Profesa Omari: Waziri asiwe na nguvu kuamua sera za elimu - VIDEO

Tuesday April 16 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Msomi nguli wa elimu nchini Profesa Issa Omari ametilia nguvu haja ya kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu elimu, akisema Watanzania wanahitaji mwelekeo mmoja wa elimu utakaoamuliwa na wengi

Alisema mjadala huo unaopaswa kufanyika angalau mara moja kwa mwaka, unapaswa kugusia maeneo mengi ikiwamo kuachana na utaratibu wa waziri wa elimu kuwa na nguvu kubwa ya uamuzi wa katika masuala ya sera ya elimu.

Kwa nyakati tofauti marais wastaafu waligusia haja ya kuwapo kwa mjadala kuhusu mustakabali wa elimu nchini.

Novemba 11, 2017, Rais wa Serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya kuutafakari upya mfumo wa elimu na kushauri kuanzishwa kwa mjadala utakajumuisha makundi mbalimbali.

Alitoa kauli hiyo katika kongamano la wanataaluma lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Aprili 18, 2018, Rais aliyemfuatia Jakaya Kikwete akagusia suala hilo alipokuwa akizungumza katika kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Havard cha nchini Marekani.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi Profesa Omari aliyewahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 30, alisema Taifa limekosa dira ya elimu ndio maana kila waziri anakuja na sera zake.

‘’ Nafahamu waziri anayo mamlaka na ndiyo maana wakati mwingine yanatumika vibaya. Imekuwa kawaida kila mmoja akija anakuja na sera zake, badala ya sera ya elimu kuwa moja,’’ alisema na kuongeza:

‘’Mijadala kama niliyozungumzia hapo awali ndiyo itakayotumika kupinga mabadiliko ya sera ya kila mara; tunahitaji kuwa na sera ya elimu ya taifa ambayo ni moja kwa mawanda mapana ya elimu.’’

Swali: Eneo jingine linalozungumzwa sana na wadau juu ya hatima ya elimu ni kuhusu lugha inayofaa kutumika kama lugha ya kufundishia shuleni na vyuoni kati ya Kiswahili na Kiingereza. Upi mtazamo wako?

Jibu: Nikiangalia kwa mtazamo wangu, sijaiona na hakuna sababu ya kielimu au kimaendeleo inayosababisha kuwapo na wazo la kubadili lugha ya kufundishia kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili. Hatuwezi kuwa na elimu bora kwa sababu ya kubadili lugha ya kufundishia kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili. Na tukibadili ni lazima kama nchi ijiandae kushuka kielimu kwa kiasi kikubwa.

Vitabu vyote vya ziada na kiada vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, hivyo kuvitafsiri viwe kwenye Kiswahili vitachukua muda inawezekana miaka 10. Katika kipindi hicho cha mabadiliko lazima elimu itashuka sana, walimu na wanafunzi watayumba hususani wa elimu ya juu.

Lugha ya kufundishia siyo kikwazo cha mafanikio ya masomo kwa mwanafunzi mwenye nia, leo kuna magari kwa baadhi ya shule, walimu bora, vifaa vya kisasa vya kusoma na kujifundishia, teknolojia, maabara za kutosha na mabweni ya kuishi kama upo Ulaya, lakini kuna wanafunzi wanafeli kwa sababu wanataka kila kitu watafuniwe na jamii imelikubali hilo.

Swali: Nje ya ubora wa elimu kuna athari nyingine unayoiona ya kutumia Kiswahili?

Jibu: Kuna madhara yatakayopatikana ikiwamo kukosa fursa za ajira katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.Kutokana na kutojua lugha vizuri wafanyakazi wanachukuliwa Rwanda, Kenya Uganda na Zimbabwe; hawachukuliwi hapa nchini.

Kiingereza ni lugha ya ulimwengu, hivyo kuacha kukitumia inamaanisha Watanzania hasa vijana watakosa nafasi ya kufanya kazi kwenye ulimwengu wa leo. Hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kusema Kiingereza ni lugha ya ulimwengu siyo ya Uingereza.

“Hakuna teknolojia inayotumia lugha ya Kiswahili, unapozungumzia ulimwengu wa dijitali ambao tupo sasa ni Kiingereza , watoto wetu wakijifunza Kiswahili tutakuwa tumewaandaa kuachwa nyuma katika mambo haya.

Swali: Wewe ni msomi bobezi katika fani ya elimu na ualimu. Ungekuwa na mamlaka kama yale ya waziri wa elimu, unadhani nini ungefanya kuboresha sekta ya elimu?

Jibu: Kwanza nitaondoa ubaguzi katika elimu kwa maana watoto, vijana wapate elimu sawa bila kuwatenga kwa umasikini wao. Nadhani hili ndilo suala linalokosekana; kumekuwapo na ubaguzi mkubwa kwani watoto kutoka familia masikini wanaendelea kuwa masikini kwa sababu ni wachache wanaomaliza shule na kupata stadi za maisha. Wengi wanaishia mitaani.

Ukiangalia watu wa umri wa miaka 16-18 wanaotakiwa wawe sekondari wapo mitaani wanauza mahindi, sigara, nyanya na wote hawatoki kwenye familia za kitajiri ambazo angalau zina wasomi wawili, watatu.

Serikali imejitahidi elimu ya msingi wanafunzi wanakwenda kwa asilimia 99, lakini sekondari wanapungua na kufikia asilimia 35-40, kidato cha sita wanapungua kabisa na kufikia asilimia nne. Ukifika vyuo vikuu ni ndiyo maajabu kabisa wanaokwenda ni asilimia 3.5 au asilimia 4 ambao wana umri kati ya miaka 18 hadi 24.

Wenzetu Kenya wanaokwenda elimu ya juu wapo kwenye asilimia 7, Malaysia asilimia 15. Ghana walipokuwa wakibadili uchumi wao walikuwa kwenye asilimia 10, sasa uchumi umekua inawezekana hata idadi imeongezeka.

Tusijidanganye taifa lolote ambalo watu hawakusoma na kufika ngazi ya chuo kikuu, kupata maendeleo ni ndoto, kwa sababu hawajui nchi nyingine zinafanikiwa vipi. Hata huo uchumi wa viwanda unahitaji wasomi wa vyuo vikuu angalau wenye shahada ya kwanza.

Swali: Tunaweza kuwa na watu wengi waliosoma na hata sasa wapo hao wachache lakini hakuna ajira. Hili unalizungumziaje?

Jibu: Dhana ya wasomi kukosa ajira, hilo siyo jambo la kujadili kabla ya kusoma, ni suala la kujadiliwa baadaye. India walipoulizwa watawapatia wapi kazi watu wao wanaowafundisha kwa wingi shahada ya uzamivu, wakajibu tutawafundisha wengi zaidi ya hawa. Walipohitimu wengi wakaja kupata kazi ‘Silicon valley’ (eneo lenye kampuni nyingi za masuala ya teknolojia) huko California Marekani. Eneo hilo ndio kitovu cha teknolojia ya Marekani; walifanya kazi na kujikuta wametengeneza eneo lao nyumbani kwao na sasa Wamarekani wanakwenda kufanya kazi ‘Silicon Valley’ ya Bangalore India.

Siyo lazima kila wakati mhitimu anapomaliza shahada afanye kazi nzuri kama niliyofanya mimi. Wapo watu walikuwa wanasoma chuo kikuu cha Havard, lakini usiku wanaendesha teksi; muhimu ilikuwa kusoma kwanza.

Swali: Nini maoni yako kuhusu sekta ya elimu kuwa chini ya mamlaka zaidi ya moja ya usimamizi?

Jibu: Hilo ni tatizo. Mgawanyiko wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, masuala mengine ya elimu kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), hii ni shida.

Mapendekezo yangu wizara iwe moja na iwe na sauti moja, hivi sasa kila mmoja ana lake, hawa wanasema hivi na wale wanasema vile.

Advertisement