Rwanda yapiga marufuku raia wake kuoa, kuolewa Burundi

Muktasari:

Ni mgogoro wa pili ambao Rwanda imeingia ukiacha wa Uganda ambao Rais Kagame amedai kwamba wanashirikiana na waasi wanaompinga

Kigali, Rwanda. Jeshi la Rwanda limepiga marufuku wananchi wa nchi hiyo kuoa au kuolewa nchini Burundi.

Pia Jeshi hilo limewataka wananchi wake wanaoishi jirani na mpaka kati ya nchi hiyo na nchi ya Burundi kusitisha biashara yoyote na majirani zao hao.

Uamuzi huo ni wa siku chache baada ya Rwanda kuwakataza wananchi wake kwenda nchini Uganda. Rwanda inazishutumu nchi hizo kwa kusaidia makundi ya waasi yanayoipinga.

Wito wa kuwakataza wananchi wa maeneo ya mpaka baina ya Rwanda na Burundi kutokwenda nchini humo umetolewa na Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo Jenerali Mbarac Muganga.

Muganga alisema hayo wakati wa mkutano wa usalama baina yake na wananchi na viongozi wa maeneo ya mpakani upande wa Kusini Mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa Mujibu wa Shirika la Habari la BBC, Jenerali Muganga aliwataka wananchi hao kusitisha shughuli zote zinazoweza kuwalazimisha kwenda Burundi hata kama itakuwa ni kuoa au kuolewa na raia kutoka upande wa pili.

‘’Rwanda tunachimbiwa shimo, kila mnyarwanda anayekwenda huko anatupwa ndani, hii ni kwa mujibu wa taarifa za uhakika tulizo nazo. Hatutawashambulia nchini mwao kwani sisi tunalinda mipaka yetu,’’ alisema Jenerali Muganga.

Aliongeza “Rwanda tunajitosheleza kwa chakula ndiyo maana tunawasihi kutumia kile kidogo tulicho nacho.’’

‘’Kuna wengi pia wanaokwenda kuoa au kuolewa huko si kwamba tunataka kuvunja ndoa zenu lakini tunawasihi kusitisha safari za kwenda huko na vilevile kupunguza wageni mnaopokea kutoka huko kwa sababu wanakuja wakiwa na malengo mengine mengi,’’ aliongeza Jenerali Muganga.

Nchi hizo zinashutumiana kuunga mkono makundi ya waasi kutoka kila upande. Miaka mitatu iliyopita Burundi ilitangaza kusitisha biashara yake na Rwanda hasa mboga na matunda na pia kusitisha huduma ya mabasi ya abiria kutoka Rwanda.

Rwanda imekuwa na tahadhari kubwa kwenye mipaka yake kutokana na makundi mbalimbali ya waasi yanayotishia kuishambulia.

Sakata la Rwanda na Uganda

Jambo kubwa linalosikitisha kwa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni mgogoro kati ya Rwanda na Uganda uliofikia hatua ya kuzuiliana usafirishaji bidhaa baina ya nchi hizo.

Pia Rwanda ilishutumu Uganda kuwanyanyasa wananchi wake wanaokwenda ama kuishi nchini Uganda na pia kusaidia makundi ya waasi wanaotaka kuuangusha utawala wa Rais Paul Kagame.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Dk Richard Sezibera aliliambia gazeti la Serikali kwamba mazungumzo kati ya Rais Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda yaliyofanyika mwaka jana na kushirikiana na viongozi wengine wa juu serikalini yameshindwa kutatua mgogoro huo.

Burundi ilitumbukia kwenye mzozo mwingine wa kisiasa mwaka 2015, Rais Nkurunziza alipokataa kung’atuka baada ya kumaliza muhula wake na akaamua kuwania tena kiti cha urais.

Mwaka huo pia kulitekelezwa jaribio la kuipindua Serikali ya Nkurunziza ambalo halikufanikiwa.

Museveni amwandikia barua Kagame

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alimwandikia barua Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuhusu madai ya kuwepo waasi wa Rwanda nchini Uganda.

Vyanzo vya kuaminika vinadai kwamba Museveni alimwandikia Kagame barua hiyo, Machi 10, mwaka huu baada ya kukutana na raia wawili wa Rwanda ambao nchi hiyo inadai wanatokea kwenye kundi la waasi la Rwanda National Congress (RNC).

Raia hao ni Charlotte Mukankusi na mfanyabiashara Tribert Rujugiro Ayabatwa, anayemiliki miradi mingi mikubwa nchini Uganda na nchi nyingine.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, japokuwa Museveni alimwandikia Kagame barua kuhusu mazingira aliyokutana na watu hao, Rwanda imekuwa ikibadili habari hiyo na kudai kuwa Museveni anawaunga mkono waasi wa RNC.

Shirika la Habari la Rwanda la KTpress, lililo karibu na Serikali ya Rwanda, liliripoti tukio hilo likisema kwamba kuna ushahidi wa Rais Museveni kuliunga mkono kundi hilo la kigaidi ili kuiyumbisha Rwanda kupitia Uganda.

“Machi 1, 2019, mkuu wa diplomasia wa RNC, Charlotte Mukankusi, alikuwa jijini Kampala, akiwa huko alikutana na Rais Yoweri Museveni. Mukankusi alikuwa naibu wa Kayumba Nyamwasa wakati kiongozi huyo wa RNC alipokuwa balozi wa Rwanda nchini India,” lilisema KTpress.

Hata hivyo, gazeti la New Vision la Uganda limeona nakala ya barua ya Museveni aliyoiandika kwenda kwa Rais Kagame, Machi 10, 2019.

Katika barua hiyo Museveni amejitahidi kuelezea mazingira aliyokutana na Mukankusi.

Kwa mujibu wa New Vision, Museveni inadaiwa alisema kwamba Mukankusi alimtaka asaidie kulipiza kisasi cha kifo cha mumewe Rutagarama ambaye aliuawa na Serikali ya Rwanda, hata hivyo Museveni alimkatalia akisema kwamba asingeingilia masuala ya Rwanda.

Kuhusu Rujugiro, Museveni alidai kwamba mtu huyo alizungumza naye kuhusu masuala ya biashara zake nchini Uganda na kumwambia kwamba kama kulikuwa na matatizo mengine alimshauri ayapeleke kwenye mahakama za Uganda.

Awali Rais Kagame alielezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Akihutubia mkutano wa kitaifa Rais Kagame alisema kwamba mgogoro huo ulishika kasi miaka ya hivi karibuni kutokana na Serikali ya Uganda kuunga mkono kundi hilo la RNC.

Baadhi ya wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanaamini kwamba mgogoro baina ya Kagame, Museveni pamoja na Kagame na Nkurunzinza unaweza kuwa na madhara makubwa katika mustakabali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kagame na Museveni

Rais Kagame, alipata mafunzo ya kijeshi katika mataifa tofuati ikiwemo nchini Uganda na Tanzania yaliyomfanya kuonekana kama mpanga njama mzuri wa kijeshi.

Ameishi kama mkimbizi nchini Uganda kwa miaka mingi akiwa mfuasi na muasisi wa jeshi la waasi la Rais Yoweri Museveni.