Patashika ya hotuba za upinzani kuondolewa, kuhaririwa bungeni

Tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti mwaka 2019/20 si jambo la ajabu kuona vitabu vya hotuba za wasemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu wizara mbalimbali karibu kila kurasa vikiwa vimeandikwa, “maneno haya yameondolewa kwa maelekezo ya kiti.”

Kwa mujibu wa kiti maneno hayo yanadaiwa kuwa si ya kibunge, hata wasemaji wa upinzani wanaposoma hotuba halisi huzuiwa na kutakiwa kusoma zilizofanyiwa uhariri na kuondolewa baadhi ya maneno.

Kubwa kuliko yote ilikuwa ni hotuba ya upinzani kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuondolewa kabisa katika kumbukumbu za Bunge huku ile ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuhusu Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kutosomwa bungeni, lakini ikaingia katika kumbukumbu za Bunge.

Asubuhi ya siku ambayo Mbowe alitakiwa kusoma hotuba yake, wapinzani walitoka bungeni kupinga kusimamishwa kuhudhuria Bunge kwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na kuzuiwa na Spika Job Ndugai kurejea bungeni jioni.

Walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kumsindikiza Lema ambaye alikumbana na adhabu ya kutohudhuria vikao vitatu vya Bunge kutokana na kusisitiza kuwa Bunge ni dhaifu, akiunga mkono kauli ya mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliyekumbana na adhabu ya kutohudhuria vikao viwili vya Bunge.

Hata Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali alipotaka kuisoma alikataliwa kwa maelezo kwamba spika hakuwa na maandishi yanayoelekeza hivyo.

Spika Job Ndugai alipoulizwa kuhusu suala hotuba hizo kuhaririwa na uongozi wa Bunge alisema hakuwepo kwa muda bungeni na akataka apewa muda ili aweze kulifuatilia jambo hilo kwa kina.

“Sikuwepo kwa kweli ila baada ya Pasaka (kuanzia jana) nitaangalia hili jambo lipo namna gani. Nitajibu suala hili nitakapofuatilia kwa kina maana ukiniuliza nini kimeondolewa hata sijui,” alisema Ndugai.

Katika ufafanuzi wake Mbowe alisema, “Watadhibiti vyama vya siasa nje ya Bunge, mikutano ya vyama vya siasa, kuminya uhuru wa vyombo vya habari na walizuia vikao vya Bunge visionyeshwe moja kwa moja na haya mambo yalikuwa na maana kubwa sana kwa nchi.”

“Bunge likiwa moja kwa moja wananchi wanaona kila kitu lakini kwa sasa Bunge linatoa kitu ambacho wanataka wananchi wakisikie. Waliona Bunge Live liliwapa wapinzani nguvu kubwa na katika uchaguzi wa 2015, walitengeneza mkakati baada ya uchaguzi ili lisionekane moja kwa moja.”

Mbunge huyo wa Hai alisema zuio la Bunge Live liliwafanya kuhamia katika mikutano ya hadhara ambayo pia ilizuiwa na waliporejea kueleza mambo mbalimbali bungeni, pia maneno yao yanaondolewa, jambo linalofanya yasiingie katika kumbukumbu za Bunge.

“Walibaini kuwa sekretarieti ya KUB (Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni) ndio huandaa hotuba na tafiti na walifukuzwa wote mwaka jana mwanzoni na waliobaki ni sekretari, dereva mmoja na mkurugenzi ila watumishi wote waliondolewa,” alisema Mbowe.

“Kwa sasa hawaruhusiwi kuingia katika maeneo ya Bunge, unaweza kuwafungia watu ila si kwa mawazo. Leo kambi ya upinzani ina watumishi ambao hawaruhusiwi hata kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge.”

Mbowe alibainisha kuwa kwa sasa wanaandaa hotuba zao nje ya Bunge na zinahakikiwa na kutakiwa kuziwasilisha siku moja kabla ya kusomwa, “Wanatoa baadhi ya maneno ambayo wanaona hayafai, na wanasema kiti kimeamua maneno yatolewe. Ni kawaida kukuta nusu ya hotuba imeondolewa.”

Alisema hotuba ya kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni ndiyo hutoa dira kwa hotuba zote za kambi hiyo, lakini ilizuiwa katika mazingira ambayo si ya kawaida.

“Spika alisahau kuwa kuna wabunge wengine wa upinzani walikuwa hawapo wakati wengine tukitoka bungeni na ikawa ngumu kuwazuia. Tukawaagiza wakaisome kwa niaba yetu lakini walikataliwa huenda ilionekana inatoa mwanga katika masuala mbalimbali,” alisema Mbowe.

Alipoulizwa nini kifanyike, Mbowe alisema, “ujenzi wa demokrasia ni safari ndefu, ni hapo ambapo Watanzania wataelezwa hili si tatizo la Mbowe wala Chadema, ACT wala CUF. Uongozi wa Bunge haututendei haki na hatujawahi kuona mambo haya katika mabunge yaliyopita.”

Huku akitolea mfano uchaguzi wa Arumeru Mashariki kwa mgombea wa CCM kupita pekee huku wengine wa upinzani wakidaiwa kutotimiza masharti, alisema, “Ni bahati mbaya sana kwa demokrasia ya nchi hii. Kiti cha Spika kinaamua kufanya uamuzi ambao unashangaza sana kwa kweli.”

Kaimu mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Joseph Selasini alisema, “Wiki ijayo tutakaa kama kambi na kufanya tathmini ya hali hii na kulitolea ufafanuzi wa kina, tutawasikiliza wabunge wanasema nini kisha tutatoa maoni yetu. Katiba ya nchi inazungumza uhuru wa wananchi kusema, kuikosoa Serikali na uhuru wa habari. Sasa kama wabunge tunazuiwa kutoa maoni maana yake ni watu wa kawaida au wanahabari wakiyatoa si ndio itakuwa mbaya zaidi. Taifa linaloheshimu maoni ya viongozi peke yake ni taifa la aina gani.”

“Hili jambo si zuri kumbuka Bunge liliondoa wasaidizi wa kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni ambao walikuwa wakitusaidia kufanya tafiti na kuandika hotuba. Kuna mwaka mmoja hotuba za upinzani hazikusomwa kabisa bungeni. Baadaye tulifanya utaratibu tukaamua kuchangishana wabunge kwa ajili ya kuwawezesha wanaotufanyia utafiti ili kupata maoni.”

Selasini aliongeza, “Kinachotuumiza ni kwamba waliwaondoa wasaidizi wa kufanya hiyo kazi. Pili tulipofanya utaratibu wa kujinyima ili tulete maoni, sasa wanataka tuandike maoni ambayo wanayataka wao, yaani maoni yawe yao si yetu.”

Selasini alisema Bunge linahitaji mjadala na Serikali inahitaji mawazo ili iweze kujitathmini na kufanya vizuri zaidi. Kuzuia hotuba za upinzani ni kuwakosea wapinzani na Taifa linataka kusikiliza maoni mbadala.

Mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde alisema,

“hiki kitendo hatukipendi, kinachoonekana ni Serikali haipendi kusikiliza maoni yanayowakwaza, wanachotaka ni kusikia maneno mazuri tu. Katika hotuba vitu vinavyoondolewa ni vitu vinavyotokea na sisi tunavikemea.