Polisi wanavyozilenga Fainali za U-17

Tanzania itakuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika Aprili mwakani.

Fainali hizo zitashirikisha timu nane kutoka mataifa mbalimbali Afrika ikiwemo mwenyeji Tanzania, Angola, Uganda, Morocco, Cameroon, Senegal, Guinea na Nigeria.

Kutokana na uwepo wa mashindano hayo, Tanzania itanufaika kiuchumi katika nyanja mbalimbali ikiwemo usafiri,hoteli, utalii na wakalimani.

Kila eneo litakuwa na manufaa kwa eneo lake kutokana na kuguswa kwa njia moja ama nyingine. Zipo taasisi, mtu mmojammoja ama makundi ya watu yatanufaika lakini kati ya yote ni ulinzi na usalama kuimarishwa zaidi wakati wa mashindano.

USALAMA BARABARANI

Kitengo cha usalama barabarani licha ya kuwa na haki ya kuhakikisha usalama unakuwepo, lakini nao wanaweza kufaidika na uwepo wa mashindnao hayo.

Inavyosemekana mtu ukitaka kukodi pikipiki kwa ajili ya kukuongozea msafara kwenda sehemu yoyote ndani ya jiji la Dra es Salaam unatozwa sh 600,000,ingawa Kamanda wa kikosi cha Polisi Usalama barabarani, Kamishina Msaidizi(SACP) Fortunatus Muslim amesema hawatozi fedha yoyote kuongoza misafara ya shughuli za kitaifa kama hizo .

Anasema wamejipanga vizuri kuhakikisha timu zinafanya mizunguko mbalimbali bila bhuguza yoyote.

“Hayo ni mashindano ya kimataifa ambayo yanashirikisha nchi mbalimbali hivyo lazima tuhakikishe kwamba timu zinaweza kuzunguka sehemu mbalimbali bila tatizo.

“Kazi yetu ni kuhakikisha mizunguko ya timu kwenda mazoezini,kwenda kwenye mechi na kurudi hotelini inakuwa salama bila kikwazo chochote”anasema Muslim.

Aliongeza: ”Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) wameshaunda kamati mbalimbali za maandalizi ya mashindano hayo na mojawapo ya wajumbe ni kikosi cha usalama barabarani ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa.

Muslim alisema tayari wameandaa pikipiki maalumu kwa ajili ya kusindikiza timu muda wote watakaokuwepo hapa nchini kwa ajili ya mashindano hayo.

“Sisi Tunaendelea na maandalizi ikiwemo kuhakikisha tuna pikipiki za kutosha na tunachosubiri ni mashindano kufika muda wake na kupewa maelekezo timu zitafikia wapi,” alisema.

Kamanda Muslim anasema huwa hawatozi fedha yoyote kuongoza misafara ya shughuli za kitaifa kama hizo.

“Hayo ni mashindano ya kimataifa hatuwezi kutoza fedha kwa kuongoza misafara kwani hata ukiangalia pikipiki tunazotumia ni za serikali sasa kwa nini tutoze fedha?.

MAWASILIANO

Waongoza timu (liason officers) nao waula. Kunapotokea mashindano makubwa kama hayo huwa kunaibuka fursa kwa baadhi ya watu kunufaika kiuchumi.

Mojawapo ya watu hao ni waongoza timu ambao huwepo katika kila timu ili kuhakikisha mambo yanakwenda sawa ikiwemo kuwasiliana na wenyeji.

Mmoja ya watu waliowahi kuifanya kazi hiyo ni Joster Mwangulumbi anaelezea.

“Zinapokuja timu kutoka nje ya nchi lazima kuwepo na mtu anayeweza kuongea lugha ya sehemu husika na kujua sehemu mbalimbali ili kufanya mawasiliano ya wageni kuwa rahisi na jukumu la malipo huwa linafanywa na TFF.

“Mtu huyo huwapeleka wageni sehemu mbalimbali watakayotaka kwenda mfano kwenye maduka ya vifaa vya michezo,sehemu wanapouza nguo kwani wakati mwingine wanaweza kukuta vitu wanavyotaka ni bei ya chini kuliko kwao.

“Hata kule katika soko la mitumba la Ilala tumeshawahi kuzipeleka baadhi ya timu kununua vifaa mbalimbali,” anasema Mwangulumbi.

Katibu mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Wilfred Kidao anasema hakuna kiwango maalumu cha fedha wanachowapa wakalimani bali hugharamiwa chakula na malazi.

“Safari hii tunawahitaji kwa wingi watu kama hao kutokana na ukubwa wa mashindano yenyewe ili kutusaidia kuanzia uwanja wa ndege,viwanjani,kuhudumia chakula na mambo mbalimbali mengine.

“Ila kikubwa kwanza watu kama hao huwa wanakuwepo katika timu shiriki kuanzia mwanzo wa mashindano hadi mwisho wakipewa chakula na malazi kwa lengo la kuzisaidia timu kimawasiliano katika sehemu mbalimbali wanapokwa .

“Ni ngumu kusema moja kwa moja huwa tunawalipa kiasi gani kwani bado tunajipanga kuiona jinsi gani tutawawezesha kulingana na ukubwa wa mashindano yenyewe.

USAFIRI

Kutokana na timu hizo kuhitaji usafiri wa kuzipeleka mazoezini na kwenye mechi baadhi ya wamiliki wa mabasi watapata dili katika mashindano hayo.

Wenye mabasi kama Coaster watanufaika zaidi na uwepo wa mashindano hayo hapa nchini kwani mabasi hayo yatatumika kuzibeba timu kwa siku zote za mashindano ikiwemo kuzipeleka uwanjani kwenye mechi au katika mazoezi

Mmoja wa madereva wa mabasi ya Coaster maeneno ya Kinondoni,Rashid Seif anasema kwa siku mtu akitaka kukodi usafiri kwa safari za ndani ya jiji la Dar es Salaaam wanaweza kumtoza 200,000 hadi 300,000 lakini inaweza kuwa pungufu ya hapo kutokana na makubaliano yao.

Pia baadhi ya wenye magari madogo aina ya Noah nao wanaweza kukumbukwa kwani magari hayo mara nyingi huwabeba waamuzi, viongozi na makocha wa timu.