Punguzeni daladala stendi Morogoro imeelemewa

Usafiri wa daladala umekuwa ukitumiwa na watu wengi wakiwamo wafanyakazi na wanafunzi na unaonekana ni wenye gharama nafuu licha ya kuwa na changamoto nyingi.

Kukua kwa Manispaa ya Morogoro sambamba na ongezeko la watu kunafanya usafiri wa daladala kuwa ni huduma muhimu zaidi. Hata hivyo miundombinu ya vituo vya daladala bado si ya kuridhisha.

Mbali na kuwapo vituo vya njiani kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria, mbiundombinu yake hairidhishi licha ya manispaa kuchukua ushuru kwa kila daladala inayoingia kwenye vituo hivyo.

Vituo hivyo ni kile cha mjini kati ambacho kutokana na wingi wa daladala zinazoingia hapo kinaonekana kuwa finyu na hivyo kimekuwa kisababisha msongamano mkubwa wa magari.

Pamoja na ufinyu wa kituo hicho lakini pia mvua kubwa inaponyesha sehemu ya kituo hicho hugeuka bwawa linalotokana na kuziba kwa mifereji iliyozunguka kituo hicho. Jambo hili ni hatari kwa afya za abiria.

Miaka michache iliyopita kituo hicho cha mjini kati kilionekana kuelemewa na hivyo manispaa iliamua kutumia eneo la wazi la Kaloleni kuwa kituo cha daladala zinazokwenda nje ya mji ili kupunguza msongamano wa magari katika kituo cha mjini kati.

Hata hivyo, kituo hicho nacho hakitoshelezi wingi wa daladala zinazoegeshwa hapo kwa kuwa kimewekwa katikati ya makazi ya watu na jirani na Kituo cha afya Mji Mpya na hivyo kuzua usumbufu.

Uchache wa vituo vya daladala Morogoro linaweza lisiwe tatizo lakini ufinyu wa maeneo ya vituo vilivyopo ndio inaonekana kuwa changamoto ambayo inahitaji utatuzi wa haraka.

Kila kukicha daladala zinazofanya safari ndani na nje ya manispaa hii zinaonekana kuongezeka na hivyo kusababisha madereva wa daladala kushusha au kupakia abiria nje ya kituo jambo ambalo ni kosa kisheria lakini hawana namna ya kufanya.

Umefika wakati sasa manispaa ya Morogoro kupanua, kurahisisha na kuboresha huduma ya usafirishaji kwa njia ya daladala kwa kuwa Morogoro inakua kwa kasi, hivyo ongezeko la daladala nalo linakuwa kubwa.

Kwa hali inayoonekana sasa kwenye kituo cha daladala cha Mjini Kati Serikali inapaswa kutafuta eneo jingine kujenga kituo kikubwa zaidi.