Pierre Liquid kuwafundisha kina JB, Steve Nyerere kupanda Mlima Kilimanjaro

Saturday October 12 2019

 

Siku chache baada ya baadhi ya wasanii kushindwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro, mchekeshaji maarufu, Pierre Liquid, amewashangaa walioshindwa kumaliza safari.

Huku akicheka, Liquid, ambaye jina lake halisi ni Peter Mollel, alisema akipata nafasi atawafundisha wasanii walioshindwa kupanda Mlima Kilimanjaro kwa sababu atafika kileleni.

“Kupanda mlima mrefu kama ule si maigizo, ni maandalizi. Nikipata nafasi nitawafundisha jinsi ya kuukabili, nitajipanga mapema,” alisema.

“Kwanza sitakunywa pombe kwa wiki nzima, push up itakuwa ndiyo mapumziko yangu. Haya mambo hayahitaji majigambo, yanahitaji kujipanga. Lazima nifike kileleni.”

Pierre, ambaye amejizolea umaarufu kutokana na vibwagizo vyake kama “Mama Nakufa”, “Hiyoo” na ‘“Utabaki Kuwa Juu”, alisema siku zote mlima hauna ujanja na alikuwa anashangaa jinsi walivyokuwa wakisema wataupanda mara saba.

“Mimi kwetu Iringa kuna milima nina uzoefu nayo kidogo japokuwa si mirefu kama ulivyo Mlima Kilimanjaro,” alisema.

Advertisement

“Pia kwa wasiojua, mimi pamoja na kunywa kwangu pombe huwa nafanya sana mazoezi na ni mchezaji mzuri wa kareti, hivyo nipo fiti kuliko mnavyofikiria.”

Alisema ataonyesha mfano wa uzalendo kwa kufika kileleni.

Advertisement