Rita Paulsen:Msinilazimishe kumsaidia Casian ,hanidai tulishamalizana

Muktasari:

  • Casian ambaye kwa sasa ni msanii wa injili anaumwa kwa kipindi cha miezi minane sasa akiuguza majeraha ya ajali aliyoyapata Oktoba 10, 2018.

Mwandaaji wa shindano la Bongo Star Search (BSS), Rita Paulsen amesema siyo lazima amsaidie Pascal Casian kwa sababu hawadaiani.

Mwanamama huyo amesema hayo baada ya kuwapo kwa shinikizo mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari la kumtaka amsaidie matibabu Casian ambaye ni mshindi wa BSS mwaka 2009.

Casian ambaye kwa sasa ni msanii wa injili anaumwa kwa kipindi cha miezi minane sasa akiuguza majeraha ya ajali aliyoyapata Oktoba 10, 2018.

Katika ajali hiyo nyota huyo alipasuka kibofu cha mkojo, hivyo kuhitaji kiasi cha Sh25 milioni kwa ajili kwenda kutibiwa India.

Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Rita anasema amevumilia vya kutosha kusikia lawama na shinikizo kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka amsaidie matibabu Casian.

“Watu wanadhani ni lazima nimsaidie, kisa alipita kwenye shindano la BSS. Kimsingi Casian hanidai, nilishamalizana naye miaka tisa iliyopita,” anasema Rita.

“Kumsaidia kupata tiba ni hiari yangu nashangaa watu wanavyonilazimisha kufanya hivyo, nimemsaidia sana kama kijana wangu hata alipokuwa mzima akitaka kwenda nje ya nchi kwa shughuli zake, tubadilike siyo lazima kwa sababu ulifanya kazi na mtu anapopata matatizo umsaidie wewe, wapo wengi wanaoweza kutoa msaada huo.”

Rita anasisitiza kuwa yeye siyo mtu tajiri kwamba akitakiwa kutoa milioni kadhaa anazipata kwa urahisi.

Anasema kuwa anayo majukumu ya kifamilia na fedha zinazohitajika kwa matibabu ya Casian ni nyingi.

“Suala hili lisichukuliwe linanihusu mimi tu hata lile shindano la BSS linalowafanya watu waamini nina fedha nyingi nawategemea wadhamini, sina fedha, anayeweza kumsaidia afanye hivyo, ”anasema Rita maarufu kama madam Rita.

Casian kupitia vyombo vya habari amekuwa akimuomba Rita amsaidie mara kwa mara kwa madai kuwa ni miongoni mwa watu anaowategemea kufanya hivyo.

“Sijui Rita amekwama wapi maana alikuwa ni miongoni mwa watu wanaotaka kunisaidia kwenda nje kutibiwa, gharama za matibabu ya kibofu ni Sh25 milioni,” aliliambia Mwananchi lililotaka kujua hali yake kwa sasa.