika Ulaya, hivyo England ilikuwa ikaona ina nafasi kubwa ya kuandaa fainali za 2018, lakini ikakosa na ikapewa Russia.

Advertisement