Pierre katika ubora wake

Muktasari:

Awali kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jokate hakusita kutoa shukrani zake kwa kitendo kilichofanywa na Pierre ambapo aliandika, ”Ahadi imetimia leo nimepokea madawati yenye viwango vya juu kutoka kwa Pierre Liquid.

Pierre Liquid maarufu kwa vibwagizo vya kama ‘utabaki kileleni’, ‘mama nakufaa’,’chiii’ na ‘hiyooo’ ameahidi kuendelea kuisaidia Kisarawe katika masuala mbalimbali kama njia ya kuunga juhudi za mkuu wa wilaya hiyo, Jokate Mwegelo za kuwaletea wananchi wake maendeleo.

Kauli hiyo ya Pierre ambaye jina lake halisi ni Peter Mollel, inakuja ikiwa ni siku moja tangu atoke kukabidhi madawati 20 kwa kushirikiana na kampuni ya Afro Furnishers and Hardware, ambayo yeye ni mmoja wa wabia wake baada ya kuahidi kuchangia Sh100,000 Machi 30 mwaka huu kwenye harambee ya ‘Tokomeza Ziro’ iliyoandaliwa na Jokate ili kuinua kiwango cha ufaulu wilayani Kisarawe.

“Sisi Watanzania tunapaswa kusaidiana na kupendana bila kujali uwezo ulionao na mimi kama Perre nimevutika kufanya kazi za kijamii na ninaona zina thawabu hata kwa Mwenyezi Mungu.

“Kikubwa wanafunzi tunawahangaikia wajitahidi kusoma na kujiuliza kwa nini watu waache kuwasaidia watu wengine wawasaidie wao.

“Pia katika kuweka msisitizo napanga siku nikazungumze nao ana kwa ana kama njia ya kuwapa moyo wa kujituma kusoma na hatimaye kufaulu na kufanikisha ndoto zilizowapeleka shule, nilipoenda kukabidhi madawati sikufanikiwa kuwaona,” alisema Pierre ambaye watu walimpachika jina la mlevi wa Taifa, huku mwenyewe akilikataa na kusema yeye si mlevi bali ni mnywaji.

Awali kupitia ukurasa wake wa Instagram, Jokate hakusita kutoa shukrani zake kwa kitendo kilichofanywa na Pierre ambapo aliandika, ”Ahadi imetimia leo nimepokea madawati yenye viwango vya juu kutoka kwa Pierre Liquid.

“Kwenye Harambee yetu ya tarehe 30 Machi aliahidi kutoa laki moja lakini leo amekuja na madawati 20, nasema asante.”