Pele katikati ya Messi na Ronaldo

Monday January 7 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi

Moja ya mijadala ambayo imekuwa ikiibua maswali mengi kwa wapenda soka ni kuhusu nani na yupi ambaye anaweza kuwa kwenye orodha ya wachezaji bora wa muda wote duniani au legendari.

Wapo wachezaji wengi wanaopewa kipaumbele na heshima kubwa kwenye soka kutokana na mafanikio waliyoyapata wakiwa na klabu zao hadi kwenye ngazi ya taifa, wafuatao ni nyota 10 miongoni mwao.

1. Pele

Jina lake kamili ni Edson Arantes de Nascimento akitambulika rasmi mara baada ya kuiongoza timu yake ya Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1958 akiwa ana miaka 17 hu ku akifunga mabao sita katika michuano hiyo likiwemo goli la ushindi katika fainali zilizoifanya Brazil ishinde taji lake la kwanza katika michuano hiyo. Miaka minne baadaye yaani mwaka 1962, Brazil ilishiriki Fainali hizo lakini kwa muda huo wakiwa mabingwa watetezi. Lakini hali haikuwa nzuri kwa Pele ambaye alipata majeraha katika mchezo wake wa pili.

Ukiachana na mambo mengi aliyoyafanya hapo kati, mwisho wa siku aliweka rekodi kubwa ya magoli 1,281 katika maisha yake ya soka na kumfanya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye historia ya soka duniani.

2. Diego Maradona

Maradona nae hakumaliza soka lake vizuri ambapo aliingia kwenye kashfa ya kutumia dawa za kulevya.

Ukiachana na makosa mengi aliyokuwa akiyafanya kwenye soka lakini uwezo wake uliendelea kuwa juu akiwa na uwezo wa kukimbia kwa kasi na kuufanya mwili wake unyumbulike zaidi.

Uwezo wake mkubwa uliifanya Napoli kushinda mataji ya ligi kuu Italia na UEFA Cup.

3. Lionel Messi

Hakika kuna ladha ukimtazama wakati akiwa uwanjani, makubwa anayoyafanya yanadhihirisha ana mengi ambayo Mungu amemjaalia kwenye miguu yake.

Ukiachana na rekodi nyingi alizoziweka lakini pia mpaka sasa yeye ndiye mfungaji bora wa muda wote katika Ligi kuu Hispania maarufu kama La Liga lakini pia akiweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga magoli mengi Barcelona.

Messi ana mataji nane ya Ligi Kuu Hispania, mataji manne ya Klabu Bingwa Barani Ulaya na tuzo ya mchezaji bora wa dunia akishinda mara tano uku mara nne akishinda mfululizo.

Usisahau pia anashikilia tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014.

4. Johan Cruyf

Ndiye mwanzilishi wa mtindo wa soka wa Total Football ambao umekuwa na kufanya makubwa klabuni Barcelona lakini pia akihusika kwa kiasi kikubwa kuanzishwa kwa akademi ya Barcelona maarufu La Masia.

Mwaka 1974, katika Fainali za Kombe la Dunia aliiwezesha Uholanzi kufanya vyema kwenye michuano hiyo uku akitengeneza mtindo wake uliopewa jina la ‘Cruyf Turn’.

Kabla yake yeye hakuna klabu ya Uholanzi iliyowai kushinda taji la Ulaya lakini mpaka yeye anaachana na Ajax, aliifanya klabu hiyo kushinda taji la Ulaya kwa miaka mitatu mfululizo lakini pia alipojiunga na Barcelona mwaka 1973, aliifanya klabu hiyo ishinde taji lake la kwanza la ligi kuu Hispania baada ya miaka 14.

4. Alfredo di Stefano

Aliwahi kusema: “Sisi wote ni wachezaji, tunacheza soka hivyo tunapaswa kucheza katika nafasi zote uwanjani.” ndio uwezo aliokuwa nao, alikuwa na uwezo wa kucheza karibu kila namba uwanjani, lakini akitumika haswa kama mshambuliaji wa kati.

Alifanya makubwa wakati alipokuwa na Real Madrid ambapo huko aliiongoza kuweka rekodi ya kushinda mataji matano mfululizo ya michuano ya Ulaya hiku akihusika kwenye ufungaji wa kila mchezo miaka hiyo ya 1950.

5. Ferenc Puskas

Jina la Puskas wengi wamezoea kuliskia likitumika kama tunzo ya goli bora la dunia inayotolewa na chama cha soka duniani (FIFA), lakini jina hilo ni jina la nyota wa zamani raia wa Hungary ambaye aliutumia vyema mguu wake wa kushoto kufanya makubwa mpaka kufikia hatua ya kupewa heshima ya jina lake kutumika kwenye tuzo ya goli bora la mwaka.

Alikuwa msaada mkubwa kwa taifa lake kufikia fainali ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1954 lakini pia akiisaidia Real Madrid kufanya makubwa kwenye ulimwengu wa soka.

Maisha yake ya soka yalionekana kama yameshaisha mara baada ya kufungiwa kucheza soka kwa miaka miwili na chama cha soka duniani (FIFA) lakini klabu ya Real Madrid ilimrudisha tena kwenye soka.

6. Franz Beckenbauer

Anakumbukwa sana kutokana na ukali wake uwanjani na aliisaidia timu yake ya taifa ya Ujerumani kushinda taji la Ulaya mwaka 1972 pamoja na Kombe la Dunia mwaka 1974 huku akiisaidia pia klabu yake ya Bayern Munich kushinda mataji matatu ya Ulaya pamoja na mataji manne ya Ligi Kuu na mwenyewe akishinda tuzo mbili kama mchezaji bora Ulaya.

Aliinoa Ujerumani Magharibi kushinda michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1990 na kuweka historia ya kubeba taji akiwa mchezaji na kocha.

7. Zinedine Zidane

Ni moja kati ya viungo wachezeshaji wachache waliowai kuliteka soka la dunia na kufanya makubwa katika miaka yao akikumbukwa vyema kwa goli lake bora zaidi alilolifunga kwenye mchezo wa fainali ya Klabu bingwa Ulaya mwaka 2002.

Lakini pia akiisaidia timu yake ya taifa ya Ufaransa kushinda taji la Kombe la Dunia kwa kuibamiza Brazil magoli 3-0 na Zidane akifunga mara mbili mwaka 1998.

Tuzo zake tatu za mchezaji bora wa mwaka zilizokuwa zikitolewa na FIFA na nyengine ya mchezaji bora wa Kombe la Dunia havikumfanya amalize soka lake vizuri.

Mwaka 2006 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Italia alimpiga kichwa mlinzi wa Italia, Marco Matterazzi na kupata kadi nyekundu.

8. Paolo Maldini

Anakumbukwa sana kwa makubwa aliyoyafanya akiwa na klabu ya AC Milan ambayo aliitumikia kwa miaka 25 toka alipopata nafasi kwa mara ya kwanza kuichezea klabu hiyo akiwa ana miaka 17.

Alistaafu soka akiwa ana miaka 42 lakini kutokana na heshima aliyoijenga klabuni AC Milan, klabu hiyo iliamua kuistaafisha namba ya jezi aliyokuwa anaitumia mlinzi huyo, namba 3 hivyo haitokuja kutumika tena kwa mchezaji yoyote labda litokee la kutokea huko baadae.

Maldini akiwa ni raia wa Italia, aliisaidia timu yake ya Italia kufanya makubwa katika soka la ulimwengu huu akiwa sehemu ya kikosi kilichoshiriki michuano ya Ulaya mara tatu na Kombe la Dunia katika vipindi vinne.

9. Michel Platini

Rais wa zamani UEFA, Mitchel Platini ambaye alifungiwa kwa kukutwa na kashfa ya ufisadi naye ni mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kutokea duaniani.

Akiwa na kikosi cha Ufaransa, mshindi huyo mara tatu wa Ballon d’Or kwenye miaka ya 1983, 1984 na 1985, alifunga mabao tisa, ukijumuisha na yale matatu ‘hat trick’ aliyofunga kwenye michezo miwili tofauti zilizoifanya taifa lake kuchukua taji la Ulaya, 1984.

10. Cristiano Ronaldo

Nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo ambaye naye anashikilia tuzo nne za Ballon d’Or , akiwa na Real Madrid mbali na kushinda mataji kadhaa aliweka rekodi ya kufunga zaidi ya mabao 50 ndani ya misimu sita mfululizo.

Advertisement