UCHAMBUZI: Ni vigumu shule kufundisha kila kitu

Tuesday January 15 2019

 

By Joseph Chikaka, Mwananchi

Mfumo wa elimu wa nchi yoyote duniani huhusisha uchaguzi wa maarifa na umahiri unaopaswa kurithishwa kwa wanafunzi katika kila ngazi ya elimu. Maarifa hayo na ujuzi hupimwa kwa namna mbalimbali ili kuweza kutathmini utekelezekaji wake kwa walengwa.

Mamlaka husika huchagua ni maarifa gani na ujuzi gani ambao hupaswa kufundishwa shuleni. Aghalabu, watu wengi wamekuwa wakitamani kuona kila kile wanachofikiri kinaingizwa katika mfumo rasmi wa elimu na kwa kuwa kinafaa kwa maisha, basi kiweze kufundishwa shuleni.

Jambo hilo siyo rahisi hususani kwa nchi ambazo zinatumia mfumo wa kuwa na mamlaka ya elimu inayotunga, kusimamia na kukuza mitalaa.

Zipo sababu nyingi zinazoeleza kwa nini shule haziwezi kufundisha kila kitu ama kila maarifa yaliyopo duniani au nchini.

Miongoni mwa sababu hizo ni kuwapo kwa taarifa au maarifa mengi duniani

Kila kukicha maarifa na ujuzi vimezidi kuongezeka duniani.

Watu wengi binafsi na taasisi wanafanya tafiti na kutoka na majawabu mapya ya kutatua matatizo mbalimbali yaliyopo katika jamii. Kila siku kila saa maarifa na ujuzi huo unaozaliwa huingia katika ushindani wa kipi kipya na kilichothibishwa ili kiweze kutumiwa.

Sababu nyingine ni mabadiliko yanayotokea duniani kila siku. Dunia hubadilika kila siku katika elimu ya masuala mbalimbali. Wakati mwingine mabadiliko hayo husababisha maarifa ambayo siku za nyuma yalionekana kufaa sana baada ya kupitwa na wakati maarifa hayo huonekana ni ya kale.

Hivyo na mifumo ya elimu pia nayo itaendelea kubadilika kila siku ili kuweza kukidhi mahitaji ya jamii. Vivyo hivyo na mitalaa ya elimu nayo itaendelea kubadilika ili kukidhi malengo ya elimu kwa ujumla.

Pia, kukua kwa kasi kwa sayansi na teknolojia kumesababisha maendeleo makubwa kwa dunia. Vitu hivi vinafanya maarifa kubadilika kila siku.

Pamoja na hayo, wataalamu wa elimu wanapaswa kuichagulia jamii maarifa na ujuzi ambao ni muhimu. Yawe ni maarifa yanayoweza kutumika na kila mwanafunzi shuleni na mara baada ya kuhitimu.

0658 423 258

Advertisement