NDANI YA BOKSI: Nipe Nandy, Ruby na akili za Gigy Money

Unakutana na msichana ana iPhone ya bei kali. Kila siku hakosi bando la ‘intaneti’, analewa, usafiri wake siyo daladala ni Uber, Taxfy au bodaboda. Kila ‘wikiendi’ yupo viwanjani akiwa na pamba na nywele mpya. Amepanga chumba Tabata, hana kazi zaidi ya kuchati katika ‘magroup’ na instagram.

Huyo ni wa utawala huu wa Msukuma. Wakati ule wa Mkwere, ungekutana na asiye na kazi wala biashara. Kapanga nyumba nzima Sinza au Kinondoni. Anasomesha wadogo zake shule za gharama. Ana ndinga kali, analewa kila siku huku pia akikimiliki ‘kiserengeti boy’ anachokilisha, kukivisha na kukipangia chumba.

Haya ndo maisha ya Daslama mjini. Watu pekee waliotoweka ni wale wa “Unanijua mimi ni nani?” Wengi wao wako Segerea kama siyo Keko basi wamejikita huko ‘Sauzi’. Wamekimbia au kutoweshwa mjini. Pesa za udananda hakuna.

Na kwenye muziki kulikuwa na wadananda waliopelekea ‘bifu’ kati ya wasanii kadhaa na Clouds Fm. Wasanii wakidai kubaniwa. Na watangazaji wakiwa wahanga wa lawama. Huku baadhi ya makundi na wanamuziki wakionekana kufaidika na uwepo wa Clouds. Hao usingewasikia wakilalamika kuhusu Clouds.

Said Fella na Babu Tale ni miongoni mwa wana ambao usingesikia wakilalamika. Kwanza wangekuona mchawi wa maisha yao kuwahusisha na ‘harakati magirini’ zako za kuisema Clouds Fm. Wao walikuwa jikoni wakati huo wakipika na kupakua. Wakawa na sauti kana kwamba ‘wanalimeneji’ mpaka lile ghorofa pale Mikocheni.

Huo ulikuwa utawala uliopita (zilipendwa). Ikulu kila wikiendi. Kunywa ‘juisi’ na Mkwere huku vichwa vyao vimesokotwa nywele na suruali zimelegea kama nyaya za simu za mezani (TTCL) kwenye makalio.

Leo hii hali ni tofauti. Maisha yamebadilika. Hakuna ‘pati’ za kupongezana. Said Fella na Babu Tale nao wamebadilika. Kutoka maisha ya utiifu na unyenyekevu kwa Clouds mpaka uadui mkubwa. Yaani walichofanya ni kukopa hasira za Vinega wa Ant Virus kisha wakapandikiza vichwani mwao.

Maisha na unafki ni pacha. Walioonekana kubebwa na Clouds leo ndo wamekuwa walalamishi wakubwa. Hawaogopi tena kama zamani, anayeingia kwenye anga zao wanamparua vibaya kama kilichomtokea Fid Q. Ujasiri huu ni kitu bora kama wanafanya kwa ajili ya sanaa kwa ujumla. Ila sidhani.

Nasema hivi kwa sababu wengi wao wamekuwa imara kwa kujitetea wenyewe tu na siyo wengine. Wanaonewa? Okay sawa. Wameamua kujikomboa wenyewe? Ni vyema na haki. Hata kusema tu naonewa si kitu kibaya ni jambo zuri sana. Lakini je, hapo kabla waliwahi kuzuia au kuwapigania walioonewa? Hakuna!

Hivi sasa Tale na Fella na wenzao wanajipigania matumbo yao kama walivyofanya walipokuwa bega kwa bega na Clouds. Kujitetea unaweza, lakini haina maana kabisa kama asilimia kubwa ya kundi la wanzako wanaendelea kuonewa. Kubaki peke yako unayejiweza huku wengi wakionewa ni kazi bure.

Jide alikuja kuweka wazi maumivu yake kwa Clouds mwaka 2013. Kabla hakuthubutu. Miaka 10 nyuma au zaidi alikaa kimya, akila na kipofu. Nyimbo zake zikagongwa huku akienziwa kama Malkia wa Bongo Fleva.

Jide ni mkali. Mi binafsi ni shabiki wake. Lakini si sahihi kudai alichofanya kilikuwa bora kiasi cha kumpa ‘ustaa’ mkubwa. Hapana. Maadui zake wa sasa walivuja jasho kumuweka pale alipo. Kama malalamiko yake juu yao baada ya miaka kumi yalikuwa sahihi, basi ana kipaji kikubwa cha uvumilivu kuliko muziki.

Wasanii wana utajiri wa unafiki. Chuki. Kugeukana na kujenga makundi. Hawajahi kuwa na umoja. Wengine walipolia. Siyo Jide, Tale, wala Fella waliotetea muziki na wasanii. Walikaa kimya kulinda keki yao kwa wakati huo. Hawakuwa wajinga bali ni mbinu ya kumtumikia kafiri. Bila hivyo hata walichonacho leo wasingepata.

Hawakutaka kupinga nyendo za ubaguzi wa nyimbo na wasanii au uonevu wowote toka kwa washika mpini. Kilio cha Sugu na Vinega wake, pamoja na ‘andagraundi’ wengine wengi kwao ilikuwa kama vituko vya Bwakira na Mkude Simba. Walalamishi walionekana wanatapatapa au kuishiwa kimuziki!

Kilio kile ndo kilio cha leo. Bwana Misosi alikuwa na mstari katika wimbo wa “Nitoke Vipi?” Anasema: “Sugu ni Mkongwe, kastaafu tena kwa heshima, Wabongo wamemchoka na kimtindo wamemtema”. Bwana Misosi mwenyewe hivi sasa sijui anashughulika na uvuvi wa Kambare au ufugaji wa nyuki wadogo.

Wasanii waliokuwa wanaibukia kwa wakati ule kama kina Misosi na wenzao hawakujua madhila ya wenzao. Wakavimba vichwa na kutanua mabega kama wacheza sumo. Kwa kuamini wao ni bora. Mwisho wa siku wengi wamejifia kwa stress huku wengine wakijenga undugu na dawa za kulevya.

Muziki kama pesa za majini. Unakupandisha juu kama yule mwewe ‘Ndege John’ kisha unakuacha. Ukishindwa kujishikilia unakwenda chini jumla. Vinega walimaliza stress kwa ‘mitusi mtambuka’, Chidi Benzi, marehemu Langa na wenzao wakamalizia kwenye mondo (unga). Noma sana.

Jide na wengineo wameisha kisanii? Hapana. Muziki wa kizazi kipya watu wake wengi mapoyoyo, wachovu wa kufikiri. Wasio na hulka ya uthubutu. Watu wa kusubiri waletewe kisha wakiyumba waanze gubu na kumsaka wa kumuangushia lawama. Ndiyo maana kila anayekosea hesabu zake, lawama ghorofani.

Mtazame Nandy. Kwa mtazamo wa nje huwezi kujua lolote kama ana tatizo na sanaa yake. Anaonekana mtu wa kupata anachotaka na kula apendacho. Ndivyo tulivyomuona Jide na wenzake wakati ule. Subiri mambo yageuke. Lakini kwa sasa husikii wakisema neno zaidi ya kusifia mafanikio.

Wanaolia leo ni wanafiki. Hawana tofauti na wale wa “Unanijua mimi ni nani?” Ambao utawala huu umewahamisha mjini. Wanajipigania wao siyo kwa muziki na wamamuziki. Kama wapo kwa maslahi ya muziki wangeungana na wenzao toka wakati ule. Matatizo haya yalikuwepo na walikaa kimya.

Afande Sele aliwaona vichaa Vinega wa Ant Virus walipolalamika juu ya wadau wa muziki. Leo hii kabadili gia gizani (maana siyo angani) analalamika kwa namna ileile waliyotumia kulalamika aliowaona wehu. Ndo maisha ya wanamuziki wa kizazi kipya (unafki). Walichelewa kuanika tabia zao hadharani.

‘Gemu’ la muziki limejaa watu wanafiki tupu. Ambao wanajali matumbo yao kuliko akili. Wako radhi wakatwe vichwa vyao ili mradi washibe. Na ndo chanzo cha yote yanayotokea kiasi cha kina Dudubaya kujitoa ufahamu hii leo. Zile ni stress. Na kila mtu ana namna yake ya kupunguza stress kichwani.

Sanaa ya muziki Kibongo ni kama ndoa ya mwanamke mtu mzima. Ambaye anateswa lakini hataki talaka. Kwa hofu ya watoto au ataolewa na nani tena umri ushamtupa mkono. Kwa wasanii waliopandishwa juu na watu tu, ndo wanaumizwa na hawasemi kuogopa kushushwa chini.

Bongo Fleva inahitaji watu wenye vipaji vikubwa kama Ruby na wenzake. Lakini wenye akili kama Gigy Money. Mfuatilie Gigy Money hulka zake utanielewa. Ni aina ya viumbe ambao hawajui kupindisha jambo.

Gigy Money akipewa nafasi hiyo hawezi kuishi kwa mateso haya ya kibwege.

Ukweli unamuacha mtu huru. Jide akikusimulia alivyounga unga mpaka kumiliki bendi. Utagundua wewe uliyemsikia redioni na kumtazama runingani tu ulikuwa na amani ya moyo na nafuu ya maisha kuliko yeye. Kitu ambacho akili ya Gigy Money kamwe isingeweza kuvumilia. Miaka ileile angekiwasha.

Babu Tale na Said Fella. Mtu mgeni anaweza kukataa kama hawa watu walikuwa zaidi ya staff wa pale Clouds. Ukisikia maneno yao leo utashangaa kama ni wao au misukule yao? Siyo wajinga jamaa. Wasingekuwa hapa walipo bila unafiki.

Kama toka mwanzo tungechanganya vipaji vya kina Lady Jaydee na akili mtambuka kama za Gigy Money. Huenda lile bata la kina WizKid na wenzao lingetafunwa kitambo sana na kina TID. Tatizo wengi waliishi kinafiki ili washibe wao maisha yaendelee. Naomba muelewe. Wadau wakubwa wa muziki siyo Clouds tu. Ni pamoja na Basata. Vyombo vyote vya habari. Makampuni makubwa ya biashara ambayo yalitumia na yanatumia muziki kujitangaza pamoja na serikali yenyewe. Vyote hivi kwa pamoja vimechangia umasikini kwa wasanii.

Hawawezi kusema ukweli sababu vimelea vya unafki bado vimejenga vibanda kwenye akili zao.

Lakini ukweli ni kwamba fujo za Vinega wa Anti Virus. Ambazo wajinga waliona ‘harakati magirini’. Ndiyo chanzo kikuu cha kupanda kwa kiasi kikubwa malipo mazuri ya shoo kwa wasanii. Waulize kina Shetta.

Mleteni Ruby na Nandy. Nipeni Vanessa Mdee na Jide. Kama hamtaniletea na akili mtambuka ya Gigy Money. Basi hawa wote kaeni nao tu siwataki. Tunahitaji vipaji vya muziki na akili za Kigigy Money. Ambaye anaweza kusema bila hofu kuwa ‘prodyuza’ flani anataka nimpatie ‘papa’ anitengenezee ‘biti’. Unafki bakini nao.