Nyambaya: Serengeti Boys ni Taifa Stars ijayo

Monday April 8 2019

 

Fainali za soka Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 za mwaka huu zinapigwa hapa nyumbani kuanzia Aprili 14 wiki hii.

Mpaka sasa maandalizi ya mwishomwisho yanaendelea kwa ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kujua undani wa matayarisho ya kikosi chetu cha Serengeti Boys kitakachoiwakilisha Tanzania, Spoti Mikiki lilifanya mahojiano na Makamu Mwenyekiti wa Soka la Vijana, Lameck Nyambaya ambaye anaelezea mipango ilivyo lakini pia uwekezaji wa jumla katika eneo la soka la vijana.

Maandalizi ya Serengeti Boys

Nyambaya alianza kuelezea jinsi ya matayarisho ya kikosi cha Serengeti alisema: ”Timu inaendelea kupata uzoefu mkubwa na kesho alfajiri watarejea wakitokea Rwanda walikokwenda kushiriki mashindano maalumu ya vijana,” anasema Nyambaya huku akiendelea kueleza.

“Shabaha ya TFF ni kuona vijana wanapata uzoefu wa kutosha ili wawe tayari kwa kushindana utaona chini ya Rais Karia (Wallace) .

“Timu ilikuwa kwenye maeneo mbalimbali ya mashindano na bahati nzuri ilifanya vizuri

“Kulikuwa na mashindano ya vijaba kule Burundi yale ya Cecafa, lakini pia mashindano ya Cosafa ambayo tulitwaa ubingwa. Pia tuliipeleka Uturuki kule walipata mechi zilizosaidia maandalizi, lakini kama haitoshi wakaunganisha mpaka Rwanda.

“Kule Uturuki walipambana lakini matokeo hayakuwa mazuri sana, lakini cha msingi ni mazoezi waliyopata.

“Mechi na Australia, mechi na Uturuki lakini hata ile ya Guinea ziliipa timu maandalizi ya maana.

“Unajua mtu anaweza kuangalia kufungwa, lakini matokeo yale yalikuwa na maana sana.

“Kama ukiangalia pia mashindano ya Rwanda, sasa yale yanaweza kuwa majibu ya Uturuki kwani timu yetu iliifunga Cameroon mabao 2-1 lakini ikatoka sare ya 3-3 na Rwanda.

“Rwanda walisawazisha dakika za lalasalama, sasa hapa ni kirekebisha maeneo madogo, upande wa makipa na mabeki, ninaamini kocha ameliona na atalifanyia kazi,” anasema

Nyambaya anasema matokeo ya ushindi wa jumla waliyoyapata kule Rwanda walipokutana na Cameroon na Rwanda utaona jinsi timu inavyoimarika, ingawa bado kuna changamoto chache na anaamini makocha watazifanyia kazi ili tuwe sawa.

Malengo ya TFF

“Unajua uwekezaji wa kuzalisha vijana ni sera ya uongozi huu wa TFF tunatambua kwamba uzalishaji wa vijana ni jukumu kubwa la klabu lakini kwa sasa TFF itaendelea kuzilea hizi timu ili kuweza kuzalisha wachezaji wa kutosha wa timu za taifa.

“Kwasasa tuna vikosi vya U-23, U-20, U-17 na Taifa Stars lakini wakati tunafanya vipimo vya timu ya U-17 tulipata wachezaji wazuri ambao umri wao umezidi.

“Hawa hatukutaka kuwapoteza tumewaundia timu yao ya U-18 ambao wameondoka juzi kwenda Misri utaona ni jinsi gani tunataka kuona malengo ya kuzalisha vijana yanatimia.

Vijeba waepukwa

Tanzania iliwahi kuondolewa kwenye mashindano miaka ya nyuma kufuatia kubainika wachezaji kuzidi umri hapa Nyambaya ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF nalielezea hilo akisema: “Kama kuna nchi itakayokuwa na umakini mkubwa katika kutafuta vijana sahihi kwa umri sahihi baso Tanzania tunaweza kuwa ndani ya timu mbili bora.

“Ngoja niwaambie kila timu zetu hizi za vijana zinapokwenda kushiriki mashindano mbalimbali ukiacha kufanya vizuri kwa kucheza soka la kuvutia lakini mataifa mengi yamekuwa yakitusifia kwa kuchukua vijana wenye umri sahihi.

“Hatutaki kuharibu heshima ya taifa letu ndiyo maana umakini huo unaanzia mbali kwa sisi wenyewe kwanza kuwa makini katika kutafuta vijana na kuwachuja kwa usahihi lakini pia kama tunaona kuna mashaka maamuzi yetu ni kufanya uamuzi ambao utakuwa na tija.

Maandalizi ya viwanja

Nyambaya ambaye ndiye mkuu wa kituo cha kila mashindano kwa Dar es Salaam, anasema fainali hizi zitatumia viwanja viwili ambavyo ni Uwanja wa Taifa na Azam Complex katika mashindano hayo lakini pia Uwanja wa Uhuru kama uwanja wa mazoezi hapa Nyambaya anasema: “Mpaka sasa tuko vizuri katika maandalizi utaona juzi tu Waziri Mwakyembe (Dk Harrison) alifanya ziara ya kufuatilia matayarisho haya na tunaendelea vizuri pale Uhuru nyasi zimebadilishwa.

“Timu zitakuwa zikifanyia mazoezi pale lakini pia Uwanja wa Taifa na ule wa Azam zile changamoto zote tulizotakiwa kuzifanyia kazi mpaka kufika Jumatano wiki ijayo (wiki hii) zitakuwa zimemalizwa na kuacha sasa kusubiri mashindano.

Wito kwa Watanzania

“Wito wangu kwa Watanzania wenzangu hebu tushikamane kuisaidia Serikali na TFF kuhakikisha fainali hizi zinakuwa na mafanikio kwa taifa letu.

“Kuna uwezekano mkubwa viongozi wakubwa wa Fifa wakaja nchini hii ni ishara njema kwa taifa letun kwa kuaminika.

“Hapo kabla hatukuwa tunapata ugeni wa namna hii lakini sasa kupitia uwazi wa uwendeshaji chini ya Rais Karia ishara njema kama hizi zimeanza kuonekana watu waje kwa wingi viwanjani kufuatilia mashindano haya lakini hasa mechi za timu yetu kama tulivyofanya mechi ya Taifa Stars.

“Vijana wameonyesha ni watu sahihi kupigania heshimja ya taifa sasa tuje kuwaunga mkono lakini pia wadau mbalimbali wajitokeze zaidi kuasaidiana kusimamia mashindano haya kwa michango mbalimbali.|

Advertisement